Tanzania kumaliza utegemezi wa ngano 2035

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (Copra), imesema hadi ifikikapo mwaka 2035 Tanzania inalenga kuzalisha ngano tani milioni moja kwa mwaka hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi.

Kwa sasa asilimia 90 ya ngano inayotumika Tanzania inaagizwa kutoka nje ya nchi huku uzalishaji wa ndani ukiwa ni tani 100,000 sawa na asilimia 10.

Mkakati huo umebainishwa leo Februari 21, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Copra, Irine Madeje alipozungumza na wadau wa zao la ngano jijini Dar es Salaam.

“Zao la ngano lina mchango katika kukuza uchumi wa nchi yetu, lakini bado kuna uzalishaji mdogo wa zao hilo kwani tunazalisha tani 100,000 ukilinganisha na mahitaji ni tani milioni moja  ambayo ndio matumizi yetu ndani ya nchi,” amesema Madeje.

Irene ameongeza kuwa kwa kusema “tumebalikiwa ardhi, maji, watu, uwezo na hali lakini kama nchi bado tunaingiza ngano asilimia 90 kutoka nje ya nchi,” amesema.

Aidha amesema Serikali imeona kuna haja ya kuweka mkakati wa kuendeleza zao la ngano nchini, ambao utatekelezwa kwa muda wa miaka 10 (kuanzia 2025 hadi 2035).

Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Uendelezaji Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Marko Mgheke amesema hiyo ni taasisi ya umma inayomiliki viwanda sita vya ngano lakini mara nyingi hukumbwa na changamoto ya malighafi hadi kulazimika kuiingia mikataba na wakulima wauziwe wao.

“Tulienda kwenye mikoa inayolima ngano kukutana na wakulima na kuingia nao mikataba watuuzie sisi tu ngano yao lakini bado tukawa na uhaba wa malighafi viwandani kwetu,” amesema Mgheke.

Aidha amesema wanakutana na changamoto kutoka kwa wakulima mara baada ya kuingia nao mikataba ya kuwataka wasiuze kwa mtu mwingine, lakini ifikapo kipindi cha kuuza wakulima hao huwauzia watu wengine.

Mchakataji wa ngano kutoka Kampuni ya Bakhresa, Egbert Mpanzile amesema uhaba wa ngano hapa nchini ni hali ya juu ukilinganisha na mahitaji hasa wao wenye viwanda vinavyozalisha bidhaa zitokanazo na ngano.

“Sisi Bakhresa tuna viwanda vitatu vinavyozalisha bidhaa zitokanazo na ngano mfano kiwanda cha Buguruni kinahitaji tani 2250, kiwanda cha mzizima tani 5,000 na kiwanda cha kipawa tani 150,000 lakini hatujawahi kupata idadi hio,” amesema Mpanzile.

Mkurugenzi wa Biashara na Mawasiliano kutoka Kampuni ya Azania, Joel Laiser amesema kwenye kampuni yao hawajawahi kutosheka kuhitaji ngano.

“Wakulima wa ngano Tanzania watumie njia ya kisasa ili waweze kuzalisha ngono nyingi ili waweze pia kuuza kimataifa,” amesema Laiser.

Isaya Wanga, mkulima wa zao la ngano kutoka Mkoa wa Arusha amesema kuna haja kwa serikali kuwasaidia wakulima wa zao hilo kupata mbegu za kisasa na kuwahakikishia soko.

“Serikali inabidi kutusaidia wakulima wa zao la ngano kupata mbegu za kisasa zitakazotusaidia kupata bidhaa bora zaidi,” amesema.

“Pia tuwahakikishiwe soko maana kuna mikoa kama mitatu hivi mteja wetu mmoja kuna wakati inabidi atukope sababu anazidiwa na bidhaa,” amesema Mwanga.

Related Posts