UCHAMBUZI WA MALOTO: Maadui sita wa Tundu Lissu Chadema

Leo, Februari 21, 2025, umetimia mwezi mmoja tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kifanye uchaguzi mkuu wenye sifa zote za kuitwa wa kihistoria. Uchaguzi unaotosha kuitwa huru, haki, wazi na unaominika.

Historia siyo kwa sababu ilikuwa mara ya kwanza mwenyekiti madarakani wa chama hicho kushindwa uchaguzi, bali mchakato wenyewe kwa jumla.

Kishindo cha uchaguzi kilikuwa kizito kupata kutokea. Mvumo wa uchaguzi, ulitoka zaidi nje, mitandaoni, kisha kuingia ndani na kutikisa busara za wajumbe.

Asubuhi, Januari 22, 2025, ilikuwa Jumatano. Mkesha wa uchaguzi ulimalizwa kwa matokeo kuwa Tundu Lissu alimshinda Freeman Mbowe, aliyeiongoza Chadema kwa miongo miwili. Wito wa Mbowe kwa Lissu, baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi ni kukiponya chama.

Halafu, Februari 3, 2025, Kamati Kuu Chadema, ikiongozwa na Lissu, ilifanya kikao Bagamoyo, Pwani, kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta mwafaka.

Baada ya kikao, walipiga picha iliyosambazwa mitandaoni kuonesha kwamba sasa Kamati Kuu ni moja, hakuna mgawanyiko.

Hayakutimia majuma matatu tangu kikao cha Bagamoyo, kada wa Chadema, Lembrus Mchome, aliwasilisha barua kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, kuomba ufafanuzi wa ukiukwaji wa Katiba ya Chadema, wakati wa kuthibitisha baadhi ya viongozi.

Januari 22, 2025, Lissu, kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Chadema, aliwateua baadhi ya viongozi, akiwemo Mnyika kuendelea na nafasi yake ya ukatibu mkuu, Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Aman Golugwa, Ally Juma, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar. Wote hao walithibitishwa na mkutano wa Baraza Kuu.

Lissu, aliwateua pia Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Saleh na Dk Rugemeleza Nshala kuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu. Kama ilivyotakiwa kikatiba, wateuliwa wote walithibitishwa na Baraza Kuu.

Hoja ya Mchome ni kuwa wote walioteuliwa na Lissu na kuthibitishwa na Baraza Kuu, ni kinyume cha Katiba ya Chadema kwa sababu mkutano wa Baraza Kuu uliowathibitisha wateuliwa hao wa Lissu, haukukidhi akidi kama inavyotakiwa kikatiba.

Kisha, Mchome kupitia akaunti yake ya mtandao wa X, aliandika kuwa Mnyika alitoa maagizo avuliwe nafasi zote za uongozi alizonazo ndani ya Chadema. Mchome ni Katibu wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Kilimanjaro.

Malalamiko ya Mchome yanamtengeneza adui wa kwanza wa Lissu kwenye nafasi yake ya uenyekiti. Lissu, anafahamika kuwa ni mtetezi wa haki.

Wasifu wake wa kisiasa, kwenye harakati hadi taaluma yake ya sheria, Lissu anayejulikana ni mmoja; wakili wa haki, sheria na utawala wa sheria.

Kitendo cha Lissu kuonekana anasigina Katiba ya Chadema na kufanya uteuzi ambao haukupata uthibitisho wa kikatiba, halafu wateuliwa wake kutumikia nafasi zao, maana yake kuna kupuuzwa kwa nyaraka ya chama kwa hali ya juu.

Ukizingatia kuwa Lissu ni mmoja wa waandishi wa Katiba ya Chadema, tena yeye enzi hizo akiwa mwanasheria wa chama, alicheza nafasi kubwa na muhimu kuiandika na kuipitisha, iweje tena yeye mwenyewe ageuke na kuisigina kwa sababu ya kutanguliza mbele matakwa yake?

Kingine, Lissu ni alama ya uhuru wa maoni. Na maisha yake yana gharama kubwa ya maumivu kwa sababu ya ujasiri wake wa kutoa maoni hata kwenye nyakati za hatari.

Kutambua hilo, iweje Mchome atakiwe kufukuzwa uongozi Chadema kwa kutoa maoni kuhusu kukiukwa kwa Katiba ya chama chao?

Sasa basi, adui wa kwanza wa Lissu ni yeye kuruhusu Chadema kuwafanyia watu wanaompinga, yale ambayo yeye kwa miaka mingi aliyasimamia kama kielelezo cha utetezi wa haki.

Kwa nini Mchome aadhibiwe kwa kutoa maoni? Mbona yeye alizungumza mengi dhidi ya Mbowe na hakufukuzwa?

Lissu ni mwanasheria na amekuwa akipaza sauti kubwa mahali popote alipoona utawala wa sheria unaingizwa kwenye majaribu.

 Sasa, adui wa pili wa Lissu ni pale atafanya uamuzi kinyume na Katiba ya Chadema.

Kitendo cha kuteua na aliowateuliwa kuthibitishwa na Baraza Kuu lenye upungufu wa akidi (kama hoja za Mchome ni sahihi), itamfanya Lissu kuwa sawa na imamu wa msikiti anayekula vibudu, wakati ni yeye ndiye anapaswa kuongoza waumini kula halali.

Je, ni kweli aliowateua hawakidhi matakwa ya kikatiba? Upo utetezi unatolewa kwamba wajumbe walitosha, na uthibitisho wa walioteuliwa na Lissu ni halali.

Mwingine atauliza, kwa nini uchaguzi wa wajumbe wa Mkutano Mkuu, waliopaswa kuchaguliwa na Baraza Kuu, ulishindikana kwa sababu ya akidi kutotimia?

Uchaguzi wa wajumbe wa Kamati Kuu Chadema, ushindikane kufanyika kwa sababu akidi, halafu walioteuliwa kuwa wajumbe wa Kamati Kuu Chadema, uteuzi wao iwezekane kuthibitishwa kwa sababu akidi ilifikiwa. Siku hiyohiyo na muda huohuo!

Adui wa tatu wa Lissu ni msimamo wa chama chake, “No Reforms, No Election”, yaani bila mabadiliko ya kikatiba na mifumo ya uchaguzi, hakuna uchaguzi. Wakati wote Lissu anapaswa kufahamu kuwa msimamo huo, mafanikio au kufeli kwake, anayetazamwa ni yeye.

Tafsiri ya mtaani kuhusu “No Reforms, No Election”, ni kuwa kama hakutakuwa na mabadiliko ya sheria na mifumo ya uchaguzi, basi uchaguzi hautafanyika Tanzania mwaka 2025.

Endapo uchaguzi utafanyika, moja kwa moja Lissu atatazamwa kama aliyeshindwa. Ikiwa Chadema watashiriki uchaguzi ambao hautafanyiwa marekebisho yoyote ya kisheria, Lissu atageuka kichekesho.

Hii maana yake ni kuwa Lissu anatakiwa apambane ama kuhakikisha mabadiliko ya kikatiba yanafanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu 2025, au kupambana kisheria kuhakikisha uchaguzi haufanyiki. Vinginevyo, wapo wengi watapoteza imani juu yake. Ndiyo maana, msimamo huo wa Chadema, kwa jicho la uchambuzi, unaweza kuwa adui wa Lissu.

Matarajio ya Watanzania, hususan wapenda mabadiliko, ni makubwa kwa Lissu. Upepo wa Lissu kuwa Mwenyekiti Chadema, ulivuma zaidi kutoka nje ya Chadema.

Wanamabadiliko waliweka matumaini yao kwa Lissu kwa imani kwamba yeye ni jawabu la vilio vingi vya mageuzi ya kisiasa. Wanaamini Lissu ni mwarobaini.

Wapo waliofanya kampeni kumtaka Lissu awe Mwenyekiti Chadema kwa imani kuwa yeye kukalia kiti itakuwa wakati mzuri wa kukomeshwa kwa matukio ya utekaji nyara watu. Lilitajwa sana jina la Deusdedith Soka, aliyepotea tangu Agosti 2024, akiwa na wenzake Jacob Mlay na Frank Mbise. Endapo matukio ya utekaji yataendelea, Lissu akiwa Mwenyekiti Chadema, kibao kitageuka.

Kisiasa, matarajio ya watu ni adui mkubwa wa nne. Watanzania wapenda mabadiliko wanamtarajia Lissu kwa mengi. Huo ni mzigo ambao ameubeba. Bila shaka, Lissu anafahamu kuwa matarajio ya Watanzania ni adui yake mwingine.

Lissu anaongoza taasisi ambayo ina ufinyu wa rasilimali. Fedha ndiyo kitu kinachotakiwa ili aweze kutimiza mengi anayoyataka.

Hivi sasa kuna tangazo la kuomba michango kwa Watanzania ili kuwezesha harakati za kisiasa zifanyike. Endapo atakosa fedha za kutosha, itakuwa vigumu kwake kufanikisha chochote.

Kwa muktadha huo, fedha ni adui wa tano wa Lissu Chadema, kama atazikosa kuelekea harakati zake za kisiasa. Kipindi hiki, kabla ya mambo mengine, anatakiwa kujikita kwenye kusaka fedha ili zirahisishe mbio zake za kisiasa.

Kuna adui wa jadi wa Lissu, na wa sita ni Jeshi la Polisi Tanzania. Huyu ni adui wa sita. Kwa vyovyote, Lissu katika harakati zake za kuzunguka mikoa ya Tanzania ili kueneza agenda yake ya “No Reforms, No Election”, atakutana na polisi.

Adui wa saba wa Lissu ni busara. Jinsi atakavyoweza kuwachukua wanachama na viongozi ambao wanapishana mtazamo.

Asipotumia busara na kwenda nao kidemokrasia, akataka kushindana au hata kutengeneza mazingira ya kuwafukuza, haitakuwa salama kwake.

Watu hao wenye msimamo unaokinzana na wake, wengi wao ni wale waliokuwa wanaamini kwamba Mwenyekiti aliyepita, Mbowe, ndiye hasa alistahili kuendelea kuongoza chama hicho. Lissu anapaswa kutumia busara dhidi ya wafuasi wa Mbowe, halafu aruhusu demokrasia itawale Chadema.

Related Posts