Korti yamfutia dhamana anayeshtakiwa kwa kumiliki kobe

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemfutia dhamana na kumrudisha rumande, mshtakiwa Mwaluko Mgomole (41) baada ya kuruka dhamana.

Mgomole ambaye ni mshtakiwa wa nane katika kesi ya kuongoza genge la uhalifu na kumiliki kobe 116, amefutiwa dhamana yake, baada ya kutoroka na kushindwa kuhudhuria kesi yake tangu Machi 2024.

Uamuzi huo umetolewa leo, Februari 21, 2025 na Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga, baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa mkoani Dodoma na kusafirishwa hadi Dar es Salaam na na kupandishwa kizimbani.

Kabla ya kufutiwa dhamana yake, Wakili wa Serikali Mwandamizi Neema Moshi akishirikiana na Gloria Kilawa, waliomba mahakama imfutie dhamana yake kwa kushindwa kuhudhuria mahakama wala kutoa taarifa.

Pia, alisema wadhamini wa mshtakiwa huyo nao hawakuwahi kufika mahakamani hapo wala kutoa taarifa alipo mshtakiwa huyo.

Kutokana na mshtakiwa pamoja na wadhamini wake kutokufika mahakamani ilitoa hati ya kumkamata mshtakiwa pamoja na wadhamini.

Baada ya kutolewa kwa hati hiyo, mmoja wa wadhamini alifika na kueleza sehemu anazopatikana mshtakiwa na baadaye kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi alikamatwa na kufikishwa mahakamani pamoja na mdhamini mmoja, baada ya mdhamini mwingine kufariki dunia.

“Hivyo kutokana na hali hii tunaiomba mahakama imfutie dhamana Mgomole kwa sababu amekuwa kikwazo kwa kesi hii kuendelea,” alisema Wakili Moshi.

Moshi baada ya kuwasilisha ombi hilo, Hakimu Ruboroga alimhoji mshtakiwa sababu ya kuruka dhamana na sehemu ya mahojiano ilikuwa kama ifuatayo:

Hakimu: Mshtakiwa kwa nini usifutiwe dhamana kwa kitendo ulichofanya?

Mshtakiwa: Kipato ndicho kilinishinda, nikakosa hadi nauli ya kuja mahakamani.

Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu hata simu sikuwa nayo, hivyo nilishindwa kuongea hata na wadhamini wangu, lakini nilipopata simu niliwasiliana nao.

Hakimu: Kwa hiyo ukikosa hauli huji mahakamani? Kesi hii ulikuwa imeiweka nafasi gani?

Mshtakiwa:  Ilikiwa lazima nifike mahakamani, lakini mheshimiwa nauli ya kutoa Dodoma kuja huku Kisutu na kurudi sikuwa nayo.

Hakimu: Mwaka mzima hujafika mahakamani kuhudhuria kesi yako, ulishindwa hata kuweka salio kwenye simu yako ukapiga na kutoa taarifa?

Hakimu: Kwa hiyo ukaamua kujiruhusu mwenyewe?

Mshtakwa: Hapana, kuna vitu vingine mheshimiwa unajilazimisha lakini inashindikana.

Mshtakiwa: Niliwasilisha ombi kwa upande wa mashtaka niwe naripoti kulekule Dodoma lakini walikataa, sasa kesi hii ilikuwa inatajwa kila baada ya siku 14 na mimi nimekosa nauli, nafikaje Dar ?

Akitoa uamuzi, Hakimu Ruboroga alisema kwa maelezo aliyotoa mshtakiwa anaonekana hana sifa za kupata dhamana.

“Sasa kwa maelezo hayo mshtakiwa, Mahakama inaona wewe ni ulifanya makusudi ya kuitekeleza kesi yako. Kwa mazingira haya, unaonekana huna sifa za kupata dhamana, hivyo Mahakama inakufutia dhamana na utaendelea kubaki rumande,” alisema Hakimu Ruboroga

Baada ya uamuzi huo, Hakimu alipanga kesi hiyo iitwe Februari 24, 2025 kwa kutajwa.

Mbali na Mgomole, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Josephat Moyo (52) mkazi wa Tabata; Deogratius Lugeng’a (40) mfanyabiashara na mkazi wa Kipunguni pamoja na MT 88046 Sajenti Cosmas Ndomba(39) mkazi wa Kivule.

Wengine ni MT 118102 Kassim Abdallah(35) ambaye pia ni  Ofisa Usalama wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere( JNIA) na mkazi wa Tabata Segerea.

Washtakiwa wengine ni Nkanamuli Mgaza (52) ambaye ni ofisa Usalama Uwanja wa Ndege JNIA;  Stephano Chedego (51) mkulima na mkazi wa Dodoma pamoja na raia wa Ukraine, Olga Kryshtopa (35) mwenye makazi yake Kiev – Ukraine ambaye yupo rumande kutokana na dhamana yake kuzuiwa na DPP.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na kumiliki nyara za Serikali, kinyume cha sheria.

Washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kukusanya, kununua na kusafirisha kobe 116 wenye thamani ya Sh18.93 milioni bila kibali cha Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Related Posts