KIUNGO mshambuliaji wa San Jose Earthquakes ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), Amahl Pellegrino mwenye uraia wa Norway na asili ya Tanzania, ameanza kujinadi akionyesha anatamani kuichezea timu ya Taifa Taifa Stars.
Nyota huyo ambaye aliwahi kuitwa kwenye kikosi cha awali cha Stars na Kocha Adel Amrouche ingawa hakucheza mechi hata moja, ameoinyesha ana nia ya kuitumikia timu hiyo baada ya kuposti katika ukurasa wake wa mtandao wa Instagram akiwa na bendera ya Tanzania huku akiambatanisha na maneno ‘maandalizi ya msimu mpya’.
Pellegrino aliyezaliwa mwaka 1990 ni msimu wake wa pili kuitumikia timu hiyo na alitua mwaka 2024 akitokea Bodø/Glimt ya Norway na alifunga mabao saba kwenye mechi 32 za mashindano yote.
Kiungo huyo mshambuliaji alizaliwa Jiji la Drammen, Norway na wazazi wake ni Watanzania halisi ingawa hakukulia Tanzania hivyo anasomeka na uraia wa nchi mbili, ingawa ana uwezo wa kucheza timu yoyote ya mataifa hayo na aliwahi kuitwa Stars mwaka 2023.
Maisha ya soka la kulipwa kwa Pellegrino yalianza akiwa na Drammen alikocheza kwa misimu miwili mwaka 2009/11, msimu uliofuata akajiunga na Baerum ya nchini humo akifunga mabao 33 kwenye mechi 68.
2014/15 akatimkia Lillestrøm akacheza mechi bila kufunga bao lolote, 2015/17 akajiunga na Mjøndalen akacheza mechi 70 (28), 2018/19 Strømsgodset alifunga mabao manne kwenye michezo 39
Msimu uliofuata akaitumikia Kristiansund kwenye mechi 39 akafunga (33) zote za nchini kwao Norway, msimu 2021 aliitumikia Damac Ligi Kuu Saudia kwenye mechi 12 alifunga mabao mawili.
Msimu ulifuata akarejea Morway na kujiunga na Bodø/Glimt aliyocheza mechi 71 (55) na sasa San Jose alipocheza kwa msimu wa pili mfululizo.