Unajua sababu kutokea dimpozi shavuni, kiunoni?

Dar es Salaam. Dimpozi la kwenye shavu ni maarufu kwa kuleta tabasamu la kipekee na mvuto wa aina yake, dimpozi la kiunoni maarufu kama ‘dimples of venus’ ambazo wakati mwingine, huchukuliwa kama ishara ya uwiano sahihi kati ya umri na uzito wa mwili wa muhusika.

Kwa mujibu wa utafiti wa American Journal of Physical Anthropology wa mwaka 2013 ulijikita katika uchunguzi wa mifumo ya anatomi ya misuli, mabadiliko ya tishu za mwili na tishu ya ngozi ya misuli ya uso.

Wakati wa uchunguzi huo, Journal of Physical Anthropology ulibaini kuwa, mifumo ya anatomi ya misuli huvuta ngozi maeneo ya kwenye shavu na kisha husababisha mbonyeo, ambao huitwa (dimpoz) na kuwa, alama hizo hutokea baada ya misuli ya shavu kuvuta ngozi wakati wa tabasamu.

Kadhalika, uchunguzi kuhusu mabadiliko ya tishu za mwili ulibaini kuwa, dimpozi huonekana baada ya mabadiliko ya kawaida ya tishu za ngozi ya misuli kwenye mashavu, na wakati misuli na ngozi zinavutana na kusukumana sehemu fulani ya ngozi hutengeneza dimpozi.

Utafiti huo ulionyesha kuwa, uwepo wa dimpozi ni maendeleo ya kawaida ya tishu za ngozi na misuli na mifumo ya kibaolojia ya uso.

Pia, wataalamu walienda mbali zaidi na kuchunguza kama uwepo wa dimpozi hutokana na sababu za kijenetiki au urithi, na wataalamu walibaini kuwa dimpozi ni tatizo la kurithiwa kutoka  wazazi au ukoo.

Utafiti mwingine uliofanywa na wataalamu wa jeni kutoka Chuo Kikuu cha Oxford mwaka 2010, ulibaini kuwa dimpozi ni mojawapo ya alama zinazohusiana na sifa za urithi zinazoshikiliwa na vinasaba.

Utafiti huu pia ulionyesha kuwa sifa za dimpozi zinaweza kutokea kwa mtu mmoja kati ya wazazi, lakini pia inaweza kutokea kwa mchanganyiko kutoka kwa wazazi wote wawili au mmoja.

Kwa mujibu wa tafiti za wataalamu wa afya dimpozi za kiuno, zinahusishwa na maumbile ya watu wenye asili ya miili membamba na hutumika kuonyesha uwiano sawa baina ya umri na uzito wa mwili na kuwa uwepo wa dimpozi ni kati ya ishara ya afya bora.

 Sambamba na hilo, uwepo wake unahusishwa na usawa wa homoni katika mwili, na wataalamu wanaamini kuwa dimpozi za kiuno hutokea kwa watu wasio na matatizo ya homoni pekee.

Kama ilivyo, kwa dimpozi za mashavu, tafiti nyingi zinabaini kwamba uwepo wake hutokana na kurithi kupitia vina saba.

Aidha, mtaalamu wa afya Dk Paul Masua anasema dimpozi ni moja ya ishara ya udhaifu kwenye misuli ya shavu.

“Kwenye ngozi kuna tabaka lenye udhaifu, na huvuta ngozi ndani na kusababisha hicho tunachokiita dimpozi,” anaeleza.

Anasema udhaifu huo hutokana na urithi kutoka kwa baba au ukoo wa upande wa baba pekee.

“Kuhusu dimpozi za kwenye kiuno mara nyingi inaonyesha kuwa hauna mafuta mengi mwilini na zinapotoweka maana yake umekuwa na mafuta yaliyoziba sehemu hiyo,” anaeleza Dk Masua.

Kadhalika Dk Mugisha Clement anasema uwepo wa dimpozi si ugonjwa wala tatizo ambalo lina madhara kwa afya ya mtu.

“Dimpozi hazina madhara na ni urembo kama ilivyo urembo mwingine usio na madhara,” anaeleza.

Related Posts