Israeli imebaini mwili waliokabidhiwa na Hamas siyo raia wake

Tel Aviv. Mwili mmoja kati minne ya raia wa Israeli iliyorejeshwa jana kutoka mikononi mwa wapiganaji wa kundi la Hamas siyo wa raia wa taifa hilo.

Miili iliyorejeshwa kwa mujibu wa Hamas ni mwili wa Shiri Bibas, aliyekuwa na umri wa miaka 32 wakati alipochukuliwa mateka pamoja na miili ya watoto wake Ariel (4)  na Kfir (miezi 9). 

Pia, kuna mwili wa Oded Lifshitz, aliyekuwa na umri wa miaka 83 wakati anachukuliwa mateka pamoja na mkewe, Yocheved Lifshitz, ambaye ni mke wa Oded aliachiliwa na Hamas Oktoba 24, 2023.

Hata hivyo, Al Jazeera imeripoti leo Ijumaa Februari 21, 2025, kuwa ripoti ya vipimo vya vinasaba (DNA), uliofanyika jana Alhamisi umebaini kuwa vinasaba vya mwili uliokuwa kwenye jeneza linalotajwa kuwa na mabaki ya, Shiri Bibas havioani na vinasaba vyake.

Ripoti hiyo pia imesema vinasaba vya miili mingine ikiwemo ya watoto wawili wa Shiri ambao ni Ariel (4) na Kfir (miezi 9) vinaona na vinasaba vyao sambamba na mwili wa Oded Lifshitz.

Oded na mkewe, Yocheved walichukuliwa mateka na Hamas wakiwa katika nyumba yao huko Kibbutz Nir Oz, kusini mwa Israeli.

Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) tayari limeifahamisha familia ya Bibas kwamba miili ya watoto wake imetambuliwa baada ya mabaki yao kukabidhiwa kwa Israeli na Hamas Alhamisi.

Hata hivyo, IDF imesema mwili wa tatu si wa mama yao.

IDF imedai Hamas irejeshe mwili wake pamoja na mateka wengine waliosalia. Hamas bado haijatoa tamko lolote kuhusu madai ya Israeli kuwa mwili huo siyo wa mke wa Bibas.

“Wakati wa mchakato wa utambuzi, ilibainika kuwa mwili wa ziada uliopokelewa si wa Shiri Bibas na haukuoana na mateka yeyote mwingine. Huu ni mwili wa mtu asiyetambulika,” IDF ilichapisha kwenye X.

“Hili ni ukiukaji mkubwa sana wa makubaliano uliofanywa na wapiganaji wa Hamas ambao walipaswa kulingana na makubaliano kurejesha miili ya mateka wanne waliokufa. Tunataka Hamas imrejeshe Shiri nyumbani pamoja na mateka wetu wote,” limesema jeshi hilo.

IDF imesema watoto hao wawili, waliuawa kikatili na magaidi wakiwa matekani Novemba 2023, kulingana na taarifa za Shirika la Ujasusi wa Israel la Shin bet na taarifa za uchunguzi wa kitabibu.

Hata hivyo, Hamas imedai kuwa watoto hao na mama yao waliuawa kwenye shambulio la mabomu la Israel.

Shiri, Ariel, na Kfir Bibas walikuwa na umri wa miaka 32, minne, na miezi tisa walipotekwa wakati wa mashambulizi ya Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.

Baba wa watoto hao, Yarden Bibas, mwenye umri wa miaka 34, aliachiliwa na Hamas katika mabadilshano yaliyofanyika Februari Mosi mwaka huu.

Israel pia imethibitisha kuwa mwili wa nne uliorejeshwa Alhamisi ni wa mwanaharakati mkongwe wa amani, Oded Lifshitz.

Kuachiliwa kwa miili ya mateka kulikubaliwa kama sehemu ya makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo yalitekelezwa Januari 19, mwaka huu. Israeli imethibitisha kuwa kutakuwa na jumla ya miili minane.

Pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya kubadilishana mateka 33 kwa wafungwa takribani 1,900 ifikapo mwisho wa wiki sita za kwanza za usitishaji mapigano hayo.

Mazungumzo ya kuendelea na hatua inayofuata ya makubaliano ambapo mateka waliosalia wangerejeshwa na vita vingemalizika kabisa yalipangwa kuanza mapema mwezi huu lakini bado hayajaanza.

Hadi sasa, mateka 28 wa Israeli wameachiwa na Hamas na zaidi ya wafungwa 1,000 wamerejeshwa eneo l Gaza kutoka katika magereza ya Israel.

Mateka 66 waliotekwa Oktoba 7, 2023, bado wanashikiliwa Gaza. Mateka wengine watatu waliotekwa zaidi ya muongo mmoja uliopita pia wanashikiliwa. Karibu nusu ya mateka wote waliobaki Gaza wanaaminika kuwa hai.

Takribani watu 1,200, wengi wao wakiwa raia waliuawa katika mashambulizi ya Hamas la Oktoba 7, 2023 na wengine 251 walichukuliwa mateka na kupelekwa Gaza.

Israel ilizindua operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya Hamas kama majibu, operesheni ambayo imewaua Wapalestina angalau 48,297 wengi wao wakiwa raia kulingana na Wizara ya Afya inayoendeshwa na Hamas.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts