Morogoro. Mahakama ya hakimu mkazi Morogoro imemhukumu Mohamed Salange (37) kwenda jela miaka 30 kwa kosa la kumbaka mtoto wake wa kike wa kufikia mwenye umri wa miaka 12. Kosa hilo alilitenda kati ya Januari 2023 na Januari 2024.
Mei 3, mwaka huu, Salange alihukumiwa kifungo kingine cha miaka 30 jela baada ya kukutwa na kosa la ukatili dhidi ya mtoto wake wa kufikia mwenye miaka tisa.
Katika kesi hiyo, alidaiwa kwa nyakati tofauti, alimfanyia ukatili mtoto huyo kwa kumng’oa meno, kumchoma moto sehemu ya juu ya mdomo na kwenye makalio, kumpiga na kumvunjavunja mkono na kuvunja korodani kisha kumtoboa sehemu ya ngozi ya uume wake.
Leo Alhamisi Mei 16, 2024 katika hukumu iliyotolewa na Hakimu mkazi Mwandamizi, Renatus Barabara amesema Mahakama imeridhishwa na ushahidi ambao haukuacha mashaka, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo la ubakaji dhidi ya mwanawe huyo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti kati ya kipindi cha Januari 2023 na Januari 2024 katika kijiji cha Kimamba A, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.
Kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka, kitendo hicho kilimsababishia maumivu makali na hata mtoto alipomwambia baba yake huyo kuwa anasikia maumivu alimwambia atulie maumivu yataisha akizoea.
“Baada ya kupitia ushahidi wote na vielelezo vilivyoletwa, mahakama hii imejiridhisha pasipo kuacha mashaka yoyote kwamba upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa,” amesema Hakimu Barabara na kuongeza:
“Mshtakiwa amesema kesi iliyofunguliwa dhidi yake sio ya kweli maana katika kipindi chote tajwa hakuwahi kushtakiwa katika kituo chochote cha polisi na hata kwenye kumbukumbu hakuna popote aliposhtakiwa kuwa alitenda kosa hilo.”
Hata hivyo, hakimu aliukataa utetezi wa mshitakiwa huyo na kueleza kuwa mahakama imemtia hatiani kwani katika sheria ya makosa ya kujamiiana, Ushahidi mzuri na usiotiliwa shaka ni wa mtoto kama umepokelewa kisheria.
Kumbe ana mvua nyingine 30
Kabla ya Hakimu kutamka adhabu, mwendesha mashitaka wa Serikali, Edna Alloyce akisaidiana na mwenzake, Jackline, aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa ana kumbukumbu ya nyuma ya makosa ya jinai hivyo mahakama izingatie hilo.
Wamesema tayari mahakama hiyo hiyo imemhukumu kwenda jela miaka 30 kwa kumfanyia ukatili mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa hivyo inaonyesha kuwa mtuhumiwa ni mtu hatari na hafai katika jamii.
Pia Mwendesha mashtaka huyo aliiomba mahakama hiyo impe adhabu kali mshtakiwa huyo kwani kitendo alichokifanya ni unyanyasaji wa kijinsia, maana ukiangalia binti aliyembaka ni mdogo na alikuwa baba mlezi na ndiye alitakiwa kumlinda na ukatili wa kingono lakini yeye ndiye kageuka kumnyanyasa
Akizidi kujenga hoja ya kutolewa adhabu kali, alisema mshtakiwa huyo amevunja haki ya mtoto kulindwa kwa kumbaka na pia amemharibu kisaikolojia kwa kumbaka kitu ambacho kitakuwa kigumu kufutika kwenye kumbukumbu zake.
“Mshtakiwa amemsababishia magonjwa ya zinaa jambo linaloweza kumharibia via vya uzazi na kumsababishia saratani hivyo tunaomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hizo,”alisisitiza.
Mshtakiwa alipopewa nafasi ya kuomba huruma ya mahakama, mshitakiwa aliieleza mahakama kuwa japo mahakama imemtia hatiani kwa kosa ambalo hajatenda, yeye ni mtu mzima na mwenye thamani na mwenye umri wa miaka 38 anaomba apunguziwe adhabu isiwe kubwa kama mlima Kilimanjaro.
Hata hivyo katika hukumu yake, Hakimu Barabara, amesema kwa kuzingatia uzito wa kosa na umri wa mwathirika, ni dhahiri yako madhara kiakili na kifikra ameyapata na kwa kuangalia umri wa mshtakiwa mahakama inatoa adhabu kali ya miaka 30.
Ushahidi dhidi yake ulivyokuwa
Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo mashahidi wa upande wa mashtaka akiwemo mtoto huyo mwathirika, wameieleza mahakama jinsi mshtakiwa alivyombaka binti huyo kiasi cha kumfanya apate maumivu makali.
Kutokana na maumivu hayo, yalimfanya mtoto wake huyo wa kufikia na kubadili muondoko ambapo waliieleza mahakama jinsi mshtakiwa huyo alivyoingiza uume kwenye uke wa Mwathirika huyo na kumsababishia magonjwa ya zinaa.
Mtoto huyo mwathirika ambaye jina lake linahifadhiwa, alikuwa shahidi wa kwanza, aliieleza mahakama hiyo kuwa kati ya Januari 2023, na Januari 2024 walikuwa wakiishi na mama yao ambaye alimpiga mpaka kupoteza Maisha.
Alieleza pia kuwa alimbaka mama yake alipokwenda mtoni na wakati mwingine alimbaka mama yake akiwa amelala ndani na kufunga mlango kwa nje na baada ya hapo alimtisha kwa kumwambia kuwa kama atasema popote atamuua.
Na kabla mama yake hajafa aliwahi kumshtakia kuhusu tukio hilo lakini mama yake hakuamini na alimwambia kuwa anataka kuleta ugomvi kwenye familia.
Pia alieleza kuwa baba yake huyo wa kufikia hata alipomwambia kuwa waalimu shule waliwakataza watoto kufanya mapenzi kwenye umri mdogo, mshtakiwa huyo alimtaka kupuuza taarifa hizo na kuendelea kumfanyia kitendo hicho.
Vitendo hivyo vimemuathiri kwa kutotembea vizuri na alipona vidonda baada ya kuhama kutoka Kimamba A, kwenda Ludewa walikoishi na mama yao wa kambo.
Kwa mujibu wa ushahidi huo, wakati mshtakiwa akimbaka mtoto huyo, mama yake alikuwepo lakini hakumuamini jambo lililomfanya akae kimya bila kusema maana mama yake aliyemzaa kama hakuamini basi hata wengine wasingeamini.
Shahidi wa pili ambaye ni kaka mdogo wa mshtakiwa mwenye umri wa miaka tisa, alisema baba yao alikuwa akifanya mapenzi na dada yake kama mara mbili na kuna wakati alimsikia dada yake akilia akisema “Baba unaniumiza “ na wakati huo mama akiwa amefungiwa ndani wakati huo yeye aliambiwa akaangalie kuku.
Shahidi wa tatu ambaye ni daktari wa hospitali ya wilaya ya kilosa, alisema alipomchunguza mtoto mwathirika mwenye umri wa miaka 12, aliona maji meupe yanatoka na hakuwa bikra kwani vidole vitatu vilipita.
Alieleza kuwa kwa mtoto wa umri wa miaka 12 sio kawaida vidole vitatu kuingia kwa maana hiyo inaonyesha aliingiliwa na kitu baada ya kuchukua sampuli za maji yale maupe aligundulika kuwa ameambukizwa ugonjwa wa zinaa.
Alimpa dozi ya siku 10 ambapo ugonjwa huo unaweza kusababisha ugumba na anaweza kupata ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Hii ni moja ya kesi nne zilizokuwa zinamkabili Salange, zikiwemo kesi nyingine ya ukatili kwa mtoto wake wa kiume ambayo ameshahukumiwa miaka 30 jela, kesi ya ukatili kwa mtoto wake wa kike wa kufikia na kesi ya tuhuma ya mauaji ya mkewe.
Katika kesi hiyo ya mauaji ambayo anadaiwa kuwa alimuua mkewe kisha kumzika ndani ya nyumba ambayo bado inaendelea mahakamani hapo katika hatua ya uchunguzi.