Dar es Salaam. Uamuzi wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) uliotoa agizo kwa Tanzania kufuta adhabu ya kifo iliyotolewa kwa Ladislaus Chalula na kumwondoa katika orodha ya wanaosubiri kunyongwa, umechochea upya mjadala kuhusu mustakabali wa adhabu ya kifo nchini.
Hii si mara ya kwanza kwa mahakama hiyo kutoa uamuzi wa kuitaka Serikali ya Tanzania kufuta adhabu hiyo, iliwahi kufanya hivyo kwenye hukumu yake ya mwaka 2019 na kutaka utekelezaji ufanyike ndani ya miezi sita.
Hata hivyo, hukumu hiyo mpya ya Februari 5, 2025 ni mwendelezo wa hukumu kama hizo za kuitaka Serikali kuifuta adhabu ya kifo.
Wakizungumzia hukumu hiyo jana, wataalamu wa sheria na wanaharakati wa haki za binadamu wamehoji ikiwa Tanzania itazingatia maagizo ya mahakama hiyo, ikizingatiwa kuwa kumekuwa na historia ya kutotekelezwa kwa uamuzi kama huo na Serikali.
Maoni ya wataalamu hao yamezingatia uanachama wa Tanzania katika Mahakama ya Afrika, huku wakianisha rekodi kadhaa zenye mkanganyiko kuhusu utekelezaji wa uamuzi ya mahakama hiyo.
Wataalamu wa sheria wanasema uamuzi huu mpya unaipa Serikali mtihani mkubwa wa kuchagua njia ya kufuata.
Dk Emmanuel Ndyali, mtafiti wa masuala ya sheria, amesema ingawa Mahakama ya Afrika ni kimbilio la wale wanaotafuta haki nje ya mipaka ya kitaifa, ufanisi wake unadhoofishwa na Serikali zinazokaidi uamuzi yake.
“Tumeshuhudia kesi nyingi ambapo Tanzania na nchi nyingine za Afrika zimeshindwa kutekeleza uamuzi ya Mahakama hii. Swali ni kama Tanzania itabadilika safari hii na kutekeleza maagizo haya,” anasema.
Kesi hii itakuwa tofauti?
Wakili wa masuala ya katiba, Sarah Mwakapango anaamini kuwa agizo la kuondoa adhabu ya kifo ya lazima, linaendana na mwelekeo wa kimataifa wa haki za binadamu na linaweza kuwa fursa ya Tanzania kufanya mageuzi ya mfumo wake wa sheria.
“Hii si kesi ya mtu mmoja tu. Ni mwaliko kwa Tanzania kutathmini upya msimamo wake kuhusu adhabu ya kifo,” anaeleza Mwakapango.
“Nchi nyingi zimeachana na adhabu ya kifo, na Tanzania haijatekeleza hukumu ya kunyonga kwa miongo kadhaa. Huu unaweza kuwa mwanzo wa kufutwa kabisa kwa adhabu hiyo.”
Ingawa mamlaka za kisheria za Tanzania hazikupatikana kuzungumzia uamuzi huu, hukumu hii inaelezwa huenda ikawa mwanzo wa Tanzania kufuta adhabu ya kifo, ambayo kwa mara mwisho ilitekelezwa wakati wa utawala wa awamu ya pili, chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.
Mwinyi alikuwa Rais wa pili wa Tanzania kuanzia mwaka 1985 hadi 1995, baada ya Rais Mwalimu Nyerere.
Ugumu wa Tanzania kutekeleza adhabu hiyo umeanzia kwa marais, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli ambao hawakusaini utekelezaji wake kwa waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa.
Rais wa sasa Samia Suluhu Hassan yeye aliunda Tume ya Haki Jinai ambayo moja ya mapendekezo yake kwa Serikali ni kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini na kurekebishwa sheria kuhusu adhabu kifo.
Tume hiyo ambayo iliwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Julai 2023, inapendekeza sheria inayotoa adhabu hiyo irekebishwe.
Ilipendekeza Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, ifanyiwe marekebisho ili adhabu ya kifo isiwe adhabu pekee kwa kosa la mauaji, bali adhabu itolewe kulingana na mazingira ya utendaji kosa.
Pia, inapendekeza adhabu ya kifo isiporidhiwa na Rais kwa kipindi cha miaka mitatu, itenguke kuwa kifungo cha maisha.
Tume katika ripoti hiyo inabainisha adhabu hiyo imekuwa haitekelezwi kwa miaka mingi, hivyo kusababisha waliopewa adhabu hiyo kuishi maisha ya hofu, huku wakisubiri utekelezaji wa adhabu hiyo.
Kwa takwimu za Mei 2023, wafungwa wanaosubiria kunyongwa walikuwa 691.
Kilichofanywa na Magufuli
Rais wa awamu tano, hayati John Magufuli licha ya kuacha kusaini utekelezaji wa adhabu ya kifo, yeye alikwenda mbali kwa kubadilisha adhabu kwa baadhi ya waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na kuwa kifungo cha maisha jela.
Kwa mfano, wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 3,973 kati yao, 256 wakiwa ni waliohukumiwa kunyong’wa hadi kufa na aliwabadilishia adhabu.
Pia, Desemba 2017, hayati Magufuli aliwasamehe wafungwa 61 waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa.
Mbali na hivyo, Rais huyo alikuwa ameweka wazi msimamo wake juu ya utekelezaji wa hukumu ya kifo, akisema hawezi kusaini mfungwa yeyote aliyehukumiwa adhabu hiyo kwenda kunyongwa.
Mwaka 2017, wakati akimuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, Rais Magufuli alivunja ukimya kuhusu adhabu hiyo:
“Sisi wanasiasa tunaogopa kunyonga, natambua kwa sasa orodha ya watu ambao wanatakiwa kunyongwa ni kubwa sana, ila mimi naomba hiyo orodha msiniletee kwa sababu najua ugumu wake ulivyo,” alisema Rais Magufuli.
Kesi iliyosababisha mahakama hiyo kutoa hukumu hiyo ilianza mwaka 1991 wakati Chalula, raia wa Tanzania, alipohukumiwa kifo na Mahakama Kuu ya Tanzania iliyoketi Sumbawanga kwa kosa la mauaji.
Alikata rufaa katika Mahakama ya Afrika, akidai kuwa Tanzania ilikiuka haki zake kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu.
Mahakama ilibainisha kuwa adhabu ya kifo ya lazima inakiuka haki ya kuishi, na kwamba kunyongwa ni ukatili unaodhalilisha utu.
Ilitoa amri kwa Tanzania kumhukumu upya Chalula kwa mchakato usiohusisha adhabu ya lazima ya kifo, kuondoa kunyongwa kutoka katika kanuni zake za jinai, na kisha kuripoti utekelezaji wa hukumu hiyo ndani ya miezi sita.
Uamuzi kama huo huo ulitolewa pia Juni 4, 2024, Mahakama ya Afrika ikiagiza Serikali ya Tanzania kufuta adhabu ya kifo ya lazima katika sheria zake na kuipa miezi sita kutekeleza agizo hilo.
Agizo hilo lilitokana na rufaa iliyowasilishwa mahakamani hapo na Dominick Damian, mfungwa wa kifo dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hukumu yake, Mahakama kwa mara nyingine iliagiza Serikali kufuta adhabu ya kifo dhidi ya Dominick, ambaye amekuwa akisubiri kunyongwa katika Gereza la Butimba, mkoani Mwanza. Hata hivyo, hadi sasa, agizo hilo halijatekelezwa.
Mbali na hukumu ya Juni 4, 2024, pia Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) ilitoa hukumu nyingine kama hiyo kwa Serikali ya Tanzania.
Ilikuwa mwaka 2019 katika shauri la maombi namba 007 la mwaka 2015, lililofunguliwa na Ali Rajabu na wenzake wanne, dhidi ya Serikali ya Tanzania, ilipoamuru Serikali kufanya marekebisho na kuondoa adhabu ya kunyongwa kama sharti la lazima.
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Amnesty International hadi kufikia 2017, nchi 142 zilikuwa zimeacha kutoa hukumu ya kifo kisheria na/au kiutekelezaji.
Umoja wa Mataifa (UN) unakadiria kuwa nchi 170 zimeachana na adhabu hiyo kwa namna moja au nyengine.
Hata hivyo, baadhi ya nchi zimekuwa zinajiondoa uanachama wa Mahakama hiyo kwa kutokubaliana na hukumu zake.
Nchi ambazo zimejiondoa uanachama wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) ni Benin, Rwanda na Ivory Coast.
Pia, Tanzania mwaka 2019 ilitoa uamuzi wa kupiga marufuku watu binafsi kuifikisha moja kwa moja kwenye mahakama hiyo, hali iliyozua maswali kuhusu dhamira yake ya kuheshimu haki za binadamu.