Dar es Salaam. Una tatizo la kunuka miguu? Kama jibu ni ndiyo si peke yako mwenye tatizo hilo takwimu zinaonesha asilimia 10 ya watu duniani wana changamoto hiyo.
Hata hivyo, wataalamu wanasema ni mara chache mno tatizo hili likahitaji matibabu ya kitabibu kwani linaweza kumalizwa kwa kudhibiti chanzo chake.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kroko Foot Care ya Afrika Kusini, Lynsey Hammond amesema mara nyingi tatizo hili husababishwa jasho na bakteria wanaosababisha harufu kali kwenye miguu.
Amesema hayo ni matokeo ya mtu kuvaa viatu kwa muda mrefu bila kuruhusu miguu kupata hewa au wakati mwingine kuvaa viatu vichafu.
“Si watu wote wanaweza kukutana na hili ila kuna wale ambao miguu yao ikifunikwa na viatu kwa muda mrefu inapata joto na inatoa jasho, hali hiyo ikiwa kwa muda mrefu itaanza kutengeneza harufu.
Sasa inawezekana joto na harufu inayotengenezwa ikawa kali, hapa ndipo utaona mtu ananuka miguu. Hali hii inaweza kuwa ya muda mfupi au tatizo la muda mrefu itategemea na namna mhusika alivyoamua kushughulika nalo.”
Hammond ametaja sababu nyingine zinazochangia miguu kutoa harufu ni uzito kupita kiasi, matumizi ya dawa, mabadiliko ya homoni au kutokwa na jasho kupita kiasi.
Nini ufanye kukabiliana na hali hii
Mtaalamu huyo ameeleza kuwa kitu muhimu anachopaswa kuzingatia mtu mwenye tatizo la kunuka miguu ni usafi wa miguu na viatu anavyovaa.
Amesema bakteria wanaohusika na harufu ya miguu hukua kwenye unyevu, hivyo ni bora kuweka miguu yako kuwa kavu kila inapowezekana.
“Hakikisha wakati wote miguu yako ni misafi na yenye ukavu, usiruhusu ikae na jasho kwa muda mrefu. Unapochagua viatu vyako, kumbuka kwamba vitambaa vya asili kama pamba na ngozi vinaruhusu hewa kupita.
“Jitengenezee utaratibu wa kuisafisha miguu yako kwa maji na sabuni, anza kwa kuiloweka kwenye maji kwa muda usiopungua dakika 20 kisha isuuze na kuikausha iwe mikavu. Kama unavaa viatu vya kufunika usiache kuvaa soksi na ikiwezekana uwe na nyingine za ziada ili uweze kubadilisha.
“Kama inawezekana usirudie viatu mara mbili ikiwa havijakauka, ukishajua una tatizo hili hakikisha unaporudi nyumbani viatu vyako unaviweka sehemu yenye hewa ili jasho likauke na kupunguza harufu mbaya,” ames