Tel Aviv. Israeli imeishtumu Hamas kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano baada ya uchunguzi wa vinasaba (DNA) kubaini kuwa mwili uliorejeshwa kutoka Gaza siku ya Alhamisi haukuwa wa Shiri Bibas.
Jeshi la Ulinzi la Israeli (IDF) limesema leo kuwa miili mingine mitatu iliyokabidhiwa imetambuliwa kuwa ya watoto, Ariel na Kfir, ambao wakati wanatekwa walikuwa na miaka miwili na miezi sita pamoja na mwanaharakati wa amani Oded Lifschitz, mwenye umri wa miaka 84.
Hata hivyo, mwili wa nne haukuwa wa Shiri wala mateka mwingine yeyote, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akidai kuwa Hamas iliweka mwili wa mwanamke wa Kipalestina ndani ya jeneza hilo.
Pia, inadaiwa kuwa mtoto wa Shiri, Ariel na Kfir Bibas waliuawa kikatili na magaidi.
“Magaidi hao hawakuwapiga risasi watoto hao wawili wadogo. Waliwaua kwa mikono yao wenyewe,” alisema Msemaji wa Jeshi la Israel, Daniel Hagari, kuhusu watoto hao wawili ambao miili yao ilikabidhiwa na Hamas jana Alhamisi.
Akijibu tuhuma hizo leo Ijumaa Februari 21, 2025, Msemaji wa Hamas, Ismail al-Thwabta, alisema kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, kwamba inaonekana mabaki ya Shiri yalichanganywa na miili mingine chini ya vifusi vya jengo baada ya shambulio la anga la Israeli.
Hamas imesema inachunguza madai ya Israel kwamba moja ya miili iliyokabidhiwa Alhamisi haikuwa ya mateka mwanamke Shiri Bibas.
Hamas imesema: “Kunaweza kuwa na uwezekano wa kosa au kuchanganya miili na iliahidi kutangaza matokeo ya uchunguzi wake kwa uwazi,” imesema Hamas.
Kundi hilo liliongeza kuwa mkanganyiko huo huenda ulisababishwa na mashambulizi ya Israel kwenye eneo ambapo familia hiyo ilikuwa pamoja na Wapalestina wengine.
“Tumepokea madai na tuhuma za uvamizi kutoka kwa ndugu wa upatanishi, na tutachunguza madai haya kwa umakini kamili, na tutatangaza matokeo kwa uwazi,” ilisema taarifa hiyo.
Majibu hayo yalikuja baada ya jeshi la Israel kusema kuwa mabaki ya watoto wawili wa familia ya Bibas, Ariel na Kfir, yalitambuliwa na Taasisi ya Kitaifa ya Tiba ya Uchunguzi wa vifo na Polisi wa Israeli.
Hata hivyo, ilisema kuwa mwili wa tatu haukuwa wa mama yao wa miaka 32, kama Hamas ilivyodai, wala mateka mwingine yeyote.
Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu naye ameendelea kuishutumu Hamas kwa kukiuka makubaliano na kutenda unyama dhidi ya watoto hao na mama yao.
“Tutachukua hatua kwa uthabiti kumrudisha Shiri nyumbani pamoja na mateka wetu wote walio hai na waliokufa na kuhakikisha Hamas inalipa gharama kamili kwa ukiukaji huu mkatili na mwovu wa makubaliano,” amesema Netanyahu.
Kama sehemu ya awamu hiyo, mateka sita walio hai wanatarajiwa pia kuachiliwa na Hamas siku ya Jumamosi kwa makubaliano ya kubadilishana na wafungwa na mahabusu wa Kipalestina 602.
Hamas iliwataja mateka wa Israeli inaotarajia kuwaachia kesho Jumamosi kuwa ni Eliya Cohen, Omer Shem Tov, Tal Shoham, Omer Wenkert, Hisham al-Sayed na Avera Mengisto.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.