Washtakiwa wa ‘unga’ waihoji Serikali, wajibiwa

Dar es Salaam. Washtakiwa tisa wanaokabiliwa na kesi ya kusafirisha kilo 332 za heroine na methamphetamine, wamehoji upande wa mashtaka uwaeleze upelelezi wa kesi yao umefikia asilimia ngapi.

Washtakiwa hao ni mvuvi wa samaki Ally Ally (28) maarufu Kabaisa, Bilal Hafidhi (31) ambaye ni mfanyabiashara; Mohamed Khamis (47) Mvuvi wa samaki na  Idrisa Mbona (33) ambaye ni  muuza magari.

Wengine ni Rashid Rashid (24) Beach Boy na mkazi wa Ubungo Maji; Shabega Shabega (24) mbeba mizigo na mkazi wa Saadan Kasulu.

Pia, yupo Dunia Mkambilah (52) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Madale Kisauke;  Mfanyabiashara Mussa Husein (35)mkazi wa Mwambani na Hamis Omary (25).

Washtakiwa hao wametoa hoja hiyo leo Alhamisi Februari 20, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kabaisa na wenzake wamefikia hatua hiyo, baada ya wakili wa Serikali Roida Mwakamele kuieleza Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo, haujakamilika.

Mwakamele ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini, anayesikiliza kesi.

Kufuatilia hali hiyo, wakili wa washtakiwa hao, Hassan Rugwanya, amedai wateja wake wamekuwa ndani muda mrefu kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana.

“Upande wa mashtaka tunaomba angalau watueleze upelelezi wa kesi hii umefikia asilimia ngapi,” amehoji wakili Rugwanya.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Mwakamele amedai hawezi kujua upelelezi umefikia asilimia ngapi, isipokuwa atafuatilia kujua upelelezi umefikia hatua gani.

Hakimu Mhini baada ya kusikiliza hoja za pande zote ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 6, 2025 kwa kutajwa.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na kesi inayowakabili haina dhamana.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Aprili 16, 2024 karibu na Hotel ya White Sands, iliyopo wilaya ya Kinondoni, wanadaiwa kusafirisha kilo 100.83 za dawa aina ya methamphetamine, kinyume cha sheria.

Shtaka la pili, siku na eneo hilo, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 232.69 za heroin, kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Aprili 22, 2024 wakikabiliwa na mashtaka hayo.

Related Posts