Hamas yawaachia mateka sita wa Israel, Wapalestina 603 nao kuachiwa

Gaza. Kundi la Hamas limewaachilia huru mateka sita kutoka Gaza na kuwakabidhi mateka hao wakiwa hai kwa Serikali ya Israel ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano ya kusitishwa kwa mapigano kati ya pande hizo.

Katika kulipa hilo, lsrael nayo inatarajiwa kuwaachilia takriban wafungwa wa Kipalestina 603 wa Kipalestina wanaoshikiliwa kwenye magereza mbalimbali wakitumikia vifungo mbalimbali.

Makubaliano ya kusitishwa mapigano kati ya pande hizo yalifikiwa Januari 19, 2025, ambapo hadi sasa mateka zaidi ya 20 wa Israel waliokuwa wanaoshikiliwa eneo la Gaza na Hamas wameachiwa guru huku wapalestina zaidi ya 1,100 nao wakiachiwa huru.

Mateka wawili wa kwanza kuachiliwa, ni Tal Shoham (40) na Avera Mengistu (38) ambapo wamekabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu katika mji Rafah uliopo Kusini mwa Gaza nchini Palestina.

Shoham alitekwa kutoka Kibbutz Be’eri, pamoja na watoto wake wawili, mkewe, na mama mkwe wake, ambao wote waliachiwa Novemba 2023.

Kwa upande wake, Mengistu, Mwisraeli kutoka Ashkelon, alivuka kuingia Gaza mwaka 2014.

Baadaye, maelfu ya watu, wakiwemo wapiganaji wa Hamas, walikusanyika katika eneo tofauti huko Nuseirat, katikati mwa Gaza, ambako mateka watatu Eliya Cohen (27) Omer Shem Tov (22), na Omer Wenkert (23) walikabidhiwa kwa maofisa hao.

Wakati wa hafla hiyo, watoto kadhaa walionekana jukwaani wakiwa wamevaa fulana zenye picha za viongozi wa Hamas waliouawa.

Wanaume hao watatu walitekwa katika tamasha la muziki la Nova karibu na mpaka wa Gaza na Israel Oktoba 7, 2023.

Walionekana wembamba lakini katika hali isiyoshtua ikilinganishwa na baadhi ya mateka waliotangulia kuachiwa, ambao hali zao zilizua maswali nchini Israel.

Shem Tov alionekana akizungumza na baadhi ya wapiganaji wa Hamas jukwaani na akarusha huku akiwabusu umati uliokusanyika eneo hilo kwa kutumia mikono.

Mateka wa sita, Hisham al-Sayed, (37), Mwarabu mwenye asili ya Israel kutoka jamii ya Wabedui kusini mwa Israel ambaye alitembea kuingia Gaza mwaka 2015, naye ni miongoni mwa mateka waliokabidhiwa kwa maofisa wa Msalaba Mwekundu huko Gaza, kwa mujibu wa chanzo cha usalama cha Israel na chanzo cha Hamas.

Inaripotiwa kuwa Al-Sayed na Mengistu wote wana matatizo makubwa ya afya ya akili. Walitekwa na Hamas takriban muongo mmoja uliopita, huku wanne wengine wakichukuliwa wakati wa shambulio la Oktoba 7, 2023.

Jeshi la Israel (IDF) limesema mateka hao wamevuka kuingia Israel na watafanyiwa uchunguzi wa kiafya kabla ya kuungana tena na familia zao.

Ofisi ya Wafungwa wa Kipalestina ilisema Jumamosi kuwa imepokea orodha ya wafungwa na mahabusu wapatao 600 wanaotarajiwa kuachiliwa kama sehemu ya mabadilishano.

Kati yao, 50 walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha, 60 kifungo cha muda mrefu, huku 445 wakizuiliwa Gaza tangu Oktoba 7, 2023.

Mateka wanaoachiliwa Jumamosi ndio wa mwisho walio hai ambao Israel na Hamas walikubaliana kubadilishana wakati wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Qatar mwezi uliopita yaliyopelekea makubaliano ya usitishaji mapigano.

Rais wa Israel, Isaac Herzog alisema Jumamosi kuwa “Kukamilika kwa mpango wa mateka ni suala la kibinadamu, kimaadili, na kiyahudi.”

Aliongeza kuwa mateka waliokombolewa leo “wanarudi kutoka katika vilindi vya mateso ili kuanza safari ya uponyaji na urejeaji wakiwa na familia zao wapendwa, waliopigana kwa nguvu zao zote kwa ajili yao.”

Kabla ya kukabidhiwa kwa Msalaba Mwekundu huko Rafah, Shoham na Mengistu walionyeshwa jukwaani, wakiwa wamezungukwa na wanamgambo waliokuwa na silaha na waliovaa barakoa. Walikabidhiwa nyaraka na Shoham alilazimishwa kuhutubia umati.

Mabaki ya mateka mwingine, Shiri Bibas, yalifika Tel Aviv Ijumaa usiku, baada ya kelele kuibuka kuhusu Hamas kuachilia mwili usio sahihi.

Mabaki ya Bibas yalitarajiwa kuwa miongoni mwa yale ya mateka wanne waliorejeshwa na Hamas Alhamisi, pamoja na wanawe, Kfir na Ariel, na mateka mwingine, Oded Lifshitz.

Hata hivyo, ingawa vipimo vya uchunguzi wa maiti vilivyofanywa na mamlaka za Israel vilithibitisha kuwa mabaki hayo ni ya wavulana hao wawili na Lifshitz, mwili wa nne haukuwa wa Shiri Bibas wala haukufanana na wa mateka mwingine yeyote wa Kiyahudi, jambo lililozua hasira na shutuma.

Msafara uliobeba mabaki ya Bibas, ambao Hamas ilikuwa imekabidhi kwa Msalaba Mwekundu, uliwasili Tel Aviv Ijumaa usiku.

“Usiku wa jana, Shiri wetu aliletwa nyumbani. Baada ya mchakato wa utambuzi katika Taasisi ya Tiba ya Uchunguzi, tulipokea habari asubuhi ya leo ambayo tuliogopa: Shiri wetu aliuawa akiwa mateka,” ilisema taarifa kutoka kwa familia yake iliyotolewa na Jukwaa la Mateka na Familia Zilizopotea leo Jumamosi.

Baada ya kuachiliwa kwa mateka Jumamosi, Hamas na washirika wake wataendelea kuwashikilia mateka 63 wa Kiyahudi huko Gaza. Takriban 32 kati yao wanaaminika kuwa wamekufa, kwa mujibu wa serikali ya Israel mmoja wao, askari Hadar Goldin, amekuwa akishikiliwa tangu 2014.

Iwapo miili mingine minne ya mateka itatolewa wiki ijayo kama ilivyopangwa, mchakato wa makabidhiano kwa awamu ya kwanza ya mpango huo utakuwa umekamilika.

Israel na Hamas zinafanya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja ili kuongeza muda wa usitishaji mapigano. Mazungumzo hayo yalianza zaidi ya wiki mbili baadaye.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts