Dar es Salaam. Uuzaji wa Malighafi ya kahawa kumeifanya Afrika kuendelea kutumia fedha nyingi katika kuingiza kahawa iliyosindikwa huku ikinufaika kiduchu na mauzo ya nje.
Imeelezwa kuwa Nchi za Afrika kwa pamoja hupata wastani wa dola bilioni 2.5 (Sh6.4 trilioni) kwa mwaka kutokana na mauzo ya kahawa nje ya bara, kati ya Dola za Marekani bilioni 500 zinazopatikana kwenye soko la dunia kwa mwaka.
Haya yamesemwa leo Februari 21, 2025 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati akifungua mkutano wa tatu wa nchi 25 wazalishaji wa kahawa katika Bara la Afrika.
Katika mkutano huu zinajadiliwa fursa zilizopo na namna ambayo vijana wanaweza kujumuishwa katika sekta ya kahawa.
Bashe amesema fedha hizo kiduchu zinatokana na asilimia 90 ya kahawa ya Afrika kusafirishwa kama malighafi, huku thamani yake ikiongezwa nje ya bara la Afrika.
“Hili linamaanisha kuwa Afrika inanufaika kwa sehemu ndogo sana ya mnyororo wa thamani ya kahawa. Sehemu yenye faida kubwa zaidi ya mnyororo huu ni usindikaji na ongezeko la thamani ambalo kwa kiasi kikubwa hufanywa katika nchi zinazoagiza kahawa. Hii inapunguza mapato yetu na nafasi za ajira kwa watu wetu,” amesema Bashe.
Amesema jambo hilo linaathiri hata wauzaji wadogo kwani wanauza kilo 1 ya kahawa kwa wastani wa Dola za Marekani 4 hadi 7 (Sh10,317 hadi Sh18,054) na kisha kuinunua kwa wastani wa Dola za Marekani 15 hadi 20 (Sh38,680 hadi Sh51,000) kwa kilo moja baada ya kusindikwa.
“Hili ni kosa kubwa kwa bara letu. Afrika ndicho chimbuko la kahawa. Huu ni urithi wetu ambao tunapaswa kuulinda na kuhakikisha unastawi,” amesema Bashe.
Amesema Afrika inachangia asilimia 11 tu ya uzalishaji wa kahawa duniani, ambayo ni nusu ya kiwango tulichokuwa tukizalisha miaka ya 1960 wakati ambao uzalishaji wa kahawa duniani unazidi kuongezeka kila mwaka Afrika inashuhudia kupungua kwa uzalishaji.
Jambo hilo linahitaji uwekezaji wa haraka kutoka sekta ya umma na binafsi ili kurejesha sehemu ya soko lililopotea.
“Ni lazima sasa tuache kulalamika na kuwategemea wafadhili kukuza sekta yetu ya kahawa na kilimo kwa ujumla. Ni jambo lisiloeleweka kuwa tunasafirisha kahawa yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 3 (Sh7.75 trilioni) na kuagiza kahawa iliyosindikwa yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 50 (Sh130 trilioni).
“Tunahitaji kuweka malengo ya kuongeza uzalishaji wetu kufikia angalau asilimia 20 ya uzalishaji wa kahawa duniani ifikapo 2030,” amesema Bashe.
Amesema kwa sasa, Afrika inaagiza nusu milioni ya tani za kahawa kwa matumizi ya ndani kwa gharama ya dola za Marekani bilioni 6 (Sh15.6 trilioni) kila mwaka.
Amesema ili kuhakikisha wakulima wa ndani wananufaika zaidi ni vyema kuwekeza katika viwanda vya usindikaji vya kiwango kidogo na kikubwa katika nchi zote zinazozalisha na kutumia kahawa Afrika.
Bashe amesema ni wakati sasa kwa nchi hizi kushikamana na kuacha kutegemea misaada na kudai haki katika biashara ya kimataifa na badala yake kuungana kama bara na kujadiliana kwa pamoja badala ya kufanya kazi kwa kutengana.
Kwa nini vijana hawalimi kahawa
Katika hili Bashe amesema changamoto ya Kupanda na kushuka kwa bei ya kahawa duniani kumeifanya sekta hiyo kukosa mvuto kwa vijana hivyo ili kushughulikia hilo uwekezaji unapaswa kufanyika hasa katika uongezaji wa thamani ndani ya nchi, kuongeza biashara ya kahawa na uwekezaji katika usindikaji.
“Afrika ina soko kubwa la watumiaji lenye watu bilioni 1.5 lakini sehemu kubwa ya kahawa inayotumiwa barani huagizwa kutoka nje baada ya kusindikwa nje ya bara letu. Hili linapaswa kubadilika kwa kuhamasisha usindikaji wa ndani na kuifanya kahawa kuwa sehemu ya utamaduni wetu,” amesema Bashe.
Amesema vijana wanapaswa kuwa kiini cha sekta ya kahawa kwa kuwawekea mbinu rafiki za kilimo na kuweka kipaumbele katika ustawi wa wakulima.
“Kwa kufanya hivi tunaweza kuhakikisha kuwa sekta ya kahawa Afrika inastawi kwa vizazi vijavyo. Mafanikio haya hayawezi kupatikana bila ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, na vyama vya kahawa,” amesema Bashe.
Amesema hilo linawezekana kwa sababu Afrika ina ardhi yenye rutuba, rasilimali za maji na nguvu kazi ya vijana na hakuna sababu ya Afrika kushindwa kuongeza uzalishaji wake wa kahawa na kufaidi kikamilifu thamani ya zao hilo.
“Ni wakati wa kubadili mwelekeo kutoka kuwa wasafirishaji wa malighafi kwenda kwenye kuongeza thamani na kutengeneza bidhaa zilizokamilika. Ni lazima tuongeze biashara kati yetu wenyewe kutoka asilimia 15 hadi asilimia 50 jambo ambalo haliepukiki, na hii inapaswa kuwa moja ya maazimio hapa Dar es Salaam,” amesema Bashe.
Amesema kinachotakiwa kufanyika sasa ni kuweka malengo kwamba ifikapo mwaka 2030 nchi zote zinazotumia kahawa Afrika zinunue kahawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji wa Kiafrika.
Amesema jambo hilo linawezekana na litafungua fursa nyingi za ajira kwa vijana na uwekezaji katika uchumi wa mzunguko.
Tanzania inavyovutia vijana
Akizungumzia kinachofanyika Tanzania, Waziri Bashe amesema katika kuvutia vijana katiki kilimo cha kahawa tayari imeanzisha mradi wa kuuza kahawa mitaani kupitia migahawa inayotembea.
Mradi huu unatekelezwa chini ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT) ambapo vijana wanapatiwa vibanda vya kahawa vilivyo na vifaa vyote na mtaji wa kuanzia ili wawe wauzaji wa kahawa katika miji yetu.
“Pia Tanzania imejizatiti kuleta mageuzi katika sekta ya kahawa kupitia hatua kama vile kuimarisha taasisi za utafiti wa kahawa, kutoa ruzuku za pembejeo kwa wakulima, na kukuza ushiriki wa vijana kupitia programu ya BBT,” amesema Bashe.
Mkurugenzi bodi ya kahawa
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Primus Kimaryo amesema sekta hii ina uwezo mkubwa wa kuhamasisha maendeleo ya kiuchumi, kukuza ubunifu na kuinua nafasi ya Afrika katika soko la kahawa la kimataifa.
Hata hivyo, licha kuwa ni kitovu cha masoko ya kahawa ya Arabica na Robusta, Bara la Afrika halijaweza kutumia kikamilifu uwezo wa kahawa yake.
“ Wito wangu kwa serikali za Afrika ni kuwekeza katika ongezeko la thamani, kuimarisha biashara ya kahawa kati ya nchi za Afrika,”
“Kuwawezesha wajasiriamali vijana na kuwaleta vijana katika mustakabali kwa kuwawezesha na kuwapa stadi, fedha na fursa za kubadili sekta ya kahawa kuwa injini inayoleta ajira na ukuaji wa kiuchumi,” amesema Kimaryo.