Dar es Salaam. Sifael Shuma (92) aliyekuwa mmoja wa vijana wanne walioshiriki tukio la kuchanganya udongo siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964, amefariki dunia na kufunga kumbukumbu ya vijana hao.
Sifael ambaye ndiye alikuwa amebaki hai, kifo chake kimefunga ukurasa wa vijana wanne, wawili kutoka Zanzibar na wengine wawili kutoka Tanganyika walioshiriki tukio la Mwalimu Nyerere kuchanganya udongo, ikiwa ni ishara ya muungano wa nchi hizo mbili.
Vijana wengine walioshiriki tukio na wametangulia mbele ya haki wakiwa tayari watu wazima ni Hassan Omar Mzee (76) na Khadija Abbas Rashid (74) (wote kutoka Zanzibar) na Hassaniel Mrema (80) na Sifael (92) waliotoka Tanganyika.
Hassan Omar Mzee na Hassaniel Mrema ndio walioshiriki kushika chungu kilichowekwa udongo wa nchi hizo mbili na Khadija na Sifael wao walibeba vibuyu vilivyokuwa na udongo.
Sifael alibeba kibuyu chenye udongo wa Tanganyika na Khadija alibeba kibuyu chenye udongo wa Zanzibar.
Udongo wa Zanzibar uliochanganywa ulitoka eneo la Kizimbani Unguja, ule wa Tanganyika ulichotwa maeneo ya Dar es Salaam.
Kifo cha Sifael licha ya kufunga kumbukumbu bado wanne hao wataendelea kubaki kwenye historia ya vijana walioshiriki tukio la Aprili 26, 1964 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam la Mwalimu Nyerere kuchanganya udongo kwa kuumimina ndani ya chungu kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Sifael aliyefariki Februari 20, 2025 katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na baadaye kupata ugonjwa wa (Brain Atrophy) seli za ubongo kukosa mawasiliano.
Brain Atrophy ni tatizo linalosababishwa na mambo mengi hasa yanayoweza kusababisha seli za ubongo kufa.
Taarifa za kifo cha Sifael zimetolewa na mwanaye Dk Vida Shuma aliyezungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Februari 21, 2025.
“Mama alikuwa anaumwa alipata ugonjwa wa sukari lakini sio ugonjwa uliosababisha kifo chake, alisumbuliwa pia na tatizo la ubongo na baadaye akashindwa kutembea kwa miaka mitano hadi umauti unamkuta,” amesema.
Dk Vida amesema mama yake alikuwa miongoni mwa waasisi wa muungano na sifa yake kubwa alikuwa na upendo ndani na nje ya familia yake, mara zote alipenda kuimba kwaya licha ya kutokuwa na uwezo wa kusimama.
Kulingana na ratiba ya mazishi, mwili wa Sifael utasafirishwa kwenda Machame siku ya Jumanne Februari 25, 2025 na Februari 26 ibada itafanyika Kanisa la Nkwaruko mkoani Kilimanjaro.
Baada ya masomo yake ya kidato cha tano na sita mwaka 1956, Sifael alichaguliwa kuendelea na masomo ya juu Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda, lakini alikataa mpango huo.
Baada ya kukataa mpango huo alikwenda kufundisha Shule ya Sekondari Loleza mkoani Mbeya, baada ya mwaka mmoja alikwenda Chuo cha Ualimu Mpwapwa kuwafundisha walimu daraja A.
Hata hivyo, baada ya muda aliomba kurudi kufundisha wanafunzi wa sekondari hasa somo la hisabati ambalo alilipenda zaidi.
Enzi ya uhai wake Sifael aliwahi kuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Machame,
Mwaka 1959 akiwa Shule ya Sekondari Machame aliweka rekodi ya kuwa mwalimu mwafrika aliyetumika kufundisha wanafunzi somo la Hisabati, Kingereza pamoja na uraia.
Akihudumu kama mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Machame, Sifael ametumikia nafasi hiyo kwa miaka 30 hadi alipostaafu kazi ya kufundisha mwaka 1993.