NYOTA wa Stand United ‘Chama la Wana’, Adam Uledi amesema hajutii kitendo cha kutoka kuichezea Ligi Kuu Bara na kuhamia Championship na kwake kambi ni kokote katika kujitafuta upya ili kuendeleza kiwango chake.
Mshambuliaji huyo alijiunga na timu hiyo ya mkoani Shinyanga baada ya kuachana na KenGold ya jijini Mbeya na hadi anaondoka alikuwa amechangia bao moja, katika sare ya kikosi hicho ya mabao 2-2, dhidi ya Dodoma Jiji Oktoba 29, 2024.
Akizungumza na Mwanaspoti, Uledi alisema anajisikia furaha sehemu aliyopo kwa sasa na anashukuru kwa alichokifanya akiwa na KenGold, ingawa malengo aliyojiwekea yalienda tofauti na vile alivyokuwa anatarajia.
“Nilikuwa na malengo ya kufanya vizuri zaidi tofauti na kiwango nilichokionyesha kwa miezi sita, binafsi naamini ulikuwa ni upepo mbaya tuliokutana nao, lakini kwa sasa nimefungua ukurasa mpya wa kujitafuta upya ili kuendeleza ubora wangu.”
Uledi aliyeichezea timu ya vijana ya Yanga huku akizitumikia pia, Namungo FC, Ruvu Shooting, African Sports na Coastal Union, ameonyesha kiwango kizuri tangu ajiunge na Stand United na hadi sasa amefunga mabao mawili.