Watanzania wapania mzunguko wa pili Uturuki

WATANZANIA wawili wanaokipiga Ligi Kuu ya Walemavu nchini Uturuki, Ramadhan Chomelo anayekipiga Konya Amputee na  Hebron Shedrack wa Sisli Yeditepe wamesema licha ya kuanza mzunguko wa kwanza vibaya, watahakikisha wa pili wanafanya vizuri.

Nyota hao ndio pekee kutoka Tanzania wanaocheza soka la ulemavu kwa msimu wa tatu sasa tangu waliposajiliwa mwaka 2022.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chomelo alisema hawajaanza vyema mzunguko wa kwanza na sababu ni pamoja na kukosa maandalizi mazuri ya ligi.

“Tupo nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi, siyo nafasi nzuri, ngoja tuone mzunguko wa pili utakuwaje lakini tunaamini siku kadhaa za mapumziko zitakuwa na manufaa kwetu kwenye maandalizi,” alisema Chomelo.

Kwa upande wa Shedrack alikiri ugumu wa ligi hiyo na wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha mzunguko wa pili wanamaliza nafasi nzuri kwenye msimamo.

“Timu yetu haiko sawa, nikiwa kama mchezaji tegemeo kwenye kikosi chetu, ninapopata majeraha inakuwa changamoto kwa hiyo ninajitahidi sana nisiumie ili niinusuru timu, lakini tuko kwenye hali mbaya,” alisema Shedrack ambaye ana mabao matano na asisti tisa.

Related Posts