Dar/Dodoma. Siku moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi, kueleza kuhusu mbinu mpya za rushwa zinazotumiwa na baadhi ya makada wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imekiri kuwa na taarifa hizo na inazifanyia kazi.
Juzi, Dk Nchimbi alieleza kuwapo kwa vitendo vya rushwa majimboni na kwenye kata, huku akiwaonya makada wa chama chake wanaotumia mbinu mpya kusaka ubunge na udiwani, akisema wakibainika watakatwa.
Dk Nchimbi alisema mbinu hizo mpya zinazotumiwa na makada hao ni pamoja na kufanya sherehe za kumbukizi za kuzaliwa, vifo vya ndugu zao, na ndoa huku wakigawa fedha kwa waalikwa.
Akizungumzia kauli ya Dk Nchimbi kuhusu mbinu hizo za rushwa kuelekea uchaguzi mkuu baada ya kuzungumza na Mwananchi kwa simu leo, Alhamisi, Februari 20, 2025, Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, amekiri kwamba wana taarifa hizo ambazo wamezipata kutoka maeneo mbalimbali na zinafanyiwa kazi.
“Tunakusanya ushahidi unaojitosheleza na usio na shaka ili kuchukua hatua stahiki za kisheria na za kiutawala, na kwa kuwasiliana na mamlaka zao kwa zile ambazo hazitakuwa na ushahidi unaojitosheleza,” amesema.
Wakati Takukuru wakieleza hayo, wadau wa siasa nchini wameunga mkono kauli ya Dk Nchimbi kuhusu vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2025 huku wakitaka hatua zaidi zichukuliwe dhidi ya wahusika.
Wadau hao wametaka chama hicho kiwadhibiti wote wanaojihusisha na vitendo hivyo. Pia, wametaka kamati za maadili za chama hicho, kuanzia ngazi za chini mpaka juu, kuchukua taarifa za matukio hayo na kuziwasilisha ngazi za juu.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amepongeza hatua zilizoanza kuchukuliwa na CCM katika mapambano dhidi ya rushwa kwenye uchaguzi.
Jaji Warioba ametoa pongezi hizo akirejea mabadiliko ya Katiba ya CCM yaliyofanywa na mkutano wake mkuu maalumu uliofanyika hivi karibuni.
Miongoni mwa marekebisho hayo ni pamoja na namna ya kupata wagombea wa udiwani, uwakilishi na ubunge, kwa kuongeza idadi ya wapigakura wa vikao vya kura za maoni.
Amesema kwa kuwa vita dhidi ya rushwa si ya siku moja, CCM haina budi kuhakikisha mapambano ya kumshinda adui huyo yanakuwa endelevu kwa kusimamia misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho.
Warioba ametoa kauli hiyo leo katika mazungumzo yake na Dk Nchimbi alipomtembelea nyumbani kwake, jijini Dar es Salaam, kumjulia hali.
Amesisitiza sifa na miiko ya uongozi ilivyoainishwa kwenye Katiba ya CCM, akisema chama kina wajibu wa kuendelea kuwapatia matumaini Watanzania kwa kutoa uongozi bora kwa mwelekeo sahihi wa nchi.
“Hivi mlivyoanza ni safi, in the long run (hatimaye huko mbele) tutakuwa na mwanga wa mapambano dhidi ya rushwa,” amesema Jaji Warioba.
Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa CCM kuendelea kusimamia misingi yake, ikiwemo ya ahadi za mwanachama.
Aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Kamati Maalumu ya CCM Zanzibar, Catherine Nao, amesema anaunga mkono kauli ya Dk Nchimbi kwa sababu ndiyo kitu kinachoendelea kwenye majimbo kwa sasa.
Amesema baadhi ya wabunge na wawakilishi hawajafanya lolote katika majimbo yao kwa miaka mitano iliyopita, lakini baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu hivi karibuni, wanaandaa mikutano na wanatoa zawadi kwa wanachama.
“Siyo tu wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, ongezea na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar; wanafanya hayo, tunawaona. Miaka minne mtu hajafanya lolote, lakini sasa wanajitokeza kwa wingi majimboni,” ameeleza.
Ameshauri kamati za maadili katika ngazi za chini zichukue hatua za awali kwa kuandika taarifa za matukio hayo yanayoendelea kwenye maeneo yao, huku akiwaonya wao wasiwe miongoni mwa wanaopokea hizo fedha.
“Tukianzia ngazi ya tawi kwa kuripoti matukio, taarifa hizo zipelekwe hatua kwa hatua hadi ngazi ya juu kwa hatua stahiki,” amesema.
Ameongeza kuwa, “Katibu Mkuu amesema tu hilo, lakini watekelezaji wa kuona haya mambo yanazuilika na hatua zinachukuliwa ni ngazi za huku chini. Wito wangu ni kwamba kamati za maadili za kila ngazi zifanye kazi yake, maana wanafanya matukio ya wazi, siyo ya kujificha.”
Nao, ambaye pia ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM, amesema wapo pia viongozi wa CCM kwenye mikoa wanaowapigia debe baadhi ya wabunge na kuwakatisha tamaa wengine kuwania nafasi hizo kwa madai kwamba wanatosha kugombea tena.
“Kama Katibu wa Mkoa ambaye ndiye Mkurugenzi wa Uchaguzi, au Katibu wa Wilaya anasema hivyo, hapo kuna nini kama siyo kuharibika kwa chama? Anasema anafaa sana huyu, ana uwezo huyu… kufaa na kutofaa siyo wewe kuamua, wewe ni Mkurugenzi wa Uchaguzi,” amesema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Madeni na Maendeleo Tanzania (TCDD) na mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Hebron Mwakagenda, amesema kwa kuwa CCM wana kanuni, wawadhibiti watu wanaofanya kampeni mapema na kutoa rushwa ili wachaguliwe.
“Ni kawaida katika ushindani, kila mtu anajitafutia nafasi ili apate yeye, lakini kuna mmoja nilimsoma anasema huko juu ndiko kumeanzisha huo mtindo, kwa hiyo hata nguvu ya kugomea huku chini ni ngumu. Kwa sababu kulikuwa na mgombea mmoja, kwa hiyo waliokuwa wakitaka wakashindwa.
“Ndiyo maana wanasema kwenye familia watoto muonyeshe mfano, ukionyesha watoto wanafuata. Kwa hiyo, hivyo vingine ni harakati tu za kushindania nafasi wapate, siyo cha ajabu sana. Kila mtu anafurukuta, ushindani ni mkali, atumie mbinu yoyote apate,” amesema.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo, amesema suala la kupinga rushwa ni jambo jema na hatua inayolenga kuwapata wagombea halisi watakaowatumikia wananchi.
“Suala hili linapaswa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa kwa sababu viongozi wenye kujitambua na waliopatikana kwa haki, ni wazi ndiyo watakaokuwa na uchungu na maendeleo ya wananchi. Lakini mtu akitoa rushwa, hatawajibika; atawaza atarejeshaje fedha zake alizohonga,” amesema Dk Masabo.
Amesema kinachopaswa ni utekelezaji wake ambao ndiyo utaleta picha halisi ya namna hali hiyo itakavyoshughulikiwa na watakaobainika wafikishwe mahakamani wakashtakiwe kwa mujibu wa sheria.
Mchambuzi wa siasa, Kiama Mwaimu, amesema onyo la Dk Nchimbi kwa makada wa CCM ni ngumu kutekelezeka kwa sababu si rahisi kutofautisha kati ya sherehe, msiba, au shughuli nyingine zenye mkusanyiko wa watu.
“Watu wakijikusanya, watafanya lolote linalowezekana ili kutumia mbinu zao za kugawa fedha. Siyo lazima fedha zitolewe taslimu, bali zinaweza kutumwa kwa njia ya simu,” amesema.
“Sidhani kama kauli ya Dk Nchimbi itaweza kuzuia. Sasa hivi ndiyo kumepamba moto. Kila mbunge yupo ‘busy’ jimboni, mara utawaona wanatoa fulana tena wanatumia kivuli cha ujio wa viongozi wakuu wa kitaifa wanaokwenda katika mikoa yao,” amesema Mwaimu.
Naye Rehema Mwangulupi, miongoni mwa wanafunzi wanaosoma Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema vijana wanafuata nyayo za wazee kwa sababu mambo hayo hayajaanza sasa kwa viongozi kutoheshimu demokrasia ndani ya chama chao.
“Watoto hufuata nyayo za wazee wao, mtoto hutizama kisogo cha mzee wake. Vyama vinapaswa kuheshimu demokrasia yao ndani ya chama, ofisi zenye dhamana zinatakiwa kukemea vyama vinavyokiuka taratibu zao,” amesema Mwangulupi.
Amesema vyama vinapofanya hivyo na Ofisi ya Msajili ikawa imekaa kimya, matokeo yake ndiyo hayo. Hivyo, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatakiwa kuchukua hatua dhidi ya mwenendo wa kuanza mchakato kabla ya kutangazwa.
Mchambuzi wa siasa, Iddi Kizota, amesema hashangai malalamiko hayo, labda kwa kuwa wamebadilisha mbinu za kutoa rushwa katika michakato ya uchaguzi.
Amesema ni vizuri kuchukua uamuzi kwa vitendo kwa kusimamia vema kanuni na utaratibu ili kuepuka kupata viongozi ambao wameingia madarakani kwa rushwa.
“Tumuombee Mungu (Dk Nchimbi) achukue hatua ili kupunguza tatizo hili, maana tukiwa na viongozi waliopatikana kwa rushwa ni hatari. Watajikusanyia mapato ambayo hayalingani na majukumu wanayoyafanya,” amesema.