Iringa. Wananchi wametahadharishwa kununua dawa za binadamu zinazouzwa kwenye vyombo vya usafiri na zile zinazotembezwa barabarani kwa kuwa ni duni na huleta madhara kwa mtumiaji.
Mara kadhaa dawa hizo zimekuwa zikiuzwa katika mabasi ya mikoani na hata daladala kwa madai kuwa zinatibu magonjwa mbalimbali.
Tahadhari hiyo imetolewa leo Alhamisi Mei 16, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba katika kikao kazi cha wahariri na Mamlaka ya Dawa na Vifaatiba (TMDA) mkoani Iringa.
Serukamba amesema tofauti na bidhaa nyingine, dawa na vifaa tiba ni nyeti na zenye madhara kiafya ikiwa hazitadhibitiwa ipasavyo na zinaweza kusababisha ulemavu, kupoteza maisha na kudhoofisha uchumi wa nchi.
Amesema Serikali haitamuonea huruma mtu yeyote atakayepatikana na dawa bandia kwa kigezo cha kutokujua wakati zinasababisha madhara kwa binadamu.
“Dawa zinahitaji kudhibitiwa kwa utaratibu wa pekee lengo likiwa ni kuzuia madhara kwa watumiaji. Katika kufikia lengo hilo bidhaa hizi zinahitaji kuhakikiwa usalama, ubora na ufanisi wake kabla ya kuruhusiwa kutumika, kazi inayosimamiwa na TMDA,” amesema Serukamba.
Pia, amesema baadhi ya majukumu ya mamlaka hiyo ni kuhakikisha afya za wananchi zinalindwa kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili bidhaa zilizopo sokoni kuwa salama na zenye ubora.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila bidhaa tiba 10 katika nchi zinazoendelea ulimwenguni, moja ni bandia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo amesema pamoja na jitihada za mamlaka hiyo kutoa elimu kwa jamii, bado uelewa wa wadau wakiwamo wananchi kuhusu shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo upo chini.
Fimbo amesema kiwango kidogo cha uelewa kimesababisha matumizi yasiyo sahihi ya dawa.
“Idadi ndogo ya wananchi wanaripoti maudhi ya dawa, baadhi ya wafanyabiashara huingiza dawa duni na bandia lakini wananchi hawazingatii tarehe ya kuisha matumizi ya dawa,” amesema Fimbo.
Amesema ili kufikisha elimu kwa wananchi, wamekuwa wakifanya kazi na vyombo vya habari kusambaza elimu kwa jamiii kuhusu kazi zinazofanywa na TMDA.
Mkurugenzi wa Udhibiti Dawa TMDA, Dk Yonah Mwalwisi amesema hakuna nchi duniani ambayo haina changamoto na bidhaa tiba bandia.
Hata hivyo, amesema wamekuwa wakitumia mifumo ya kudhibiti uingizaji wa bidhaa tiba nchini pamoja na kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali.
“Kama umesajili dawa, tunafuatilia sokoni katika soko na kuchukua sampuli ya dawa na tunafanya uchunguzi kila mwaka ili kujua ubora wake,” amesema Dk Mwalwasi.