Dar es Salaam. Wakati joto la uchaguzi likizidi kupamba moto, kuna sintofahamu kwenye mchakato wa kuwapata wabunge na madiwani wa viti maalumu ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).
Hatua hiyo imewalazimu wabunge na madiwani waliopo madarakani sasa kuhaha kutengeneza mazingira, ikiwemo mbinu chafu kama zilizokemewa na viongozi wa juu cha CCM katika kuhakikisha wanatetea nafasi zao.
Habari kutoka kwenye korido za CCM na miongoni mwa wabunge na madiwani hao, zinadai jumuiya za chama hicho (Umoja wa Vijana-UVCCM) na Wazazi nazo zinataka kupata nafasi sawa za uwakilishi bungeni na kwenye mabaraza ya madiwani kama ilivyo kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT).
Kutokana na uwepo wa taarifa hizo, inaaminika nafasi za uwakilishi kupitia UWT bungeni zitapungua ili kutoa nafasi kwa wawakilishi kutoka Wazazi na UVCCM.
Kwa sasa CCM ina wabunge wa viti maalumu 94 waliotokana na makundi mbalimbali kupitia uwakilishi UWT na Vijana. Endapo kutakuwa na mgawanyo sawa, basi idadi ya UWT kutoa wabunge itapungua katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 2025.
Hata hivyo, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla akizungumza na Mwananchi jana Ijumaa, Februari 21, 2025 amesema nafasi ya viti maalumu ni mali ya chama cha siasa.
Makalla ambaye ametembelea ofisi za Mwananchi Communications Limited (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam amesema:
“Viti maalumu ni mali ya chama cha siasa, sasa kwa kuwa CCM ina UWT basi inapewa dhamana ya kuwapata wabunge wa viti maalumu. Inawezekana mjadala ukawepo kwamba wapo kinamama walioko Jumuiya ya Wazazi, wapo kinadada walioko UVCCM, hii keki yote ya kwetu basi tuongezewe…
“Niseme tunalifanyia kazi, tutakapokaa vikao kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi CCM itatoa utararibu. Marekebisho yalifanyika kuhusu utaratibu wa kupiga kura za maoni ya kuwapata wabunge wa majimbo, wawakilishi na madiwani wanaotokana na CCM, lakini kutakuwa na marekebisho mengine yatakayoongeza wigo wa namna ya kuwapata wabunge wa viti maalumu,” amesema.
Hata hivyo, Makalla amesisitiza CCM bado inaamini UWT ndiyo yenye jukumu la kuratibu kwa kina mchakato huo, huku akiweka wazi kuwa suala la mgawanyo sawa kwenye nafasi hizo halitakuwepo.
Ukiachana na misuguano ya wanaowania ubunge huo ndani ya CCM, nafasi za viti maalumu zimepitia msukosuko mwingine wa shinikizo la ukomo.
Wanaojenga hoja ya kuwepo ukomo katika nafasi hizo wanasema miaka mitano kwa maana ya kipindi kimoja kinamtosha mbunge kujiimarisha kiuchumi na kisiasa kwenda kushindana jimboni.
Wanarejea msingi wa kuanzishwa kwa nafasi hizo kuwa ni kuwainua na kuwajengea uwezo wanawake.
Uwepo wa baadhi ya wabunge kupitia viti maalumu waliokaa bungeni kwa zaidi ya miaka 15 umeibua mvutano kutokana na makada wanaochipukia kushindwa kushindana kwa sababu mbalimbali, zikiwemo za kiuchumi.
Kutokana na hilo, shinikizo la kuwepo kwa ukomo limekuwa shubiri kwa waliopo kwenye nafasi hizo, lakini linatazamwa kuwa linaweza kuwa ahueni kwa wale walio nje ya ubunge, wenye nia ya kugombea viti maalumu.
Hata hivyo, nafasi za ubunge wa viti maalumu si lelemama, huwa na mchuano mkali miongoni mwa makada wa chama hicho kutokana na uwepo wa idadi ndogo ya wapigakura wanaoweza kufikika kwa urahisi, tofauti na kuwania kwenye majimbo ya uchaguzi.
Hata lile onyo la Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi halikulenga wabunge wa nafasi za majimbo pekee, linawahusu makada wenye nia ya kusaka nafasi za ubunge na udiwani wa viti maalumu.
“Nataka wajue kuwa CCM ina mfumo wa kufuatilia kila kinachotokea. Nataka wajue kuwa tunachukua kumbukumbu ya matukio wanayoyafanya. Na kumbukumbu hizo ndizo zitakazowafanya waje washangae kitakachotokea nini? Kwa sababu kwa hakika tutaengua majina yao.
“Labda kama wana hamu ya kutumia fedha zao kama sadaka ya kugawa na hawahitaji chochote katika chama chetu waendelee tu, tunawatakia heri lakini kama wanataka tugombee na visingizio vya kuzaliwa na kumbukumbu za marehemu bibi na ndoa waendelee tunawafuatilia,” alisema Dk Nchimbi alipozungumza na viongozi wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini.