Dar es Salaam. Wanawake wametakiwa kutumia elimu au nafasi mbalimbali za uongozi wanazopata kuinufaisha jamii huku wakisisitizwa kuwa nafasi wanazopata zisiwe kigezo cha kuvuruga familia zao.
Hayo yamebainishwa leo Februari 21, 2025 na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa hafla ya kuadhimisha ya miaka 10 ya Programu ya Mwanamke Kiongozi inayoendeshwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kwa kushirikiana na Serikali ya Norway pamoja na wadau wengine.
Hafla hiyo pia imehusisha mahafali ya 10 ya wahitimu takribani 110 waliopatiwa mafunzo hayo.
Programu hiyo ya Mwanamke Kiongozi ilianzishwa mwaka 2016 kwa lengo la kuwaongezea ujuzi wanawake katika uongozi katika sekta mbalimbali.
Akizungumza katika hafla hiyo Rais Samia amesema wanawake waliopata fursa ya elimu au nafasi mbalimbali za uongozi wana dhima ya kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na imani na amani katima maeneo wanayoishi na elimu ya mtoto wa kike.
“Elimu na nafasi za uongozi zisitufanye tukasahau jukukumu letu la msingi la malezi na makuzi ya watoto wetu, mkisahau jukumu hilo athari mbalimbali zinaweza kujitokeza katika jamii”amesema.

Amebainisha miongoni mwa athari hizo kuwa ni kuishi maisha ya huzuni wakati wa uzeeni kutokana na watoto kujiingiza katika mienendo isiyofaa au kukosa muda wa kukaa na wazazi wao kama walivyofanyiwa wakati wa utoto.
Pia itazalisha watoto ambao ni tegemezi na kuwa mzigo katika taifa vilevile itarudisha nyuma jitihada za kumuelilisha mtoto wa kike na kumuinua mwanamke.
“Zamani hakukuwa na imani juu ya uwezo wa mwanamke kuna waliosema kuna Rais ambaye ataambiwa fanya na atafanya, wapo waliosema hatuna Rais tuna ‘housegirl’ na waliosema maamuzi ya ‘kitchen party’ utaona imani waliokuwa nayo wenzetu anaposimama mwanamke,”amesema Rais Samia.
Hata hivyo amesema imani hiyo kwa sasa inaondoka hivyo ili kujenga imani thabiti juu ya uwezo wa mwanamke anatakiwa kufanya yale yanayotakiwa kufanya.
Vilevile ametumia fursa hiyo kuwasihi wahitimu kutumia maarifa waliyoyapata kipindi chote cha mafunzo kuwainua wanawake wengine kwani wana dhima ya kufanya hivyo.
“Mnaporudi katika maeneo yenu ya kazi mkumbuke kuwainua wanawake wengine, hapa simaanishi kuwapa upendeleo bali mkawaongoze na kuwasaidia,”anasema.
Amesema kwa kufanya hivyo itasaidia kuongeza idadi ya wanawake katika uongozi na hatimaye kusaidia kuweza kusukuma ajenda zao.

Pia amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kwenda kuongeza chachu ya maendeleo katika familia, jamii na taifa kwa ujumla kwani ukimuelimisha mwanamke umeelimisha jamii.
Ameongeza kuwa anajisikia faraja kuona programu aliyoizindua miaka miaka 10 iliyopita imegusa maisha ya wanawake wengi.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha ajenda ya mwanamke na uongozi inasonga mbele.