Songwe. Wakati mkoa wa Songwe ukishika nafasi ya pili kitaifa kwa uzalishaji zao la kahawa aina ya Arabika, Serikali mkoani humo imesema inahitaji kuongeza uzalishaji wake kutoka tani 11,355 hadi 32,617 ifikapo mwakani 2025.
Hayo yamebainishwa leo Mei 16, 2024 wakati wa hafla ya kufunga mafunzo kwa wakulima 681 wa zao hilo kutoka vyama sita vya ushirika (Amcos) vya Alungu, Ruanda, Hatelele, Ngh’amba, Malolo na Hasamba vya wilayani Mbozi mkoani humo yaliyoandaliwa na shirika la Sustainable Growers Rwanda (SGR).
Hafla hiyo imeambatana na ugawaji zawadi kwa wakulima waliofanya vizuri katika mafunzo ya kilimo cha zao hilo ikiwamo ng’ombe, mbuzi, godoro na vifaa vya kilimo vilizogharimu zaidi ya Sh200 milioni.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Songwe, Daniel Chongolo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi amesema ikiwa mkoa huo unashika nafasi ya pili kitaifa, wanahitaji kuongeza uzalishaji.
Amesema ipo mikakati ya Serikali kuinua kilimo hicho mkoani humo ikiwa ni pamoja na kuzalisha miche bora kufikia milioni 30, kuboresha vyama vya ushirika (Amcos) na chama kikuu (Soreku) ili kufikia malengo.
“Hivyo mikakati yetu ni kuongeza uzalishaji kutoka tani 11,355 hadi 32,617 ifikapo 2025 na kuongeza ubora wa kahawa yetu kutoka asilimia 35 hadi 70 na serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau wa kilimo hiki ili kufikia malengo.
“Zipo changamoto mbalimbali zinaliharibu zao hili ikiwamo magonjwa, mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa vitendea kazi, hivyo tutapambana kuhakikisha tunatatua matatizo haya hatua kwa hatua,” amesema Farida.
Mkurugenzi Mkuu wa shirika la SGR, Christine Condo, amesema lengo ni kuona wanaongeza ufanisi kwa wakulima hasa wanawake wilayani Mbozi ikiwa ni kuwajengea uwezo katika kuandaa zao la kahawa na kuwainua kiuchumi kuanzia ngazi ya familia na kijamii.
Amesema licha ya mafunzo hayo kwa awamu ya kwanza kulenga wanachama wa Amcos, lakini hata walio nje ya vyama vya ushirika wanaweza kupatiwa elimu hiyo na kwamba pia wanawahamasisha kupitia zawadi mbalimbali.
“Zaidi tunaomba ushirikiano kwani baada ya mafunzo haya, yatafuata ya hatua ya pili ya elimu ya udhibiti ubora masoko, tunaishukuru serikali ya Tanzania, TCB chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupokea,” amesema Christine.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa nchini (TCB), Primus Kimaryo amesema kutokana na Mkoa wa Songwe kuathirika na ukame, kipindi cha kiangazi watachimba visima 10 kwa ajili ya umwagiliaji kusaidia wakulima kufanya shughuli zao kwa ufanisi.
“Sasa shikeni sana kilimo cha kahawa, leo mmepata ng’ombe, mbuzi na zawadi nyingine, msije kupotea mkajificha kwenye ufugaji bali siku tukikutana tena tuone uzalishaji ukiwa mkubwa ili zawadi ziongezeke” amesema Kimaryo.
Mkulima Everine Sinkonde aliyejishindia ng’ombe, amesema mbali na kunufaika na zawadi hizo, lakini mafunzo yamewajenga kuanzia namna ya kuandaa kilimo cha kahawa pamoja na uongozi kwa wanawake.
“Ni faraja kubwa, kwa sasa tunaomba mafunzo haya yawe endelevu japokuwa tumefaidika na namna bora ya kuandaa kilimo hiki kuanzia kupanda, kukuza na kuvuna,” amesema Everine.
Kwa upande wake, Regina Rapahel ambaye ni mnufaika wa shirika hilo, amesema elimu waliyoipata imewapa uwezo wa kubaini kilimo cha kahawa si cha wanaume bali hata wanawake wanaweza.
“Imetuondolea ile dhana ya kwamba kilimo cha kahawa ni cha mwanaume, kumbe hata wanawake nao wanaweza kupata heshima kupitia kahawa. Tulitumia majani ya zao hili kama majani ya chai, lakini sasa tumejua kwamba hata mbegu zake zinatengeneza kinywaji,” amesema Regina.