Wananchi wa Kata ya Mkongotema Halmashauri ya Madaba Mkoani Ruvuma, wameelezea furaha yao kuhusu utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM na mafanikio yaliyopatikana katika miaka minne ya utawala wa Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Kizito Muhagama, Wananchi hao wamekiri kuwa miradi ya maendeleo inayotekelezwa imemaliza changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili na sasa wanapata huduma muhimu ambazo awali zilikuwa kikwazo kwa maisha yao.
Hazidu Mussa Njozi Mkazi wa Kijiji cha Lutukila, ameelezea furaha yake kwa kusema kuwa kero zote zilizokuwa zikiwakabili zimeshughulikiwa ipasavyo, huku Akisisitiza kuwa Mbunge ameonyesha dhamira ya dhati kwa wananchi kwa nyakati tofauti tofauti alilazimika kutumia fedha zake binafsi kusaidia changamoto zinazowakabili ikiwa ni pamoja na uchimbaji wa visima uliowasaidia kupata maji wakati suluhisho la kudumu la tatizo la maji kwa wakazi wa kijiji hicho lilipokuwa likifanyiwa kazi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ndelenyuma Stanley Ngairo, ametoa shukrani zake kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM akisema kuwa miradi ya maendeleo inayoendelea katika maeneo yao imeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi, ameeleza kuwa Mbunge ameonyesha juhudi kubwa kuhakikisha kuwa maeneo ya Lutukila, Ndelenyuma na Mbangamawe yanaendelea kuimarika kila uchao na ameahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mbunge katika awamu nyingine ya utawala.
Awali, wananchi wa Kata ya Mkongotema walikumbwa na changamoto za huduma muhimu ikiwemo maji, umeme, na shule, hata hivyo utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo umeleta mabadiliko makubwa na wananchi sasa wanashuhudia mafanikio makubwa katika sekta za elimu, afya, na miundombinu.
Katika ziara ya kikazi ya Mbunge wa Jimbo la Madaba Joseph Mhagama, amezungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa miaka minne, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kijamii, Mhagama amesema kuwa kwasasa wananchi wa Kata ya Mkongotema wanapata huduma za afya, elimu, maji, umeme, na barabara, ambazo zilikuwa changamoto kubwa awali.
Amesema Miradi ya maji imefanikiwa na sasa kuna mradi mkubwa wakusambaza maji kutoka Lutukila hadi Mtazamo ambapo wakazi wengi walikumbwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi, huku katika sekta ya elimu Kata hiyo inatarajia kupokea fedha za ujenzi wa Shule ya Sekondari, takribani Bilioni 1 na milioni 120 fedha ambazo zitasaidia kuboresha elimu katika maeneo hayo.
Kwa upande wa umeme, ajenda ya kusambaza umeme kwa Lutukila imetekelezwa na umeme umefika katika maeneo ya mbali ambayo awali yalikuwa hayana huduma hiyo muhimu.
Wananchi wa Kata ya Mkongotema wamethibitisha kuwa utekelezaji wa Ilani ya CCM katika Jimbo la Madaba umeleta maendeleo ya dhati na wameahidi kuendelea kumuunga mkono Mbunge wao katika kipindi kingine cha utawala, ili kufanikisha miradi zaidi ya maendeleo katika maeneo yao.