Uhusiano wa maumivu ya meno na hedhi kwa wanawake

Wiki iliyopita nilipokea swali kutoka kwa msomaji jina limehifadhiwa, aliuliza ni kwa nini anapata maumivu ya jino anapokaribia kuingia mzunguko wa hedhi na huendelea siku chache hata baada ya hedhi kuisha.

Hedhi inapokaribia kiwango cha homoni za kike zijulikanazo kitabibu kama ‘estrogen na progesterone’ huwa juu na husababisha damu kutiririka zaidi kwenye ufizi, hivyo kufanya hisia za fahamu kuwa za kupindukia hatimaye kuchochea msisimko kuwa juu zaidi.

Endapo kuna meno ambayo tayari yameanza kuharibika ikiwamo kuwa na matobo hisia za maumivu huhisiwa kirahisi.

Hali hiyo inampata mtu kabla na hata siku chache hedhi kuisha  kwa sababu viwango vya homoni hizo hupanda na hushuka mara hedhi inapoisha.

Uwepo wa maumivu katika meno ni njia ya mwili kujihami na kukufahamisha kuwa eneo hilo lina hitilafu.

Kama unapata hali hiyo ni vizuri kumwona daktari wa kinywa na meno mapema kwa ajili ya kuchukua hatua za mapema.

Mzunguko wa hedhi huathiri mwili mzima, mabadiliko ya homoni yanaweza kusababisha mabadiliko kwenye tishu kwenye mwili mzima, ikijumuisha kinywa na meno na hisia kama vile hasira.

Viwango vya ‘progesterone’ huathiri afya ya ufizi hali hiyo huitwa shambulizi la fizi wakati wa hedhi.

Muda mfupi kabla ya kupata hedhi, ufizi wa mtu unaweza kuvimba na kuonekana mwekundu, au hata kuvuja damu hivyo kusababisha kirahisi maumivu ya jino hasa yale yalio na matatizo.

Baadhi ya wanawake pia hupata tatizo la kuvimba kwa tezi za mate, au kuongezeka kwa vidonda vya kinywa na hata kinywa kuwa kichungu.

Ni hali ambayo inaweza kuwa ya muda mfupi au ya muda mrefu, na sio tishio kubwa kiafya na inaweza kudhibitiwa.

Uwepo zaidi wa mrundikano wa ugaga na bakteria karibu na fizi wakati viwango vya homoni hizo vinapokuwa juu kipindi cha kukaribia hedhi ni sababu ya dalili hizo.

Matokeo yake inaweza kusababisha ufizi kupata shambulizi hatimaye kuvimba, kuuma na kuvuja damu.

Hali hii ikiachwa bila kutibiwa, uvimbe unaoendelea kwenye ufizi unaweza pia kusababisha kuharibika kwa mifupa karibu na meno na hatimaye kupoteza jino.

Kwa hivyo mwanamke anatakiwa kuzingatia zaidi kutunza kinywa chake vizuri katika nyakati za maisha yake kwa kuzingatia kanuni za afya za kutunza afya ya kinywa.

Ni kawaida pia baadhi ya huduma za kinywa na meno ikiwamo ya usafishaji wa meno au kung”oa meno kuahirishwa na daktari wa meno.

Hii ni kwa sababu wakati wa hedhi, viwango vya estrojeni katika mwili wa mwanamke huongezeka kabla na wakati wa hedhi.

Estrojeni inaweza kuchangia kuwepo kwa uvimbe kwenye ufizi, hivyo kufanya iwe vigumu kwa daktari wa meno kupima kwa usahihi kubana kwa ufizi na upana wa nafasi karibu na meno.

Fizi zinapokuwa na uvimbe,  usafishaji wake unaweza kukuumiza pia. Hii ndio sababu madaktari wa meno  kwa kawaida huahirisha baadhi ya huduma za kinywa na meno mpaka pale hedhi inapopita.

Kipindi cha hedhi ni rahisi fizi kuchubuka na kuvuja damu hasa kama  unatumia mswaki mgumu na kutumia nguvu.

Ni kawaida daktari wa kinywa kumuuliza mgonjwa wa kike endapo yupo katika hedhi.

 Baadhi hujiuliza kwanini daktari anauliza swali hilo la afya ya uzazi wakati mgonjwa ana malalamiko ya afya kinywa.

Ukweli ni kwamba daktari anahitaji kumhudumia mgonjwa kwa kuzingatia weledi, kwa sababu kuna huduma hazitakiwi kufanyika kipindi cha hedhi ikiwamo ya usafishaji kinywa na meno.

Related Posts