Tanzania kuwakutanisha wadau 300 duniani Jukwaa la Utalii wa Chakula

Dar es Salaam. Tanzania itakuwa mwenyeji wa jukwaa la pili la utalii wa vyakula wa Shirika la Utalii Duniani Kanda ya Afrika litakalofanyika jijini Arusha.

Jukwaa hilo ambalo litafanyika kuanzia Aprili 23 hadi 25, 2025, litawakutanisha wadau zaidi ya 300 kutoka nchi mbalimbali za Afrika na duniani sambamba na viongozi wa ngazi za juu katika sekta ya utalii na ukarimu, watumishi wa serikali na wataalam wa vyakula.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja na Sekretarieti ya Shirika la Utalii Duniani na  waandishi wa habari leo Alhamisi Februari 20, 2025 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Pindi Chana amesema Tanzania ilichaguliwa kuwa nchi mwenyeji wa jukwaa hilo katika jukwaa la kwanza la Utalii wa Vyakula barani Afrika lililoratibiwa na Shirika la Utalii Duniani Kanda ya Afrika lililofanyika Victoria Falls, Zimbabwe tarehe 26 hadi 28 Julai, 2024. Amesema uamuzi huo ulitokana na ombi la Tanzania kuandaa jukwaa hilo kutokana na hazina kubwa ya urithi wa utamaduni na vyakula vya asili kutoka kwa jamii mbalimbali zilizopo nchini.

Waziri huyo amesema tukio hilo linaandaliwa kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) pamoja na Basque Culinary Center.

“Jukwaa hili linalenga kuangazia uhusiano muhimu kati ya utamaduni wa upishi na utalii na kufanya tathmini ya jukumu muhimu la utalii wa vyakula katika kukuza maendeleo ya kiuchumi, kuhifadhi urithi wa utamaduni na kukuza jamii kiuchumi,” amesema.

Amesema mkutano huo utahusisha matukio mbalimbali ikiwemo maonesho ya mapishi ikiwashirikisha wapishi wa mashuhuri na vipaji vya ndani, kuonja aina tofauti za vyakula na vinywaji, mijadala ya jopo na mawasilisho itakayoainisha fursa mpya katika utalii wa vyakula na jinsi unavyoweza kunufaisha uchumi na jumuiya za wenyeji.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika, Elcia Grandcourt amesema Shirika la Umoja wa Mataifa liko tayari kuandaa jukwaa hilo muhimu litakaloleta ladha ya vyakula mbalimbali kutoka katika Kanda ya Afrika na nchi nyingine duniani.

“Tayari nimeshajaribu baadhi ya vyakula vya Kitanzania kama nyama choma na ugali hivyo jukwaa hili litatuwezesha kupata uzoefu ambao Tanzania inayo katika utalii wa vyakula,” amesema Grandcourt.

Related Posts