AZAM FC iko mbioni kuachana na Kocha wa Fiziki na Mtaalamu wa tiba za Wanamichezo (physiotherapist), Mreno Joao Rodrigues baada ya msimu huu kuisha huku ikielezwa sababu kubwa ni majeraha ya wachezaji yanayoiandama.
Taarifa kutoka ndani ya timu hiyo zinasema Joao hayupo kwenye mipango yao msimu ujao huku sababu ikielezwa wachezaji na viongozi kutokuwa na imani naye tena hasa baada ya wimbi kubwa la majeruhi yaliyotibua hesabu zao.
“Ni kweli Joao anaweza akaachwa kwa sababu viongozi wamekosa imani naye licha ya uzoefu mkubwa aliokuwa nao katika timu mbalimbali alizofanya kazi, kuna muda tulibaki na wachezaji 15 jambo ambalo halikuwa na afya kikosini,” kilisema chanzo chetu.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’ alipotafutwa kuzungumzia suala hilo alisema, jambo lolote ambalo linawahusu kama klabu wana utaratibu wao mzuri wa kulitolea taarifa kupitia vyanzo vyao mbalimbali ikiwa kuna ulazima.
“Nsingependa kulizungumzia hilo kwa sasa kwa sababu ni tetesi kama zilivyokuwa nyingine, mashabiki zetu watapata ukweli wowote pale na tutakamilisha kila kitu.”
Wakati ‘Popat’ akizungumza hayo ila Mwanaspoti linatambua kocha mkuu wa timu hiyo, Youssouph Dabo alichukukizwa kwa kiasi kikubwa na huduma aliyokuwa anaitoa Mreno huyo kwani ilimsababishia kutibua mipango yake ya kuwania ubingwa.
“Wakati tunacheza na Yanga Machi 17, mwaka huu kikosi kilikuwa na wachezaji 15 hadi 16 na ukiangalia hawakuwa wote ambao ni kikosi cha kwanza hivyo tulikuwa na kipindi kigumu na nikiri wazi ilichangia kututoa kwenye mstari,” kilisema chanzo hicho.
Baadhi ya wachezaji wa kikosi cha kwanza waliopata majeraha ya muda mrefu ni, Ali Ahmada, Malickou Ndoye, Cheikh Sidibe, Sospeter Bajana, Alassane Diao, Abdullah Idrissu na Mcolombia, Franklin Navarro aliyeumia tangu Februari mwaka huu.
Wengine ni Abdallah Heri ‘Sebo’ aliyeumia tangu Septemba mwaka jana, Daniel Amoah na Yannick Bangala waliorejea hivi karibuni. Joao ni mtaalamu wa viwango vya juu kwenye tiba za wachezaji, aliyetua Agosti 20, 2022 huku akiwahi kufanya kazi na Ureno, FC Porto.