Waziri Jr amtaja Simon Msuva dili la Iraq

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Dodoma Jiji aliyetambulishwa hivi karibuni na klabu ya Al Mina’a ya Iraq amesema Simon Msuva ana mchango mkubwa kutua katika timu hiyo.

Wazir Jr aliyewahi kukipiga Yanga 2020/21, alisaini mkataba wa miezi sita na timu hiyo iliyopo nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi hiyo yenye timu 20 akiwa pia ni nyota wa pili Mtanzania kucheza katika ligi hiyo baada ya Simon Msuva anayekipiga Al Talaba.

Akizungumza na Mwanaspoti, mshambuliaji huyo alisema nyota huyo wa Taifa Stars mwenye mabao 24 akiwa na uzi huo wa Taifa na aliyepita ligi za Morocco na Saudi Arabia ni mmoja wa watu waliochangia kutua Iraq na kutokana na jitihada zake, zinashawishi nyota wengi kutoka nje.

“Ni jambo zuri kuwa watanzania wawili kwenye ligi hii kwa sababu tunaitangaza nchi kimataifa na ni fursa kwa wengine, pia namshukuru sana Msuva kwa sababu ni mmoja wa waliochangia mimi kuwepo hapa, kufanya kwake vizuri ndiyo kumeshawishi wengine,” alisema Wazir.

DATA ZA WAZIR JR LIGI KUU

Alicheza misimu miwili Toto Africans 2015/16 na 2016/17 akifunga jumla ya mabao 14, akatua Azam FC msimu mmoja 2017/18 na kufunga bao moja, 2018/19 alijiunga na Biashara United na kufunga mabao matatu na kwenda Mbao FC 2019/20 akitupia mabao 15 yakiwamo mawili ya play off.

Msimu wa 2020/21 alitua Yanga na kuifungia mabao mawili kabla ya kwenda Dodoma Jiji alikocheza misimu miwili 2021/22 na kurejea msimu huu 2024/25 na kufunga jumla ya mabao matano kabla ya kutimkia Iraq, huku KMC alicheza msimu uliopita 2023/24 na kufunga mabao mabao 12.

Related Posts