NYOTA wa kimataifa wa Riadha nchini, Gabriel Geay amefunika baada ya kuibuka mshindi wa kwanza wa mbio za Daegu Marathon 2025 zilizofanyika leo Jumapili huko Korea Kusini.
Geay ambaye ni mshindi wa pili wa Boston Marathon 2023, katika mbio hizo za leo alimshinda Shujaa wa Ethiopia aliyeng’ara Dubai Marathon 2024, Addisu Gobena kwa kutumia muda wa saa 2:05:20.
Addisu alimaliza wa pili akitumia muda wa 2:05:22 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mhabeshi mwingine, Dejene Magersa aliyetumia muda wa 2:05:59.
Kwa upande wa Wanawake, Meseret Balete wa Ethiopia alimaliza wa kwanza kwa muda wa 2:24:08 huku mshindi wa medali ya dhahabu ya Olimpiki ya Rio De Janeiro 2016 Ruth Jebet wa Bahrain akimaliza nyuma kwa zaidi ya dakika moja na nusu 2:25:43.
Mbio hizo pia zilishuudiwa Tigist Girma wa Ethiopia akimaliza nyuma ya Ruth kwa zaidi ya dakika moja akimaliza wa tatu kwa 2:26:45.
Tofauti na mbio nyingine katika mbioz hizo za Korea Kusini, wanariadha wa Kenya wakigaragazwa vibaya ambapo kwa upande wa Wanaume Gilbert Kibet alimaliza wa sita kwa muda wa 2:06:39 na kufuatiwa na mwenzake Stephen Kiprop ambaye alimaliza wa saba kwa kutumia 2:07:16.
Kwa upande wa wanariadha wa kike wa Kenya, Vivian Jerotich alimaliza nafasi ya tano kwa Wanawake akitumia muda wa 2:29:54.
Akizungumza na Mwanaspoti, Geay aliyeshindwa kumaliza mbio za Michezo ya Olimpiki 2024 zilizofanyika Julai-Agosti mwaka jana, amesema haikuwa rahisi kwake kushinda kutokana na ushindi ambao ulikuwepo baina ya wakimbiaji wenzake ila alitumia madhaifu yao kuwashinda.
“Ushindani ulikuwa mgumu sana ila nawashukuru wote ambao wameiombea lakini pia uongozi wangu juhudi zao ndio imefanikisha ushindi huu,” amesema Geay.
Mbio za Daegu Marathon zinakuwa mashindano ya pili mwaka huu kwa Geay kushiriki baada ya kukutana na changamoto za kiafya mwaka 2024, ikiwamo kuchemsha katika Olimpiki 2024.
Mbio za kwanza kwake kushiriki mwaka huu zilikuwa ni za Aramco Huston Half Marathon ambazo zilifanyika Marekani n kufanikiwa kumaliza wa tatu kwa dakika 59:18.