MSHAMBULIAJI wa Mbuni, Naku James amesema moja ya malengo yake makubwa aliyojiwekea katika ligi hii ya Championship ni kuivunja rekodi ya mabao aliyoyafunga msimu uliopita, sambamba na kukipigania kikosi hicho kumaliza nafasi nne za juu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Naku alisema hadi sasa yupo katika njia sahihi ya kutimiza malengo hayo ya kuivunja rekodi yake ya mabao kutokana na michezo mingi iliyobaki na kazi kubwa ni kumaliza kwa timu hiyo ndani ya nne bora.
“Tofauti ya mabao ya msimu uliopita na huu unaona kabisa nina nafasi ya kuivunja, malengo tunayotaka ni kumaliza nafasi nne za juu ili tupate fursa ya kucheza hata michezo tu ya ‘Play-Off’, naamini kwa gepu la pointi lililopo inawezekana.”
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo Januari 15, 2024 akitokea Copco FC ya jijini Mwanza, ndiye kinara wa kikosi hicho hadi sasa baada ya kufunga mabao 10, akibakisha bao moja tu kuivunja rekodi aliyoiweka msimu uliopita alipofunga pia 10.
Timu hiyo ya Mbuni kutoka Arusha, imecheza michezo 20, ya Ligi ya Championship na kati yake imeshinda saba, sare mitano na kupoteza minane, huku safu ya ushambuliaji ikifunga mabao 25 na kuruhusu 25, ikiwa nafasi ya tisa na pointi 26.