Njia hizi zinaweza kukutoa kwenye uraibu wa simu, mitandao

Dar es Salaam. Wakati kasi ya matumizi ya simu za mkononi ikizidi kuongezeka duniani, imeelezwa kuwa matumizi kupita kiasi ya kifaa hicho ni uraibu unaoweza kuleta madhara makubwa kwa mtumiaji.

Katika miongo michache iliyopita, simu zimebadilika kutoka kuwa zana za mawasiliano hadi kuwa kifaa cha kidijitali kilichojumuisha kila kitu, na sasa dunia yote inawezekana kufikiwa kwa kugusa kidogo tu kwenye skrini.

Kwa mujibu wa tovuti ya therapybrands kifaa hicho cha mawasiliano kimewafanya watu kupunguza muda wa kufanya kazi na kuchangamana na wengine na kujikuta wakitumia muda mwingi kuperuzi kwenye mitandao ya kijamii.

Wanasaikolojia wameeleza kuwa matumizi yaliyokithiri ya simu yanachangia kupunguza uwezo wa watu kujieleza na kujiamini kwani wapo ambao wanakosa ujasiri wa kuzungumza na mtu uso kwa uso na kuishia kutoa hisia zao kwenye mitandao.

Kwa mujibu wa mwanasaikolojia Christine Philip aliyenukuliwa kwenye makala iliyochapishwa katika tovuti hiyo, uraibu huu unaweza kumfanya mtu ajishushe thamani yake, akiamini maisha ya watu anayoyaona mtandaoni ni mazuri kuliko anayoishi.

Mitandao humsababishia pia mtu kujitenga, kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi, kutothamini uhusiano wake na watu, kuwa na hali ya kutotamani kupitwa na chochote mtandaoni na hata kupata sonona.

Tovuti hiyo imekwenda mbele na kueleza dalili za uraibu huu ni kutumia simu na mitandao ya kijamii wakati wa kazi au masomo, kuongeza matumizi ya ukiwa na familia, marafiki au hata wakati wa kula, kuitumia mitandao ya kijamii kama njia ya kujisahaulisha pale unapopata tatizo

Nyingine ni kujihisi hauko sawa unapokuwa mbali na simu yako, kuwaza  kuhusu yanayoendelea mtandaoni pale unaposhindwa kuingia au kuwa mbali na simu na kuifanya kuwa ni kitu cha kwanza pale unapofumbua macho na kuianza siku.

Akizungumza na Mwananchi mtaalamu wa saikolojia, Severin Hyera ameeleza kuwa mambo yakiendelea kuwa kama ilivyo sasa kuna uwezekano mkubwa wa hali kuwa mbaya zaidi miaka 10 hadi 15 ijayo.

“Tujiulize kama mtu ambaye alizaliwa kabla ya simu za mkononi na mitandao ya kijamii imemuathiri kiasi kwamba hafurahii uwepo wa mtu mwingine, vipi kuhusu hawa watoto wanaozaliwa na kuikuta mitandao, tatizo litakuwa kubwa kiasi gani.

“Uwezekano wa watu kujieleza itakuwa ni tatizo kubwa sana, hivyo inaweza kuathiri hata uchumi kwa kuwa utawezaje kufanya biashara bila kuwasiliana, kuathiri utendaji kazi maana unawezaje kumuajiri mtu hawezi kujielezea, hawezi kuwasilisha ripoti wala kusimama kujieleza mbele za watu.

Kando na hilo mtaalamu huyo alieleza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa watu wanaotumia muda mrefu kwenye mitandao ya kijamii ndio wanaongoza kuwa na msongo wa mawazo.

Hali hii inasababishwa na nini?

Mtaalam huyo alieleza kuwa kulingana na tafiti utumiaji uliopitiliza wa mitandao ya kijamii ni matokeo ya mitandao hiyo kuwa na uwezo wa kutengeneza kemikali iitwayo dopamine ndani ya mwili wa binadamu.

Amesema kemikali hiyo inazalishwa ndani ya ubongo ambayo kazi yake kubwa ni kumfanya mwanadamu ajisikie vizuri. Mfano mtu akipewa zawadi au kupongezwa.

“Kwa kawaida kila mmoja anapenda kujisikia vizuri mara nyingi unapokuwa na mchezo unaokufanya ujisikie vizuri ni rahisi kuurudia ili uendelee kujisikia vizuri. Hivyo hii mitandao ya kijamii kwa namna tunavyoingiliana na watu na hata kutumia lugha ya alama kama zile emoji inachochea uzalishaji wa hiyo kemikali.

“Matokeo yake utumiaji wa mitandao ya kijamii kwa watu wengi imewatengenezea uraibu kwa sababu ya hii hisia nzuri ndio maana utakuta unaongea na mtu dakika chache anatoa simu yake kuiangalia,”.

Hyera amesema kemikali hiyo ya raha si rahisi kupata kutoka kwa mtu ukiwa naye uso kwa uso kama hujamfanyia au kukufanyia jambo jema.

Kupitia mitandao ni rahisi mtu kupata raha pale anapofungua whatsapp na kukutana na meseji, au akiingia Instagram, Facebook na kukuta meseji, likes au comments kemikali hiyo inatolewa na unajisikia raha.

“Kemikali hii ndio kiini cha tatizo, inawafanya watu waingie kwenye uraibu bila wao kufahamu, ikitokea amekerwa kidogo anakimbilia kwenye mitandao kupata raha.

Hii kemikali kwa binadamu ni muhimu na wengine wanaitafuta kwa gharama kubwa lakini mitandao ya kijamii imesaidia hii kemikali kuachiliwa kwenye ubongo kwa namna nyepesi”, amesema mwanasaikolojia huyo.

Unawezaje kujinasua na uraibu huu

Kwa mujibu wa mwanasaikolojia huyo mambo matatu yanaweza kumsaidia mtu kutoka kwenye uraibu wa matumizi ya mitandao ya kijamii yaliyokithiri.

Jambo la kwanza ni mhusika kutambua kuwa hilo ni tatizo na awe tayari kufanya kila namna kujinasua kwenye tatizo hilo.

“Yaani ukijiona pale unapoamka asubuhi kitu cha kwanza ni simu, upo na wenzako lakini akili yako yote ipo kwenye simu hizo ni dalili kuwa umeishaingia kwenye uraibu wa kutumia mitandao ya kijamii.”

Jambo la pili ni kujiweka mbali na simu, “Unapokuwa na watu jitahidi kuweka simu mbali, usiku zima simu iache sebuleni au weka mbali na kitanda hii itakusaidia kukabiliana na uzalishaji wa kemikali hii ambayo inakudanganya kuwa mambo ni shwari.

Tatu ni kuruhusu ubongo ukae huru ili akili ifanye kazi mbali na simu, “Akili ya binadamu inapata ubunifu kwa kuangalia mazingira yanayomzunguka, kwa hiyo unapojizuia kuwa na mwingiliano na mazingira, inatujengea hali ya ubunifu na kupata mawazo mapya,”amesema Hyera.

Related Posts