ADC yatofautiana na Chadema, yaja na ‘Kama Mbwai na Iwe Mbwai’

Mwanza. “Kama Mbwai na Iwe Mbwai”. Hii ndiyo kauli anayoitumia Mwenyekiti wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) Taifa, Shaban Itutu kuelezea msimamo wa chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

Itutu ametoa kauli hiyo baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuja na kaulimbiu yake ya ‘No Reform, No Election’ ikimaanisha kwamba hakutakuwa na uchaguzi kama hakuna mabadiliko, mwaka huu.

Akizungumza leo Jumamosi Februari 22, 2025, alipozindua tawi la ADC Kata ya Nyamanoro Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Itutu amesema chama hicho hakitosusia uchaguzi badala yake kitautunmia kudai hayo mabadiliko chini ya kaulimbiu: “Kama mbwai na iwe mbwai”.

“ADC tunaamini katika kuhitaji Katiba mpya, Tume huru ya uchaguzi na utawala bora wa sheria. Kwamba kwa sababu Serikali ya CCM imeshindwa kutuandalia Tume huru (kwa vitendo)…sasa tunaingia nao kwenye uchaguzi ‘Kama Mbwai na iwe Mbwai’ tutakutana nao mbele ya safari ili wananchi mkaamue,” amesema Itutu.

Itutu amesema anaamini kwa kuwa CCM imeshindwa kufanya ‘reforms’ (marekebisho ya mifumo ya uchaguzi), namna pekee ya kuyafanya ni kupitia kuushawishi umma kuipigia ADC kura kwa wingi kisha itafanya marekebisho hayo ikiwa madakani.

Mwenyekiti wa Chama cha ADC taifa, Shaban Itutu (kulia) akimkabidhi Hamida Estam (kushoto) kadi ya uanachama wa Chama hicho leo Jumamosi Februari 22,2025. Picha na Mgongo Kaitira

“Tunataka wananchi mkaamue kwa kukipigia chama cha ADC kura ili tuwaondoe CCM madarakani kwa sababu usipoingia kwenye uchaguzi hata haki ya kuingia madarakani hawezi kuipata. Kwa hiyo haki ya kwanza ni kuingia kwenye uchaguzi ili tuwashughulikie CCM,” amesema Itutu.

Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa, Hamduni Maliseli akizungumza na Mwananchi, amesema umma una makovu yaliyotokana na uchaguzi, hivyo vyama vya siasa vinapaswa kuyaponya kwanza kwa kuhamasisha ushiriki kikamilifu kuanzia kujiandikisha hadi kupiga kura.

“Mwamko wa wananchi kushiriki kwenye mchakato wa uchaguzi umepungua, ni wakati sasa vyama vya siasa vianze kuhamasisha umma kushiriki kwenye mchakato wote wa uchaguzi kikamilifu baada ya hapo washughulikie mapungufu mengine yaliyopo ikiwemo ya kisheria.

“Ni muhimu kufanya hivyo kwa sababu hata ukisema uwaambie watu kuwa unataka watu washiriki mapambano ya kupata marekebisho ya sheria za uchaguzi, kama watakuwa hawana mwamko ama imani ya kisiasa bado itakuwa kazi bure,” amesema Maliseli.

Kwa upande wake, Mkazi wa Nyamanoro na mwanachama wa chama hicho, Hamisa Estam amesema namna pekee ya kupambana na changamoto hizo ni kuongeza ushawishi kwa wapigakura wajitokeze kwa wingi ili uamuzi ufanyike kwenye ‘sanduku la kura.’

“Naona mwenyekiti wetu yuko sahihi kwa sababu tutajipanga kikamilifu na hatutaki figisu, tunachotaka haki itendeke. Nawashauri ambao wanataka kususia uchaguzi wasiogope, waingie kwenye uchaguzi kama haki ipo wataipata,” amesema Hamisa.

Johnson Moshi, mkazi wa Kiseke wilayani Ilemela mkoani humo amevitaka vyama vya siasa hususan ni upinzani nchini kutotafuta kichaka cha kujificha, badala yake vianze mapema kuhamasisha wapiga kura wao kujitokeza kwa wingi kuvipigia kura ili kuiondoa CCM madarakani.

Related Posts