Msimamizi uchaguzi abadili gia angani uhalali wa mgombea ACT

Kigoma. Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa wa Livingstone, Kata ya Kasingirima, Manispaa ya Kigoma Ujiji, amebadili gia angani baada ya kukiri mahakamani kumtambua mwanachama wa ACT – Wazalendo, Luma Akilimali kuwa alikuwa mgombea katika uchaguzi huo.

Akilimali amefungua shauri la uchaguzi Mahakama ya Wilaya ya Kigoma akipinga mchakato na uchaguzi wa mwenyekiti wa mtaa huo, kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji wa mwaka 2024, uliofanyika Novemba 27, 2024.

Wajibu maombi (walalamikiwa) katika shauri hilo linalosikilizwa na Hakimu Aristida Tarimo ni aliyekuwa mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo, msimamizi msaidizi wa uchaguzi mtaa huo na Msimamizi wa Uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa).

Katika hati ya maombi ya shauri hilo, Akilimali anadai kuwa mchakato wa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na ulikiuka kanuni zilizowekwa na hivyo kuufanya kuwa batili, kutokana na kasoro zilizojitokeza.

Amebainisha kasoro hizo kuwa ni pamoja na mchakato wa uandikishaji wapigakura kutokufanyika kwa mujibu wa kanuni, ongezeko la wapigakura, mtendaji wa kata kuharibu uchaguzi kwa kuingia kituoni na kura alizozichangaya kwenye kura zilizokuwa zinahesabiwa.

Nyingine ni baadhi ya watu kupiga kura zaidi ya moja huku wakisadiwa na msimamizi msaidizi, sanduku la kura za mwenyekiti kuwekwa mafichoni ambako mawakala hawakuwa wanawaona waliokuwa wanatumbukiza kura, watu wasiokuwa wakazi kupiga kura na kuingizwa kura bandia.

Hivyo, anaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, imuamuru msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa mtaa huo atangaze uchaguzi ndani ya siku 14 na ndani ya siku 60 ufanyike uchaguzi mwingine wa nafasi hiyo.

Wajibu maombi wa pili, msimamizi msaidizi (wa mtaa huo) na wa tatu, msimamizi wa uchaguzi (Mkurugenzi wa Manispaa), katika majibu yao ya pamoja ya maandishi, wamemkana mlalamikaji kuwa hakuwa miongoni mwa wagombea katika uchaguzi huo.

Hata hivyo, katika ushahidi wake mahakamani jana, Alhamisi, Februari 20, 2025, msimamizi msaidizi ni shahidi wa pili upande wa utetezi, amekiri kumtambua Akilimali kuwa mmoja wa wagombea aliowateua katika uchaguzi huo.

Joakim amebadili msimamo wake huo wa awali wakati wa maswali ya dodoso kutoka kwa kiongozi wa jopo la mawakili wa mwombaji, Emmanuel Msasa na kwamba kama moja ya majukumu yake, aliratibu kampeni zake.

Katika ushahidi wake akiongozwa na Wakili wa Serikali, Honorina Munisi, pamoja na mambo mengine, amesema siku ya upigaji kura, watu walipiga kura bila tatizo lolote mpaka saa 10 jioni walipofunga shughuli hiyo.

Ameeleza kuwa ndani ya kituo kulikuwa na kituturi ambacho ni sehemu ya siri ya kupigia kura na kwamba si kweli kwamba sanduku la mwenyekiti lilikuwa limefichwa kwenye kituturi hicho, bali masanduku yote yalikuwa sehemu ya wazi.

Amesema upigaji kura ulifanyika vizuri bila tatizo mpaka walipofunga saa 10 na baada ya kuhesabu na kujumlisha kura, alibandika matokeo na akayatangaza saa 2 usiku, ambapo alimtangaza mgombea wa CCM, Mawazo Kiembe kuwa mshindi kwani ndiye alipata kura nyingi.

Amedai kuwa tuhuma za mlalamikaji si za kweli, hakuna kura zilizoletwa na mtendaji wa kata.

Akihojiwa na Wakili Msasa, amekiri yeye ndiye aliteua wagombea na Akilimali (mlamikaji) alikuwa ni mgombea lakini hakumbuki kama alimteua, japo aliratibu kampeni zake, sambamba na vyama vya  CCM, CUF, Chadema, UDP na TLP.

Akihojiwa na Wakili Eliutha Kivyiro, msimamizi huyo amekubali kuwa alichokisema kuhusu mpangilio wa chumba cha kupigia kura na kuwa aliyoyaeleza yeyem ambayo yalikuwa tofauti na ushahidi wa mjibu maombi wa kwanza, Mawazo; haikuwa uhalisia.

Hivyo amesema aliyoyasema aliyekuwa mgombea wa CCM ndio yachukuliwe ni ya kwake pia.

Amekiri alibandika kwanza matokeo ndipo akatangaza (badala ya kutangaza ndipo ayabandike na kwamba hakutaja kura za mshindi katika majibu yake ya maandishi.

Shahidi wa tatu wa utetezi, Ofisa Maendeleo ya Jamii, Leah Thomson amesema yeye ndiye alikuwa msimamizi wa kituo cha kupigia kura mtaa wa Livingstone.

Amesema kabla ya kupiga kura, masanduku yalifunguliwa na kuonyeshwa kwa mawakala, yakafungwa kura zikaanza kupingwa.

Amesema baada ya kumaliza kupiga kura walisoma idadi ya wapigakura waliojiandikisha na waliopiga kura kisha wakaanza kuhesabu kura zote zilizopigwa kulingana na makundi.

Baadaye wakaanza kuchambua moja moja, kura ikioneshwa kwa wawakilishi wa vyama na walipomaliza, alijaza kura kwenye fomu za matokeo na mawakala wasimamizi, nakala ikabandikwa katika kituo cha wazi na msimamizi msaidizi wa uchaguzi akatangaza matokeo.

Amedai kuwa kwenye kituo chake uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na salama na hakuona kura bandia, hivyo tuhuma za mlalamikaji si sahihi na ameiomba Mahakama iitende haki kulingana na maelezo ya pande zote.

Akihojiwa na Wakili Msasa, amesema Akilimali (mwombaji) alikuwa mgombea maana alimuona kwenye orodha ya wagombea.

Amesema Akilimali alipigiwa kura na alikuwa na wakala ambaye hao wasimamizi hawakuwahi kumtoa kwa madai kuwa si mgombea.

Kwa upande wake, shahidi wa kwanza wa utetezi, ambaye ni mjibu maombi wa kwanza, Mawazo amesema uchaguzi ulikuwa huru na wa haki na kwamba baada ya kupiga kura aliondoka kwenda nyumba akasubiria matokeo na baadaye msimamizi alimtangaza kuwa mshindi na mwenyekiti wa mtaa wa Livingstone.

Amesema mwombaji, Akilimali alikuwa mmoja wa wagombea katika uchaguzi huo na kwamba yeye alishinda kwa kura 187 na aliyefuatia ni wa ACT Wazalendo alipata kura 89.

Amesema hakuona wala kusikia vurugu wala kuchomwa kituo, ameiomba mahakama itupilie mbali shauri hilo na alipwe gharama.

Akihojiwa na wakili wa mwombaji, Prosper Maghaibuni amekubali baada ya kupiga kura na kuondoka yaliyoendelea pale, yeye hakuyaona.

Amesema hajaleta fomu ya matokeo kuthibitisha alishinda kwa kura 187 wala kwenye majibu yake ya maandishi aliyoyawasilisha mahakamani hakuandika hiyo idadi ya kura.

Akihojiwa na Wakili Kivyiro, amekiri kuwa hakuwepo kituoni kwa muda wa saa 10 na hakujua wala hakuwa na muujiza wa kujua yaliyokuwa yakiendelea kituoni hapo wakati yeye yuko nyumbani.

Amekiri kuwa mshindani wake wa karibu alikuwa ni mgombea wa ACT Wazalendo japo awali alipotaka orodha ya vyama vilivyoshiriki alimsahau.

Pande zote zimefunga usikilizwaji na Hakimu Tarimo ameahirisha shauri hilo mpaka Februari 24, 2025, saa 3 asubuhi kwa ajili ya hukumu.

Related Posts