SARE ya bao 1-1 iliyopata Tanzania Prisons dhidi ya Tabora jioni hii kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa, imeonekana kumtibua kocha mkuu wa timu hiyo, Aman Josiah, akiiwakia safu ya ushambuliaji.
Mbali na washambuliaji, lakini kocha huyo amesema kuruhusu mabao kila mechi inampa wakati mgumu kuendelea kusuka upya kikosi hicho kuhakikisha wanaondoka nafasi za chini akitoa matumaini mechi zijazo kufanya kweli.
Josiah aliyetua kwa maafande hao kuziba nafasi ya Mbwana Makata ameongoza katika mechi nne, huku akishinda moja tu dhidi ya Mashujaa iliyoinyoa mabao 2-1, akipoteza miwili kwa Namungo 0-1, Dodoma Jiji 3-2 na ikatoka sare moja ambayo ni ya leo.
Matokeo hayo yanaifanya timu hiyo kubaki nafasi tatu za mkiani kwa pointi 18 baada ya michezo 21 wakibakiwa na mechi tisa kuamua hatma yao kubaki au kushuka daraja.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Sokoine jijini hapa, Prisons walioneka kumiliki zaidi mpira huku wakishindwa kutumia nafasi walizopata kufunga mabao haswa kupitia kwa Haruna Chanongo na Adam Adam.
Hata hivyo, dakika ya 68 baada ya krosi ya pembeni iliyopigwa na Doto Shaaban ilionekana na kurukiwa na Adam ambaye aliukosa na kumgonda kifuani beki wa Tabora, Emmanuel Chigozie wa Tabora kujifunga kabla ya Nyuki hao wa Tabora kulichomoa dakika ya 82 kupitia kwa Emmanuel Mwanengo na kuwafanya wageni kubaki nafasi ya tano kwa alama 34.
Mara baada ya mchezo huo, Josiah amesema bado tatizo la kutumia nafasi wanazopata ni tatizo kwa straika akieleza kuwa hakuna tatizo linalowakabili la aidha ndani au nje ya uwanja.
Amesema mechi tatu walizocheza mfululizo walistahili kupata ushindi lakini kwa makosa ya wachezaji walijikuta walipoteza ikiwamo Tabora United.
“Kipa ni kama kalala, mtu anapiga mpira wala hatishiki, tumewazidi sana hasa kipindi cha kwanza nafasi nyingi tumepata hakuna umaliziaji”
“Tunaenda kusahihisha makosa kuhakikisha michezo inayofuata tunafanya vizuri, tutawaandaa kisaikolojia wachezaji ili kuwa na Utulivu wa uwanjani” amesema Josiah.
Kiungo wa timu hiyo, Beno Ngassa amesema matokeo hayo si mazuri sana akieleza kuwa bado ni mapema kukata tamaa akiwatoa hofu mashabiki kuwa Prisons haishuki.
“Ni matokeo ya mpira lakini tunaendelea kupambana kwakuwa bado Ligi haijaisha, makosa yaliyoonekana kocha atasahihisha ili mechi zijazo tupate ushindi na kujiweka pazuri” amesema Ngassa.