Jinsi misitu inavyoweza kuondoa hasira za wanandoa

Dar es Salaam. Dunia ya sasa inashuhudia matumizi makubwa ya teknolojia na kazi za ofisini, hali inayowafanya watu wengi kukosa muda wa kufurahia utulivu wa mazingira ya asili.

Watu wengi wanakumbana na changamoto za kiakili na kimwili kutokana na mzigo wa kazi na mafadhaiko ya kila siku. Hata hivyo, mazingira ya asili, kama vile misitu na maeneo yenye majani ya kijani kibichi, yanatajwa kuwa na manufaa makubwa kwa afya ya binadamu.

Utafiti wa wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Harvard nchini Marekani uliofanywa mwaka 2019 umeonyesha kuwa kuishi karibu na maeneo yenye misitu kuna faida kwa afya ya mwili. Utafiti huu, uliochapishwa na taasisi ya Environmental Health Perspectives, unathibitisha kuwa watu wanaoishi katika maeneo yenye misitu wana hatari ndogo ya magonjwa kama shinikizo la damu na kisukari.

Aidha, utafiti uliofanyika nchini Japan mwaka 2017 ulionyesha kuwa kutembelea misitu hupunguza shinikizo la damu na kudumisha afya ya moyo.

Uchunguzi uliofanywa kwa watu waliokuwa na matatizo ya shinikizo la damu ulionyesha kuwa walipopelekwa msituni, waliona mabadiliko chanya katika hali zao. Shinikizo la damu lilipungua na kurudi katika hali ya kawaida ndani ya dakika chache baada ya kuingia katika mazingira ya misitu.

Utafiti mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Stanford mwaka 2015 ulithibitisha kuwa mazingira ya asili yanasaidia kupunguza kiwango cha homoni ya cortisol, inayohusiana na msongo wa mawazo.

Wataalamu walifanya majaribio kwa kumpeleka mtu mwenye msongo wa mawazo ndani ya msitu, na waliona mabadiliko chanya katika hali yake baada ya saa mbili tu.

Watu waliokuwa na msongo wa mawazo waliona dalili za utulivu na kupungua kwa wasiwasi na mfadhaiko baada ya kukaa katika mazingira ya kijani kibichi, ambapo hali ya hewa ni safi na tulivu.

Utafiti wa mwaka 2010 ulionyesha kuwa kutembelea misitu na kuvuta hewa safi kutoka kwa miti mchanganyiko husaidia kuboresha kinga ya mwili.

Hewa hii inatajwa kuwa na virutubisho kutoka kwenye miti vinavyosaidia mwili kupambana na maambukizi ya magonjwa.

Utafiti mwingine kutoka Chuo Kikuu cha Ulster nchini Uingereza mwaka 2011 ulibainisha kuwa watu walioshiriki shughuli za asili walionyesha mabadiliko chanya katika afya ya akili, hasa ikilinganishwa na wale waliokaa katika maeneo ya mijini yenye kelele na uchafuzi wa mazingira. Utafiti huu unaonesha kuwa mazingira ya asili yanasaidia kupunguza mfadhaiko, kuongeza furaha na kuboresha hali ya akili kwa ujumla.

Nchi kama Marekani zimeanzisha maeneo maalumu ya misitu kwa ajili ya watu wanaohitaji kupumzika na kutuliza mawazo yao.

Mfano wa kambi moja nchini humo imeanzisha maeneo ya msitu ambapo wanandoa wanakwenda kupiga kelele, kuchapa miti na kuvuta hewa safi baada ya hasira zao kuisha.

Msitu mwingine maarufu ni Aokigahara nchini Japan, unaotajwa kuwa miongoni mwa misitu tulivu zaidi duniani.

Inasemekana kuwa bibi mmoja wa miaka 85 ameishi huko peke yake tangu mwaka 1987 bila historia ya kuumwa ugonjwa wowote tangu alipoamua kuishi katika msitu huo.

Related Posts