Waziri Ndejembi apokelewa kwa vilio mgogoro wa ardhi Handeni

Handeni. Baadhi ya wananchi katika Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wamempokea kwa vilio Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi kwenye eneo lenye mgogoro wa viwanja uliodumu kwa zaidi ya miaka 10.

Wananchi wao wamejitokeza kwenye ziara ya siku moja ya waziri huyo iliyofanyika katika halmashauri ya Mji Handeni, Februari 20, 2025 baada ya kutembelea eneo la kitalu A lenye mgogoro wa ardhi uliosababisha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kuazimia kufunga ofisi ya ardhi.

Mkazi wa Kata ya Kwenjugo, Mwajabu Kilo wakati akitoa malalamiko yake kwa Waziri Ndejembi amesema ameshindwa hadi kumsomesha mtoto wake kutokana na kufuatilia haki zake kwenye viwanja ambavyo vimechukuliwa na halmashauri.

Amesema ana kiwanja chake eneo la kitalu A ambacho ni miongoni mwa vile ambavyo vimepimwa, lakini wakati anafuatilia kupata haki zake, wapo baadhi wa watu walimkataza kufanya hivyo wakimtaka kuacha kufuatilia.

Mwajabu amesema ana miaka minne akifuatilia kuhusu kupata haki zake katika ofisi ya ardhi, lakini amekuwa akizungushwa, huku wananchi wengine waliopewa maeneo wakiendelea kujenga.

“Wale waliojenga waliambia utakapokuja huku kufuatilia kitakachokufika usije ukalalamika na mimi ni mjane nimeshindwa kumpeleka mtoto wangu chuo mwaka wa nne huu, yupo nyumbani na hakuna ufumbuzi ambao umepatikana,” amesema Mwajabu.

Baada ya malalamiko hayo, Waziri Ndejembi ameagiza kuondolewa kwenye nafasi yake Ofisa Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Handeni mkoani Tanga kutokana na kudaiwa kusababisha migogoro ya ardhi.

Amesema amemwagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kumbadilisha ofisa huyo na asipewe kituo kingine, bali aondolewe kama mkuu wa idara ya ardhi kwa halmashauri ya Mji Handeni kwa sababu ameona anahusika kwenye migogoro mingi.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi amekataza viongozi wa ngazi ya wilaya na mkoa kutoingizwa kwenye kamati za uchunguzi wa mgogoro huo, lakini ifike timu kutoka wizarani, Takukuru wakiwemo kuangalia umiliki wa maeneo hayo.

Ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa viwanja vyote na ikibainika yupo mtumishi wa serikali anahusika kumiliki achukuliwe hatua kwani serikali haiwezi kuruhusu watumishi kuchukua ardhi za wananchi.

Diwani kata ya Kwenjugo, Twaha Mgaya amesema mgogo huo unashindwa kufikia mwisho na kuendelea kila siku kwa sababu wapo baadhi ya watumishi wamejimilikisha viwanja kwenye eneo hilo la kitalu A.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Handeni, Mussa Mkombati amemuomba Waziri Ndejembi kuangalia na ofisini kwake, kwani kuna watu wanahusika kupitisha hati ya viwanja huku wakifahamu fika kuna mgogoro.

Baraza la madiwani la halmashauri ya Mji wa Handeni, Jumanne Februari 4, 2025 liliweka azimio la kumtaka mkurugenzi kufunga ofisi ya ofisa ardhi kutokana na mgogoro wa ardhi, eneo la kitalu A ambalo viongozi mbalimbali waliagiza ufanyiwe kazi, lakini hakuna utekelezaji uliofanyika.

Related Posts