“Mimi bado ni Chadema, nitagombea ubunge katika jimbo la Rungwe kwa mara nyingine kwa tiketi ya Chadema,” ni kauli ya kujiamini ya mbunge wa viti maalumu, Sophia Mwakagenda, mmoja wa wabunge 19 waliotimuliwa ndani ya Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema).
Itakumbukwa kuwa wabunge haoa 19 wa viti maalumu kupitia Chadema wamekuwa na mgogoro na chama chao kwa takribani miaka mitano sasa tangu walipoapishwa bungeni baada ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Mbali na Mwakagenda, wengine ni Halima Mdee, Esther Matiko, Grace Tendega, Cecilia Pareso, Ester Bulaya, Agnes Lambart, Nusrat Hanje na Jesca Kishoa.
Pia, yumo Hawa Mwaifunga, Tunza Malapo, Asia Mohammed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.
Uongozi wa Chadema, ambao kwa mujibu wa sheria ulitakiwa kuwasilisha orodha ya wabunge wake wa viti maalumu kwa Tume ya Uchaguzi kisha kupelekwa kwa Spika wa Bunge, kimedai kwamba hakikupeleka orodha hiyo kwa sababu kilikuwa kinapinga uchaguzi huo.
Kutokana na wanachama hao kutotii msimamo wa chama chao, Chadema iliwafuta uanachama na wao wakaenda mahakamani kufungua kesi ya kupinga uamuzi wa Baraza Kuu la chama hicho la kuwafuta uanachama.
Hata hivyo, wabunge hao walikimbilia mahakamani na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilitoa hukumu iliyowapa uhalali wa kuendelea kuwa wanachama na kubaki na ubunge wao utakaofikia tamati baadaye mwaka huu baada ya Bunge kuvunjwa ili kwenda kwenye uchaguzi mkuu.
Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Sophia Mwakagenda, mmoja wa wabunge hao waliotimuliwa uanachama na anazungumzia mambo mbalimbali ikiwemo hatma yake kisiasa baada ya Bunge kuvunjwa ifikapo Juni 30, 2025.
Katika mahojiano hayo, Mwakagenda anasema hajaondoka Chadema, yupo bungeni kama mbunge wa Chadema na atagombea Jimbo la Rungwe lililopo mkoani Mbeya kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu, kupitia tiketi ya chama hicho cha upinzani.
Anasema katika uchaguzi wa mwaka 2020 alipojitosa kugombea katika jimbo hilo, aliacha mtaji mkubwa wa watu, alikubalika kwa kura 37,000 alizopata wakati ule, ambazo anasema ni mtaji kwake kwenye uchaguzi wa mwaka huu.
“Nilipokwenda kugombea Rungwe, watu waliniuliza utaweza? Tena mwanamke! Nikasema naweza kwa kuwa tayari nilishapata uzoefu mwaka 2015 nilipokuwa viti maalumu. Nilichuana na wanaume saba kwenye kura za maoni, nikaiwakilisha Chadema kwenye uchaguzi mkuu na kupata kura 37,000 ambazo kwangu ni mtaji,” anasema.
Mbunge huyo wa viti maalumu, anayeuwakilisha mkoa wa Mbeya, anasema kilichotokea hadi wao kurudi bungeni mwaka 2020 kinafahamika na uongozi uliopita na uliopo sasa.
“Sisi tuliamua kukaa kimya, hatukuzungumza chochote na mpaka sasa nimelizungumza hili kwa kuiheshimu Mwananchi, lakini yote yaliyotokea yanajulikana kwenye uongozi. Nipo bungeni kama mwanachama wa Chadema, nitagombea jimbo la Rungwe uchaguzi ujao kupitia Chadema,” amesisitiza.
Akizungumzia hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa anasema Chadema sio mashetani kwamba hawasamehi wala sio malaika kwamba hawakosei.
“Ukweli unabaki pale pale, tulishamalizana nao, si wanachama wetu, walikikosea chama, hivyo wakitaka kurudi ni lazima wajibu maswali yetu, wakiwa na ujasiri huo, inabidi waje wajieleze, nini kilitokea, nani alisaini fomu zao kwenda bungeni, nani aliyegonga muhuri.
“Pia, inabidi wajibu hili swali kwamba hawaoni kama walikifedhehesha chama? Wakija tutawapeleka mbele ya vikao, huko ndipo itaamuliwa na ikitegemea na kukiri kwao na jinsi watakavyoomba msamaha, wanachama wakiona wasamehe basi hatutakuwa na shida,” anasema Golugwa.
Mwakagenda amekuwa karibu na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson jambo ambalo liliibua minong’ono kwamba huenda akatimkia upande wa pili.
Anasema kuwa upinzani si uadui, wanapokuwa bungeni ndipo wapinzani wanabishana kwa hoja, wakitoka bungeni si wapinzani bali ni sawa na ndugu, jamaa na marafiki.
“Hatujawahi kuchukiana kwa sababu ya upinzani, ukiona ugomvi hapo hakuna kiongozi, ukaribu wangu na Mheshimiwa Spika (Dk Tulia) ni wa kazi. Pia tumezaliwa wilaya moja, haihusiani na kuhamia CCM (Chama cha Mapinduzi),” anasema.
Jina la Covid 19 lilivyomuimarisha
Waliporudi bungeni na kuibua sintofahamu, wabunge hao 19 wa Chadema akiwamo Mwakagenda walipachikwa jina la utani la Covid-19, wakifananishwa na kirusi cha ugonjwa wa mlipuko uliokuwa umeshika kasi wakati huo na kuua maelfu ya watu duniani.
“Tulilipenda hili jina kwa kuwa ni kirusi ambacho hakina dawa, tena mimi nilikuwa najitambulisha hivyo na kuanzisha kundi la Covid Squad,” anasema.
Anasema, kuitwa Covid-19 hakukumuathiri, walijiona ni wanawake mashujaa. “Mwisho wa yote, bado Chadema ilitutunza, ni chama chetu, tunakipenda na nini kilitokea tutazungumza itakapofika wakati,” anasema mbunge huyo.
Anavyotofautisha familia na siasa
Mwakagenda ambaye ni mke na mama wa watoto watano, anelezea namna familia yake inavyomsapoti katika kazi yake ya siasa.
Mume wake, Hebron Mwakagenda ni mwanaharakati wa muda mrefu ambaye anamtaja kama mwalimu wake ambaye anasema, anapenda mabadiliko.
“Inapotokea nimekosea, basi mume wangu ananionya kama baba na kichwa cha familia, tuko kwenye ndoa mwaka wa 35 na tumepata watoto watano, mkubwa akiwa na miaka 33.
Ili uwe mama lazima ujitambue, uhakikishe watoto wanakwenda shuleni, umhudumie mumeo, wakati huo jamii inakusubiri, vikoba na jumuiya pia, wakati unafanya yote ukumbuke familia kwanza,” anasema.
Anaendelea kusema: “Mfano, Mwakagenda anaweza kuamua tu kuja Rungwe na kusema msimchague huyu mwanamke (yeye), ana moja mbili tatu, hata kama watu hawatamuamini, wapo wachache watamwamini,” anasema mbunge huyo.
Anasema ubunge haumfanyi kutoka kuwa mke na mama kwa familia yake, anapofika nyumbani ubunge anauacha getini na kuwa mke na mama.
“Namsikiliza mume wangu, ndiyo maana nimeweza kufanikiwa, kwa sababu kuna watu wakiingia bungeni wanabadilika na familia kuiacha nyuma, hii si sawa,” anasema Mwakagenda.
Watoto walivyofuata nyayo
Mwakagenda ambaye alikutana na mumewe katika harakati za uongozi na siasa, anasema alianza uongozi akiwa shule kisha chuo ambako alikuwa kiongozi wa Serikali ya wanafunzi kwa nyakati tofauti.
‘Huko ndipo nilikutana na mume wangu, hivyo siasa ipo kwenye familia yetu, watoto wananisapoti, kuna binti yangu mmoja nilimuona anafanya siasa ngumu, nikasema hapana, ikabidi nimpeleke China kwanza asome ndipo aje afuate nyayo,” anasema Mwakagenda.
Anasema katika familia, watoto wakikuta wazazi wanafanya jambo fulani, wengi wao hupita njia hizo.
“Huyu niliyemhamishia China, siku Tundu Lissu (sasa mwenyekiti wa Chadema) alipopigwa risasi, aliniuliza, mama umeumia? Akasema usiogope. Kesho yake, kwenye begi lake la shule, wakati huo alikuwa anasoma Jangwani Sekondari, akaandika ‘Lissu 2020’.
“Mkuu wa shule akasema kwa nini amefanya hivyo, akasema kama kuna mabegi ya Spider, yeye amependa kumuweka Lissu, ni mtu ambaye namuona anafuata nyayo lakini anafanya siasa ngumu.
“Nilimpeleka China, kule kidogo wana misimamo ili akajifunze, asome, akimaliza ndipo afanye siasa akitaka. Ni watoto tunahitaji kuwa-menta,” amesema Mwakagenda.
Anasema binti yake mwingine alifuata nyayo za kupenda kusaidia wahitaji. “Sisi tuna vituo vitano vya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu, vinne tunavisapoti gharama mbalimbali, na kimoja nakihudumia moja kwa moja.”
Anasema binti yake mwingine, ambaye sasa ni daktari, alipokuwa sekondari alipenda kusaidia kwa kuwashirikisha wanafunzi wenzake na kukusanya nguo kwa ajili ya watoto.
“Ndiyo maisha aliyokulia, hivyo akafuata nyayo hizo. Watoto wangu wa kiume nao huwa wanasapoti na kushauri,” anasema.
Anasema katika kituo kimoja, alipata msaada wa vyerehani 50 na kutengeneza eneo ambalo mabinti wana fursa ya kujifunza ushonaji.
“Nilianza kuhudumia vituo hivi tangu 2008. Mwaka 2015, kwenye ubunge wangu wa viti maalumu, nilisomesha mabinti 500. Katika ubunge huu wa Covid-19, nimewasomesha mabinti 630,” anasema.
Awazungumzia Mbowe, Lissu
Wiki kadhaa zilizopita, wanachama wa Chadema walimchagua Lissu kuwa mwenyekiti wao, akimshinda Freeman Mbowe aliyekuwa akitetea kiti chake. Uchaguzi huo ni kama uliwagawa Chadema, ingawa baada ya uchaguzi walikiri kuwa na kibarua cha kuponya makovu.
Akiwazungumzia viongozi hao, Mwakagenda anasema Mbowe ni kiongozi mzoefu wa Chadema, na katika uongozi wake amekitendea haki chama hicho.
“Amefanya kazi yake, tunampongeza Lissu aendeleze pale alipoishia mtangulizi wake,” amesema.