Viongozi watakiwa kuhakikisha Vijana wanakuwa kitovu cha sekta ya kahawa barani Afrika

Mkutano huo wa siku mbili tarehe 21-22 Februari 2025, unawakutanisha viongozi wa serikali, wataalamu wa sekta ya kahawa, sekta binafsi na watunga sera kujadili mikakati ya kuinua sekta ya kahawa barani Afrika kwa lengo la kuongeza thamani ya mazao, kujumuisha vijana katika sekta hiyo, na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo kwa ngazi ya Mawaziri, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ametoa rai kwa viongozi wenzake na wadau wa kahawa walioshiriki mkutano huo kuhakikisha Vijana wanakuwa kitovu cha sekta ya kahawa barani Afrika na kuongeza kuwa wadau wa Kahawa wanapaswa kuleta mbinu rafiki kwenye kilimo cha kahawa, kuunga mkono kanuni za biashara ya haki na kuweka mbele ustawi wa wakulima ili kuhakikisha sekta ya kahawa ya Afrika inastawi na hivyo kuvutia vizazi vijavyo.

“Mabadiliko katika sekta hii hayawezi kufikiwa kwa kutenda peke yetu. Ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na vyama vya kahawa ni muhimu katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa kahawa barani Afrika. Kupitia juhudi za pamoja, tunaweza kuimarisha nafasi ya Afrika katika soko la kimataifa la kahawa na kuleta ubunifu katika kila hatua kwenye mnyororo wa thamani, kuanzia uzalishaji hadi usindikaji na masoko,” alisisitiza Mhe. Bashe.

Amesema Tanzania imedhamiria kubadili sekta ya kahawa na katika kutekeleza dhamira hiyo, imeimarisha taasisi za utafiti wa kahawa ili kukabiliana na magonjwa ya kahawa, wadudu waharibifu na athari za mabadiliko ya tabianchi; Kuwapa wakulima ruzuku za pembejeo kama mbegu za kahawa na mbolea; Kuanzisha Mpango wa “Build Better Tomorrow” (BBT) unaolenga kuwawezesha vijana kushiriki katika kilimo biashara kwa kuongeza thamani ya kahawa, na kuwapa ardhi bure kwa ajili ya kilimo cha kahawa; Kuongeza matumizi ya kahawa ndani ya nchi kutoka asilimia 7% hadi 15% ifikapo mwaka 2030; Kuwekeza katika Kiwanda cha TANICA na kuimarisha vyama vya ushirika ili kuleta mabadiliko ya kudumu katika sekta ya kahawa.

Ameongeza kuwa utekelezaji wa mambo hayo matano unaendana na dira pana ya kuifanya Tanzania kuwa mfano wa kuigwa katika mageuzi ya sekta ya kahawa barani Afrika na amezisihi nchi zinazoshiriki mkutano huo, kuhakikisha dhamira ya kuleta mageuzi katika sekta ya kahawa barani Afrika inakuwepo huku wakisherehekea kazi ngumu ya wakulima wa kahawa, wasindikaji, wapishi wa kahawa (baristas), na wale wote wanaochangia kufanya kahawa ya Afrika kuwa nembo ya ubora duniani.

“Tuilinde urithi wetu! Tuwapelekee ujumbe wakubwa wa biashara duniani kwamba hatuombi misaada ya kukuza sekta yetu ya kahawa, bali tunahitaji usawa na haki katika biashara ya kahawa,” alisisitiza Mhe. Bashe.

Amezisihi nchi hizo kushikamana na kujadiliana kama kambi moja na wale ambao hawalimi lakini wanakunywa kahawa na nchi hizo zifanye biashara kati yao, zishirikiane na kusaidiana badala ya kushindana.

Ameongeza kuwa Mkutano huo umetoa fursa muhimu ya kubadilishana mawazo na kujadili njia bora za kuandaa mustakabali wa sekta ya kahawa na kwamba kwa kuongeza thamani ya kahawa, kuongeza matumizi ya ndani, kuhimiza ubora endelevu, hakutaimarisha sekta ya hiyo pekee, bali pia kutaongeza uwekezaji na fursa za ajira kwa vijana, ambao wanawakilisha asilimia 30 ya idadi ya watu barani Afrika.

Amesema ni wakati wa nchi za Afrika kupitia Umoja wa Afrika (AU) kusimama na wakulima na sekta binafsi na kuruhusu majadiliano kama kambi moja na Umoja wa Ulaya badala ya kujadiliana kila nchi peke yake.

Mkutano huo ni utekelezaji wa Azimio linalohimiza Wakuu wa nchi kutoka mataifa 25 yanayozalisha kahawa barani Afrika kuunga mkono ujumuishaji wa zao la kahawa kama bidhaa ya kimkakati kupitia Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika pamoja na kuitambua IACO kama taasisi maalum ya Umoja wa Afrika (AU).

Mkutano wa Tatu wa G25 wa Kahawa barani Afrika unalenga kuendeleza maazimio ya Nairobi na Kampala, kwa kuhakikisha sekta ya kahawa inakuwa chachu ya ajira kwa vijana na maendeleo ya uchumi wa Afrika. Mkutano unaendeshwa chi ya kauli mbiu isemayo “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uhuishaji wa Sekta ya Kahawa Afrika.”

Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe (Mb.) akifungua mkutano wa Tatu wa Nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika ngazi ya Mawaziri uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa ya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akifuatilia mkutano wa Tatu wa Nchi 25 zinazozalisha kahawa barani Afrika ngazi ya Mawaziri uliofanyika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa ya Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Related Posts