IITMZ kuongeza ujuzi wa teknolojia taasisi za Serikali, binafsi

Unguja. Ili kuongeza ujuzi na kuleta ufanisi kwa watendaji wa Serikali, Taasisi ya Teknolojia ya India Madras Kampasi ya Zanzibar (IITMZ) imesema itaendelea kushirikiana na wadau hao kuwapa mbinu na mafunzo kuhusu teknolojia za kisasa.

Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Kampasi ya Zanzibar,  Profesa Aghalayam ameeleza hayo jana Februari 22, 2025 katika mafunzo ya teknolojia ya ujenzi inayolenga maendeleo katika kuchanganya zege katika sekta hiyo.

Amesema pamoja na programu za muda mrefu zinazotolewa na taasisi hiyo, wameanzisha programu fupi kuimarisha utendaji wa watendaji serikalini na binafsi.

“Kwa zaidi ya miaka miwili tumekuwa tukitoa mafunzo ya muda mrefu lakini baada ya kuona kuna uhitaji, tumeanzisha mafunzo ya muda mfupi katika kuwapa mbinu za kisasa, ” amesema.

Akizungumzia udahili, amesema wanatarajia kupokea wanafunzi wa sayansi katika nyanja za takwimu na akili mnemba akiwataka vijana wenye sifa kutumia fursa hiyo inayotokana na uhusiano mwema baina ya India na Tanzania.

Naye Mrajisi wa taasisi hiyo, Mshauri Abdulla Khamis amesema mafunzo hayo kwa watendaji wa sekta ya ujenzi yataongeza ufanisi katika kazi zao.

Kuhusu utolewaji wa elimu ya teknolojia amesema, kadri wanavyojitokeza vijana wengi kupata taaluma hiyo ndivyo wanavyopatikana wataalamu wengi katika sekta hizo na kuifanya nchi iwe na wataalamu wengi zaidi.

“Kwa vijana wa Zanzibar wanaosomea haya masomo wanatakiwa kuikimbilia hii fursa kwani kuna ahueni kubwa maana Serikali inatoa ruzuku ya ada ya robo tatu na robo inayobaki inatolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Msiya Kessy kutoka Kampuni ya Sika Tanzania, amesema wameongeza maarifa mapya na wataimarisha utendaji kazi.

Mhandisi kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe, Massoud Suleiman Ali amesema wamepata maarifa mapya hususani namna ya kuchanganya zege na matumizi ya saruji katika ujenzi kulingana na mabadiliko ya teknolojia.

Related Posts