Washirika wa Maendeleo wameonesha kuridhishwa na Sera za Maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ikiwa ni pamoja na Mipango ya thabiti ya kushirikiana na washirika hao wa maendeleo ili kuweza kutekeleza malengo yaliyokusudiwa katika Sekta ya Uchumi kulingana na mikakati iliyowekwa.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mku wa Wizara ya Fedha Zanzibar Juma Malick Akil aliyemuwakilisha Katibu wa Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKt Elmaamry Mwambao katika Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na wadau wa Maendeleo.
“Tumejipima tukiwa na wenzetu katika mchakato wetu wa kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii na nafasi ya washirika katika kuendelea kutoa ushirikiano wao kwa Serikali katika mipango yetu ya maendeleo tuliojiwekea,” alisema.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Morisali Milanzi amesema, Mpango wa Dira Mpya ya 2050 utalenga katika miradi itakayokuza ajira na kutupatia fedha za kigeni ikiwa ni pamoja na kuinua Sekta nyingine.
“Sekta ya Kilimo na Viwanda zina ukaribu, kwa sababu Sekta ya Viwanda inategemea malighafi kutoka Sekta ya Kilimo halikadhalika Sekta ya Viwanda inapeleka malighafi katika Sekta ya Kilimo hivyo tunataka tuzitumie vizuri kulingana na mfungamano wake kiuchumi.”
Amefafanua kwamba nafasi ya nchi kijiografia kwa sisi tunaosaidia nchi nyingine zilizotuzunguka katika usafirishaji kwa kutumia Reli, Bandari na Barabara ni lazima nchi inufaike kiuchumi.
“Lakini katika eneo la kijiografia tuna madini tunapaswa kuyatumia vizuri ili yatunufaishe huo ndio ujumbe ambao tunataka Washirika wetu wa Maendeleo wajue,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza anayewakilisha Washirika wa Maendeleo, Susan Ngongi Namondo alisema kuwa Tanzania imepiga hatua katika sekta za afya, miundombinu, na mageuzi ya sera, huku akibainisha maeneo matatu muhimu ambayo yatajadiliwa katika mkutanao huo kuwa ni utulivu wa uchumi wa taifa, ukuaji shirikishi, na uthabiti wa mabadiliko ya tabianchi.
Namondo alisema kuwa Tanzania imeonyesha uimara mkubwa wa kiuchumi na usimamizi thabiti wa sera za fedha, lakini maendeleo ya haraka yanahitaji ushiriki mkubwa wa sekta binafsi, mageuzi ya kifedha, na mikakati madhubuti ya kupunguza umasikini.
Kwenye eneo la mabadiliko ya tabianchi na nishati, Mwenyekiti Mwenza huyo alisema kuwa juhudi za Tanzania kama vile Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia na Mkakati wa Nishati Jadidifu ni hatua muhimu, lakini uwekezaji zaidi unahitajika ili kuimarisha ujumuishaji wa nishati mbadala na kuongeza uthabiti wa mabadiliko ya tabianchi.
Susan Ngongi Namondo aliahidi kuwa Washirka wa Maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kuhakikisha nchi inapata maendeleo zaidi ya kiuchumi na kijamii.