Geita. Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita linawashikilia wanafunzi 30 wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Geita kwa tuhuma za kusababisha vurugu zilizosababisha hasara ya mali za shule zenye thamani zaidi ya Sh2.9 milioni.
Vurugu katika shule hiyo zilitokea Februari 20, 2025 saa 2 usiku baada ya mmoja wa wanafunzi wa kidato cha sita kukutwa na simu na kupewa adhabu ya kusimamishwa shule kwa muda wa siku 73 na wenzake kutoridhia adhabu hiyo na kuanza vurugu.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Adam Maro amethibitisha kushikiliwa kwa wanafunzi hao na kusema wanafunzi walianza vurugu baada ya walinzi kumkamata mwenzao na simu na kumnyang’anya kisha kuiwasilisha kwa uongozi wa shule.
“Wanafunzi hao walianzisha vurugu kutokana na mwenzao kukutwa na simu kinyume na taratibu za shule na walinzi walivyochukua simu ili waiwasilishe kwa viongozi wa shule, mwanafunzi yule pamoja na wenzake walianza kuwapiga mawe walinzi lakini walinzi waliwadhibiti,” amesema.
Maro amesema baada ya walinzi kufikisha taarifa kwa uongozi, mwanafunzi aliyekutwa na simu alisimamishwa masomo na kukabidhiwa kwa wazazi wake na wanafunzi wenzake walipobaini mwenzao amesimamishwa shule, ndipo walianza vurugu za kurusha mawe wakitakaka mwenzao arudishwe shule.
Kufuatia vurugu hizo, Jeshi la Polisi liliingilia kati na kulazimika kutumia nguvu za kadri kuwatuliza wanafunzi hao na katika tukio hilo, mwalimu wa zamu, Lucas Ngalabuto alijeruhiwa kwa mawe wakati akiwatuliza wanafunzi hao.