Bingwa wa kisukari asimulia milima, mabonde ya kutibu ugonjwa huo Tanzania

Dar es Salaam. Miongoni mwa wataalamu wa afya wanaoaminika nchini, ni pamoja na Kaushik Ramaiya, mtafiti na daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na tiba ya kisukari.

Ushuhuda wa baadhi ya wagonjwa wanaohudhuria kliniki zake, ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kumpa umaarufu tangu alipoanza kutoa tiba za kisukari miaka 43 iliyopita.

Profesa Kaushik (70) amefanya mahojiano maalum na Mwananchi na kufafanua kwa kina namna alivyoweza kutoa huduma na siri iliyojificha katika tiba ya kisukari.

Pamoja na hayo anaeleza kwa kina kuhusu tiba ya ugonjwa huo, sera, mikakati iliyopo, huku akisisitiza mambo ambayo watafiti wanapaswa kuyalenga kwa sasa ili kuleta suluhisho katika jamii.

Akielezea safari yake ya kitaaluma, Profesa Kaushik anasema alianza kazi mwaka 1982 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kabla ya kwenda kubobea katika masuala ya magonjwa ya ndani na kisukari.

Anasema alirudi nchini mwaka 1991 na ndipo alianza rasmi kufanya kazi katika Hospitali ya Hindu Mandal na kuendelea kufundisha kama mhadhiri katika Idara ya Tiba ya Ndani katika Chuo Kikuu cha Muhimbili cha Sayansi ya Afya na Shirikishi.

“Nilipokuwa nasoma pale Muhimbili mwaka 1986 mpaka 1989 na kufanya masters (shahada ya uzamili) yangu, nilikuwa naona wagonjwa katika kliniki mbalimbali ikiwemo ya kisukari chumba namba 4 jengo la zamani.

“Pale nilikuwa na mwalimu wangu na tulikuwa na Profesa Andrew Swai na maprofesa wengine wawili, wakati tunaanza kliniki mwaka 1985 mpaka 1986 sukari ilikuwa inaaminiwa ni ugonjwa wa watu wenye fedha au walioendelea sana kiuchumi,” anasema Kaushik ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Shree Hindu Mandal.

Akisimulia hali ilivyokuwa, Profesa Kaushik anasema miaka hiyo pia  walikuwa wakiwahudumia wananchi wa hali ya chini kiuchumi, hivyo walianza kuifahamisha Serikali kwamba huenda hali ikawa mbaya zaidi baadaye.

Anasema wakati huo, wagonjwa wa kisukari walihudhuria siku ya Alhamisi na waliona wagonjwa wengi mno (hakumbuki idadi)

Ukubwa wa tatizo, ulimfanya afanye utafiti wake wa shahada ya uzamili  katika mada ya ugonjwa wa kisukari na uhusiano wake na magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu.

“Tangu hapo nilianza kupenda eneo hilo na mpaka leo tunaendelea na tafiti mbalimbali na ndipo tuliunda Chama cha Kisukari mwaka 1985, tukiangalia namna gani tuwasaidie wagonjwa kwani wengi walikuwa wa kipato cha chini.

“Lengo ilikuwa kuhakikisha wanapata matibabu kitaalamu, wanakuwa na dawa kwani wengi walikuwa hawawezi kununua, anaeleza.

Daktari huyo maarufu, licha ya kuwa ofisa mtendaji mkuu,  bado anafanya kazi kama daktari katika kliniki ya kisukari, huku akiendelea kufundisha na kufanya tafiti.

Anasema mwaka 1998 walianza kliniki ya kisukari hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala.

“Wakati huo tatizo halikuwa kubwa, tulianza kwa kujenga makontena hospitali hizi tatu, tukapata wagonjwa zaidi ya 4000, tukapata mradi mwingine tukaweka kliniki kwenye hospitali za mikoa.

“Tukapata ufadhili wa Danida na Alliance, taratibu tulivyoanza mwaka 2000 sukari kwenye hospitali za kanda na wilaya 184 na hivi karibuni tumeshusha huduma mpaka kwenye vituo vya afya 710 tumeshaenea nchi nzima, na sasa tuna mpango wa kutoa elimu kwa watoa huduma ngazi ya jamii,” anasema.

Profesa Kaushik anasema licha ya kwamba walianza kliniki za kisukari, ongezeko la magonjwa yasiyo ambukiza ikiwemo moyo, figo, shinikizo la juu la damu, saratani, mapafu, selimundu magonjwa ya akili, lilisababisha kliniki hizo kugeuzwa na kuwa za magonjwa yasiyo ambukiza.

Pamoja na mafanikio hayo, Profesa Kaushik anasema changamoto kubwa ilikuwa kuishawishi Wizara ya Afya kuwekeza zaidi eneo la magonjwa yasiyoambukiza, kwani wataalamu waliona ni eneo ambalo magonjwa yameongezeka.

Katika utendaji wake wa kazi, anasema changamoto kubwa ilikuwa wanapofanya mafunzo kwa wataalamu hasa wauguzi, hawakudumu eneo hilo.

“Umetoa elimu kwa watu 100 ukienda baada ya  mwaka watu 60 wamehamishwa au wameenda idara nyingine, ilikuwa changamoto.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni vifaa, baada ya kuvitoa hakukuwa na usimamizi mzuri ikiwemo kuvifuatilia, kuvitunza. Pia anasema wagonjwa wengi kugunduliwa katika hatua za juu za ugonjwa.

“Wanagunduliwa na kisukari wakiwa tayari wamepata madhara ya ugonjwa huo, kama kufeli kwa figo, upofu, moyo umepanuka, amepata kiharusi au kuna matatizo mengine,” anasema.

Sababu kisukari kuongezeka 

Profesa Kaushik anataja sababu za kuongezeka kwa ugonjwa wa kisukari katika Bara la Afrika na kwamba tafiti zinaonyesha utaongezeka kwa asilimia 134 mwaka 2025.

Anasema katika nchi zinazoendelea kama Amerika Kusini, Bara la Asia, Afrika itaongoza ingawaje idadi ya watu si kubwa kama India lakini ongezeko litakuja juu kwa sababu kuu tatu.

“Sababu ya kwanza maisha yamebadilika,  chakula, mazoezi, mtindo wa maisha, mabadiliko ya hali ya maisha vinachangia kwa kiasi kikubwa.

“Sukari zingine zimetokana na kurithi katika familia. Tatu ongezeko la kisukari kwa wajawazito wanapata kisukari cha mimba, inaweza kuleta shida kwa mama na mtoto atakayezaliwa na nyingine ni ile ya watoto type one,” anasema.

Kufuatia hali hiyo, anashauri elimu iongezwe kwa jamii, 

“Mtu akiona anapata kiu sana au anaanza kukojoa sana,  uzito unapungua, anapata kidonda hakiponi anapaswa kwenda hospitali akaangaliwe kuna kisukari au matatizo mengine,”anashauri.

Anasema bado kuna kazi kubwa ya kuelimisha jamii kuacha sigara, shisha, pombe na visababishi vyote vya magonjwa.

“Tafiti zinaonyesha hali ya maisha inaweza kuchangia zaidi ya asilimia 40 hadi 50 na hata kuzuia au kukinga ugonjwa vizuri kama ukifanya mazoezi,”  anasema.

Hata hivyo, anasema kuna dhana potofu kuhusu kisukari huku  wengi wakiamini  ni ugonjwa wa wenye fedha.

Akielezea ukuaji wa teknolojia, Profesa Kaushik anasema simu za mkononi zinaweza kusaidia kudhibiti kisukari, sambamba na matumizi ya  teknolojia ya akili mnemba ambayo imekuwa ikitoa tiba kwa walio wengi.

“Kuna mashine zimetoka sasa hivi  kawaida tunapopima sukari tunatoboa kidole, siku hizi zimetoka mashine , unaweka kwenye ngozi siku 14 huhitaji mashine, programu inakuwa kwenye simu yako unaweka karibu na simu yako pale inasoma kisha unapata kujua lini sukari yako imeshuka, imepanda, anasema.

Anasema  zipo teknolojia nyingi za tiba hiyo ila zina gharama kubwa, ingawaje Tanzania teknolojia hizo rahisi za matibabu zimeingia na baadhi wanazitumia.

Dk Kaushik anasema Tanzania iko mbali katika teknolojia ya matibabu ya Kisukari Afrika Mashariki.

Kuhusu ufanyaji wa  utafiti zaidi, anasema: “Bado hatujafikia kwenye lengo, mgonjwa wa sukari akija kwenye ofisi yangu sitajua sukari amepataje, tunahitaji tafiti kwanini wagonjwa wengi wa sukari wanapata matatizo ya figo kuliko magonjwa mengine, kiharusi, moyo.”

“Matibabu gani yanafaa kuwapata, itasaidia kwa kiasi kikubwa, nadhani bado kuna maeneo mengi ya kufanyia kazi,” anasema Profesa Kaushik mwenye watoto watatu na wajukuu wawili.

Related Posts