Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho wa wakuu wa wilaya wawili na kuteua wenyeviti wa bodi wa taasisi za Serikali.
Taarifa ya kuteuliwa na kuhamishwa kwa viongozi hao imetolewa leo Februari 21, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Moses Kusiluka.
Waliohamishwa vituo vya kazi kwa mujibu wa taarifa hiyo ni Dk Vicent Anney aliyehamishwa kutoka Wilaya ya Bunda kwenda kuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa.
Aswege Kaminyoge aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Maswa amehamishiwa Bunda.
Taarifa inaeleza Juma Kimori ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) akichukuwa nafasi ya Yona Killagane ambaye amemaliza muda wake.
Profesa Edward Hoseah ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa akichukuwa nafasi ya Dk Deo Mtasiwa ambaye amemaliza muda wake.
“Renatha Rugarabamu ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) akichukua nafasi ya Emmanuel Humba ambaye amemaliza muda wake,” inaeleza taarifa hiyo.
Jaji mstaafu Awadh Bawazir ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) akichukua nafasi ya Jaji mstaafu Sauda Mjasiri ambaye pia amemaliza muda wake.
“Balozi Ramadhani Muombwa Mwinyi ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa Dk Salim Ahmed Salim kwa kipindi cha pili,” inaeleza taarifa hiyo.