Beki Namungo kadi nyekundu, refa aliyemlima kimakosa akaushiwa

BEKI wa kati wa Namungo, Derrick Mukombozi amefutiwa kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba uliopigwa Februari 19 kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na wenyeji kupoteza kwa mabao 3-0.

Mukombozi alipewa kadi hiyo nyekundu iliyozua utata na mwamuzi Japhet Smarti kutoka Katavi dakika ya 35 ya pambano hilo baada ya beki huyo wakati wa harakati za kumzuia mshambuliaji Lionel Ateba na kutafsiriwa amefanya madhambi ambayo hata hivyo hayakuonekana uwanjani hapo na hata katika matangazo ya Azam Televisheni

Kadi hiyo ilionekana kuwashtua wadau wengi kutokana na mikanda ya video kuonyesha hakukuwa na tukio lolote linaloweza kusababisha adhabu ya namna hiyo, huku ikielezwa kwamba mwamuzi alimlima kwa kumpiga Ateba, huku taarifa nyingine zikisema alimdhalilisha bila kufafanuliwa.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa leo na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi imetangaza kwamba kadi hiyo imeondolewa rasmi kwa kile ilichosema maelezo yaliyopo katika ripoti ya mwamuzi hayakuwa na ushahidi wa kutosha unaoonendana na marejeo ya picha mjongeo.

Wakati kamati hiyo ikiifuta kadi hiyo, hakuna hatua zozote zilizoainisha katika taarifa hiyo zilizochukuliwa kwa Smarti aliyetoa kadi hiyo ya utata kwa Mukombozi na kuiponza Namungo kucheza pungufu kwa dakika 55 zilizosalia na kuruhusu kipigo hicho cha mabao 3-0 ikiwa nyumbani.

Kwa upande mwingine beki wa Namungo Daniel Amoah ametozwa faini ya sh 500000 kwa kosa la kuonekana akimwaga vimiminika kwenye goli jambo linalohusishwa na vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina tukio ambalo lilitokea kwenye mchezo huo dhidi ya Simba ambao wekundu hao walishinda kwa mabao 3-0.

Katika mchezo huo Simba uilipata mabao yake kupitia penalti mbili kati ya tatu zilizopigwa kupitia Jean Charles Ahoua, huku ile ya Leonel Ateba ikidakwa na kipa Jonathan Nahimana na dakika za lala salala, mtokea benchi, Steven Mukwala alifunga bao la tatu.

Related Posts