Na Seif Mangwangi,Arusha
HATIMAYE Mwendesha mashtaka wa Serikali (DPP), ametoa idhini ya kesi inayomkabili mwekezaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini, Salehe Salim Almamry pamoja na wakili Sheki Mfinanga kesi yao kuanza kusikilizwa katika mahakama kuu kitengo cha rushwa na uhujumu uchumi masjala ndogo Mahakama Kuu kanda ya Arusha.
Kufuatia idhini hiyo, huku wakitakiwa kutokujibu chochote kufuatia mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo, washtakiwa hao kwa pamoja Februari 20, 2025 wamesomewa mashtaka yao ya awali ambapo kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 60 ikiwemo shtaka la utakatishaji wa fedha na uhujumu uchumi.
Akiwasomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Erasto Philly, Mwendesha mashtaka wa Serikali Edga Bantulaki akisaidiwa na waendesha mashtaka wengine, Jackline Mosha na Allawi Miraji pamoja na mwendesha mashtaka wa Takukuru Yona Msengi, Bantulaki ameiambia mahakama kuwa upande wa mashtaka umekamilisha ushahidi na watakuwa na mashahidi 80.
Amesema miongoni mwa mashahidi katika kesi hiyo ni pamoja na wafanyabiashara wakubwa ambao mtuhumiwa namba moja Salehe Almamry akiwa mkurugenzi wa kampuni ya kitalii ya Tarangire Sunset anatuhumiwa kuwatumia kutakatisha fedha, nyaraka 461 za ushahidi wa kimaandishi pamoja na nyaraka 12 za ushahidi unaooneka.
Bantulaki ameiambia mahakama kuwa katika kesi hiyo mtuhumiwa Salehe Almamry anadaiwa kufanya utakatishaji wa fedha wa zaidi ya bilioni 60 baada ya kuwadhulumu wabia wenzake wawili katika kampuni ya Tarangire Sunset ndugu wawili raia wa Saudi Arabia, Khalid Alraj na mwenzake Abdulkarim Alraji.
Amesema mbali ya kuhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha pia watuhumiwa hao wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu, kughushi nyaraka mbalimbali, kutoa taarifa za uongo kwenye mamlaka za kiserikali kwa njia ya kujipatia fedha isivyo halali.
“Mheshimiwa Hakimu, katika shtaka namba 16, mtuhumiwa Saleh Almamry anadaiwa kughushi nyaraka iliyokuwa ikionyesha wabia wenzake Abdulkareem Mohamed Alraj na Khalid Alraji kukubali hisa zao asilimia 18 kuchukuliwa kitu ambacho sio kweli,”ameiambia mahakama.
Amesema mashtaka hayo yote ameyafanya kati ya machi 2019 na Mei 2024 kabla ya upelelezi kufanyika na kutiwa hatiani katika mahakama hiyo na kwamba makosa yote hayo amekuwa akiyafanya katika mikoa ya Arusha, Manyara, Pwani na Dar es salaam.
Kufuatia mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo Erasto Philly aliiambia mahakama kuwa mtuhumiwa namba moja Saleh Almamry ataendelea kukaa mahabusu kwa kesi yake haina dhamana na mtuhumiwa namba mbili Wakili Sheki Mfinanga ataendelea na dhamana yake mpaka kesi hiyo itakapoanza kusikilizwa mahakama kuu kitengo cha uhujumu uchumi.
Amesema ilichofanya mahakama hiyo ni kusikiliza maelezo ya awali baada ya upelelezi kukamilika na watuhumiwa watafikishwa mahakama ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha baada ya Naibu Msajili wa mahakama kuu kutoa taarifa ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo.
Nje ya mahakama
Akizungumzia shauri hilo, Wakili Mosses Mahuna anayemtetea mshtakiwa namba moja Saleh Salum Almamry ameishukuru ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali kwa kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo na kuiomba mahakama kuharakisha usikilizwaji wake kwa kuwa mteja wake ameshakaa mahabusu kwa muda mrefu.
Amesema mteja wao anafamilia kubwa inayomtegemea pamoja na Mama yake ni mgonjwa ambaye aliugua ghafla baada ya kusikia mwanae anashikiliwa mahabusu hivyo kuendelea kucheleweshwa kwa kesi hiyo kunazidi kuweka maisha ya familia yake katika hali ngumu.
“Hata hivyo nina Imani kubwa na Serikali kwa kuwa upelelezi umeshakamilika najua ndani ya wiki moja tutaitwa ili kesi yetu ianze kusikilizwa, na ujue upande wa mashtaka una mashahidi 80 hao ni wengi sana na wote itabidi wahojiwe kwa hiyo ikianza kusikilizwa mapema haitachukua muda mrefu,”amesema.
Wakili Faisal Rukaka ambaye pia anamtetea mtuhumiwa namba moja Saleh Alammary amesema wameshindwa kutaja idadi ya mashahidi itakaowafikisha mahakamani hapo kwa kuwa kesi rasmi bado haijaanza lakini muda ukifika itaweka wazi.
Miongoni mwa mashahidi wa jamhuri ni pamoja na mfanyabiashara na mkulima mkubwa Gerald James Milla, Said Iddi Kipingu, wakili John Beatus Kasegenya, Abdull Said Msalaam, Suleiman Nkya, Abdulkareem Mohamed Alraj, Khalid Alraj na Abano Gilla.
Mwendesha mashtaka mwandamizi ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali Edga Bantulaki
Mawakili Faisal Rukaka, Mosses Mahuna na Mariam Mrutu wanaowatetea watuhumiwa Saleh Almamry na Sheki Mfinanga wakiwa mahakamani