Besigye afikishwa mahakamani kwa ‘wheel chair’, ashitakiwa kwa uhaini

Dar es Salaam. Mahakama moja nchini Uganda imemshtaki mwanasiasa wa upinzani aliye kizuizini, Kizza Besigye, kwa kosa la uhaini Ijumaa iliyopita, ikikataa ombi la wakili wake la kumhamishia hospitalini ili kupata matibabu kutokana na matatizo ya kiafya yaliyosababishwa na mgomo wa kula.

Besigye, mwenye umri wa miaka 68, ambaye ni mpinzani na mkosoaji wa muda mrefu wa Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, alionekana mahakamani katika mji mkuu wa Kampala akiwa dhaifu kwenye kiti mwendo.

Alilazwa hospitalini kwa muda mfupi mwishoni mwa wiki, huku waziri mmoja katika Serikali ya Uganda akisema hali yake ya afya inatisha.

Wanasheria wake wanasema “alitekwa” jijini Nairobi, Kenya pamoja na msaidizi wake, Obed Lutale Novemba 2024 na kurudishwa Uganda ambako walifikishwa mbele ya Mahakama ya kijeshi kwa mashtaka ya kumiliki silaha kinyume cha sheria na uhaini.

Mkewe amesema Februari 12, 2025 kuwa Besigye alianza mgomo wa kula akipinga kuzuiliwa kwake.

Wakili wake alisema Ijumaa iliyopita kuwa sasa ameumaliza mgomo wake baada ya kesi yake kuhamishiwa Mahakama ya kiraia kufuatia uamuzi wa Mahakama ya Juu Januari 31, 2025 kwamba kuwashtaki raia katika mahakama za kijeshi ni kinyume cha katiba.

Mahakama ya hakimu mkazi ilitoa mashtaka mapya ya uhaini na kuficha uhaini huo ikidai kuwa alihusika katika jaribio la kupindua serikali lakini ikakataa kumpa fursa ya kujibu mashtaka hayo kwa sababu kesi hizo zinaweza kusikilizwa tu katika Mahakama ya Juu zaidi.

Hapo awali, Besigye alikataa kujibu mashtaka yanayomkabili kwa kuwa aliona ni kinyume cha sheria.

Kuzuiliwa kwake kumezua hasira miongoni mwa Waganda na kuchochea maandamano kadhaa. Jumuiya ya Madola yenye wanachama 56, imetoa wito wa kuachiliwa kwake.

Wakosoaji wa Museveni, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1986, wanasema kuzuiliwa kwa Besigye ni ishara nyingine ya kuongezeka kwa udikteta wakati Uganda inajiandaa kwa uchaguzi mkuu mwaka 2026 ambapo Museveni anatarajiwa kugombea tena.

Hata hivyo, maofisa wa Serikali wanakanusha madai ya ukiukaji wa haki za binadamu na kusisitiza kuwa waliokamatwa wanapitia mchakato wa kisheria kupitia mahakama.

Erias Lukwago, mmoja wa mawakili wa Besigye, alimtaka Hakimu Mkuu, Esther Nyadoi Ijumaa iliyopita kuagiza mamlaka za magereza kumpeleka Besigye hospitalini kwa matibabu maalumu.

Hata hivyo, Hakimu Nyadoi alisema mahakama yake haina mamlaka ya kutoa agizo kama hilo.

Related Posts