Championship bado vita ni nzito

BAADA ya jana kushuhudia michezo miwili ya Ligi ya Championship, kipute hicho kitaendelea tena leo kwa mingine mitatu kupigwa kwenye viwanja mbalimbali, ikiingia mzunguko wake wa 20, kwa lengo la kuzisaka pointi tatu muhimu kwa kila timu.

Michezo yote mitatu leo itaanza saa 10:00 jioni na Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Mbuni iliyoichapa Biashara United mabao 3-2, itaikaribisha Songea United yenye kumbukumbu ya kuichapa Mtibwa Sugar bao 1-0.

Mtibwa Sugar baada ya kuchapwa mchezo uliopita, itakuwa kwenye Uwanja wa Manungu Complex kuikaribisha maafande wa Polisi Tanzania, yenye kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2, mechi ya mwisho nyumbani dhidi ya Transit Camp.

Mchezo wa mwisho leo, utapigwa kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi na wenyeji Bigman FC iliyotoka kuichapa Cosmopolitan bao 1-0, itacheza na Stand United ‘Chama la Wana’, yenye morali pia baada ya kuichapa TMA ya Arusha mechi ya mwisho mabao 2-1.

Kesho Jumapili itapigwa pia michezo mitatu na Mbeya Kwanza iliyochapwa bao 1-0, dhidi ya maafande wa Green Warriors, itakuwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara kuikaribisha Biashara United iliyotoka kuchapwa mabao 3-2 na Mbuni FC.

TMA ya jijini Arusha iliyotoka kuchapwa mabao 2-1 na Stand United, itajiuliza nyumbani mbele ya Mbeya City yenye kumbukumbu na morali nzuri ya mchezo uliopita, ilipoishushia kichapo kizito African Sports kutoka Tanga cha mabao 5-2.

Raundi ya 20, itahitimishwa kwenye Kituo cha Ufundi cha TFF, Mnyanjani mjini Tanga na African Sports iliyokutana na dhahama mchezo uliopita ugenini mbele ya Mbeya City, itaikaribisha Geita Gold iliyotoka kuichapa Kiluvya United mabao 3-0.

Kocha wa African Sports, Kessy Abdallah alisema kichapo ilichokipata mchezo wa mwisho kwa kiasi kikubwa kiliwatoa nyota wa timu hiyo mchezoni, ingawa amekaa nao chini na kuwajenga kisaikolojia, huku akiwataka kujipanga na michezo mingine.

“Kwa kiasi kikubwa iliwatoa wachezaji mchezoni kwa sababu unapofungwa idadi kubwa ya mabao kama ile ni lazima hali hiyo itokee, tunarudi uwanja wetu wa nyumbani ili kusahihisha makosa yaliyojitokeza hususani eneo la ulinzi kwa jumla.”

Related Posts