Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC) Bara, Innocent Siriwa ametangaza ni ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 2025.
Siriwa ametangaza uamuzi huo, leo Alhamisi Februari 20, 2025 katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam akibainisha vipaumbele vitano atakavyovipambania endapo chama chake kitampitisha kuwania nafasi hiyo.
Sirima anakuwa mtu wa pili kutangaza nia kuwania nafasi hiyo akitanguliwa na Dorothy Semu wa ACT- Wazalendo ambaye ni Kiongozi wa chama hicho akisema amejipima na kujiona anastahili na kufaa kuwania urais.
Mbali ya Sirima na Dorothy, Chama cha Mapinduzi (CCM), kimekwisha mpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwania urais huku Dk Emmanuel Nchimbi ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho akipitishwa kuwa mgombea mwenza.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipitishwa kuwania urais huku Makamu wa Kwanza wa Rais visiwani humo, Othuman Masoud akitangaza nia ya kuwania urais kupitia ACT Wazalendo.
Katika tukio la leo Alhamisi, Sirima akitangaza nia hiyo amebainisha vipaumbele hivyo vitano ambavyo ni elimu bure, afya bure, Katiba mpya, ajira kwa vijana na Tanzania ya kidijitali.
“Nikipata nafasi ya kwenda kukiwakilisha chama nitahakikisha napambania Mtanzania apate matibabu bure ili kuokoa maisha yao. Kwa sasa maisha ya Mtanzania yapo mashakani kwa sababu anafanya kazi, lakini hana uhakika wa afya yake,” amesema.
“ADC tunakwenda kuhakikisha Mtanzania anapata matibabu, lakini ili apate matibabu hayo, lazima tuongeze uzalishaji utakaowezesha pato la Taifa kupanda,” amesema Siriwa.
Siriwa amesema anaamini wakitangaza sera ya matibabu bure, uzalishaji utaongezeka kwa sababu Watanzania watakuwa na uhakika na afya zao.
“Mtanzania atafanya kazi kwa juhudi na maarifa akijua Serikali yake inamjali. Serikali itakayoongozwa na ADC itatoa matibabu bure,”amesema Siriwa.
Kuhusu kipaumbele cha Katiba mpya, Siriwa amesema licha ya suala hilo, kuwa bado changamoto lakini ADC inashiriki uchaguzi ili kupata madiwani, wabunge watakaosukuma ajenda hiyo.
“Ajenda ya ADC ni Katiba mpya kama Watanzania wanahitaji basi tunawaomba waridhie kutuchagua ili twende na ajenda hii. Tunawaomba Watanzania watuchague kwa sababu ajenda yetu ni Katiba mpya pia ili tulete mabadiliko,” amesema Siriwa.
Siriwa amesema kumekuwa na ombwe la vijana kutokuwa na ajira, lakini endapo ADC ikifanikiwa itahakikisha inakwendea kuziba pengo hilo.
“Wakati umefika wa kumchagua Innocent Gabriel Siriwa ili awe Rais wa Tanzania atakayekwenda kusimamia sera hii ya kutengeneza ajira kwa vijana. Tunatengenezaje ajira, hili ni suala la kimkakati ambapo lazima tutengeneze mikakati ya kutosha itakayohakikisha vijana wanapata ajira wanapomaliza masomo,”amesema Siriwa.
Siriwa amesema ADC itaanzisha kilimo kitakachowekewa utaratibu mzuri ili kuwawezesha vijana kushiriki.
Amesema watahakikisha vijana wanapata ajira katika sekta za viwanda na madini.
Amefafanua Serikali ya ADC itahakikisha kila shule inakuwa na umeme utakaotokana na vyanzo mbalimbali ikiwamo ya nishati ya jua.
Kwa mujibu wa Siriwa, masilahi ya walemavu katika Serikali ya ADC yatapewa kipaumbele ili kuimarisha hali za maisha zao ikiwamo kuwapa mishahara.
“Akionekana anaomba tutamuuliza mshahara wake anapeleka wapi? Kwa nini uombe wakati unapata mshahara wako, kila mlemavu kuanzia miaka sifuri na kuendelea,” amesema Siriwa.
Mwenyekiti wa zamani wa ADC, Hamad Rashid amesema wanamuunga mkono Siriwa katika hatua hiyo, huku akihimiza ujenzi wa demokrasia katika vyama vya siasa.
“Tukijenga demokrasia katika vyama vya siasa wananchi na Serikali watatuelewa. Wakati mwingi tumekuwa tukiinyoshea kidole zaidi Serikali kwamba haifanyi hiki na hiki, bila kuangalia vidole vitatu vinavyotutizama sisi,” amesema.
“Kila wakati nasisitiza sana ili kuibana Serikali, lazima vyama vya siasa vijitahidi kuhimiza demokrasia. Tukifanya hivi wananchi watajenga imani na Serikali itakuwa na tahadhari kubwa kuvunjwa misingi ya demokrasia,” amesema Rashid.