Zanda amkosha Katwila Bigman FC

KIWANGO kizuri kinachoonyeshwa na mshambuliaji mpya wa Bigman FC, Said Zanda kimemwibua kocha mkuu wa timu hiyo, Zubery Katwila aliyekiri kuridhishwa sana na usajili wake, ambao umeleta manufaa makubwa ya moja kwa moja katika kikosi hicho.

Nyota huyo amejiunga na kikosi hicho chenye maskani yake Mkoa wa Lindi dirisha dogo la usajili wa Januari mwaka huu akitokea Songea United na hadi sasa amekuwa ni muhimili mkubwa katika eneo la ushambuliaji na kuamsha morali.

Akizungumza na Mwanaspoti, Katwila alisema siku zote usajili ni kamari kwa sababu unaweza ukasajili mchezaji mzuri ila akashindwa kuonyesha makali yake sehemu nyingine, ingawa anashukuru nyota huyo ameendeleza kile alichokuwa anakifanya.

“Natambua ubora wake ndiyo maana nilipendekeza kwa viongozi kumsajili nikiamini atakuwa ni mchezaji sahihi kwetu, watu wanapaswa kutambua nimewahi kumfundisha katika timu ya taifa ya vijana, hivyo najua zaidi uwezo mkubwa aliokuwa nao.”

Zanda aliyewahi kucheza timu mbalimbali ikiwemo Stand United ‘Chama la Wana’, amekuwa na kiwango bora tangu ajiunge na kikosi hicho dirisha dogo na hadi sasa amecheza michezo mitano tu ya Ligi ya Championship na kufunga mabao matatu.

Related Posts