Wananchi Mtama wataka wataja mambo matatu kampeni ya kisheria wa Mama Samia

Mtama. Wananchi wa Kijiji cha Utimbula, Kata ya Namangale, Halmashauri ya Mtama wameiomba Serikali kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Legal Aid Campaign) kuwasaidia katika upatikanaji wa zahanati, shule pamoja na barabara.

Akizungumza leo, Jumapili Februari 23, 2025, kwenye kikao cha Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, mkazi wa Utimbula, Hija Athumani, ameiomba Serikali kuhakikisha wanapatiwa huduma za jamii kwa kuwajengea zahanati, shule na kuwatengenezea barabara.

Athumani amesema kuwa wanafunzi na wanawake wamekuwa wakitembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10 kwenda kupata huduma ya afya katika kata ya Namangale, huku kukiwa na miundombinu ya barabara isiyo rafiki.

“Sisi tulishajitolea kujenga chumba kimoja cha darasa, baadaye Serikali ikatusaidia vyumba viwili, lakini hadi sasa shule hiyo ya Utimbula bado haijasajiliwa na wanafunzi wanasoma hivyo hivyo tangu mwaka 2003,” amesema Athumani.

Ameongeza kuwa wanafunzi wa darasa la nne na kuendelea wanalazimika kwenda kusoma Shule ya Msingi Namangale, wakitembea umbali wa zaidi ya kilomita 10, huku walimu waliopo shuleni hapo wakiwa ni watatu pekee, wawili kati yao wakijitolea. Wananchi wamekuwa wakichangishana fedha ili kuwalipa posho kila mwezi.

“Wanafunzi hao wanakwenda umbali mrefu wa zaidi ya kilomita 10, na pia njia ni mbaya, inahatarisha maisha yao, hasa mvua inaponyesha kwani barabara huwa haipitiki kabisa. Pia tumechangishana kama kijiji na kupata kiwanja kwa ajili ya zahanati. Sisi tupo tayari kutoa nguvu zetu kwa kuanza na msingi, baadaye Serikali iweze kutusaidia,” amesema Athumani.

Zainabu Kambona, mkazi wa Utimbula, amesema kuwa wanawake na watoto wamekuwa wakiteseka kutokana na kukosa huduma za afya, hivyo akaomba timu ya msaada wa kisheria kusaidia upatikanaji wa huduma hiyo.

“Tunawaomba timu ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kutusaidia kupata zahanati, shule pamoja na kutengenezewa barabara. Tumekuwa kama hatupo Tanzania kwa sababu hatuna huduma yoyote ya msingi,” alisema Kambona.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Utimbula, Martin Kagembe, amesema kuwa kijiji chake kina wakazi zaidi ya 700, lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa zahanati, shule na miundombinu ya barabara.

“Tunaiomba Serikali kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kutusaidia kupata huduma hizo ambazo kwetu hakuna. Tunateseka sana kwa kukosa huduma za kijamii,” amesema Kagembe.

Hata hivyo, Mratibu wa Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Antony Kabazi, amesema tayari changamoto hiyo imechukuliwa na imepelekwa sehemu husika ili ipatiwe ufumbuzi.

“Changamoto yao tumeichukua na tayari tumeipeleka sehemu husika ili ipatiwe ufumbuzi mapema,” amesema Kabazi.

Related Posts