Mkata. Rais Samia Suluhu Hassan ameanza ziara yake ya siku tisa Mkoa wa Tanga, ikiwa ni ya kwanza kuifanya tangu alipoapishwa kushika wadhifa huo.
Mara ya mwisho Rais Samia alitembelea mkoani humo, Machi mwaka 2021 akiwa Makamu wa Rais na ndio iliyokuwa ziara yake ya mwisho nchini akiwa na wadhifa huo.
Ziara ya Rais Samia Mkoa wa Tanga, inaanza leo, Jumapili Februari 23, 2025 na atapokewa Mkata, wilayani Handeni kwa matukio mbalimbali ya kumlaki.
Baada ya kupokewa, atazungumza na wananchi wa eneo hilo, kisha kuendelea na ratiba nyingine za ziara yake mkoani humo.
Mwananchi, imezungumza na wananchi kutoka wilaya mbalimbali ikiwamo Handeni, waliofika eneo la mapokezi kujua ipi hasa kiu yao, wanapompokea mkuu huyo wa nchi.

Mbali na kiu yake ya kumwona Rais Samia mubashara, Shaaban Mgunda anayeishi Mkata amesema anatamani kusikia kauli ya mkuu huyo wa nchi kuhusu uchumi.
Uchumi anaouzungumzia Mgunda ni ule, unaohusisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo na mbegu za mazao hasa kwao wanaojishughulisha na kilimo.
“Huku tunanunua pembejeo kwa gharama kubwa sana, tunamsubiri Rais Samia tusikie akitupa kauli ya matumaini sisi wakulima kuhusu gharama ya pembejeo,” amesema.
Lingine analosubiri Mgunda, amesema ni suluhu ya migogoro ya wakulima na wafugaji, kadhalika mipaka ya vijiji na vijiji.
Amesema ingawa Serikali iliainisha mipaka ya vijiji na vijiji tangu mwaka 2017, bado migogoro inaendelea, hivyo anasubiri kusikia kauli ya Rais Samia.
Kingine, anaamini ujio wa Rais Samia utaleta suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa eneo hilo.
Aisha Hussein, amesema anatamani kumpokea Rais Samia na kusikia kauli yake kuhusu suala la upatikanaji wa umeme katika Kitongoji cha Negelo ndani ya kata hiyo.
Mbali na hilo, amesema amejitokeza kumpokea angalau naye amwone mubashara kwa kuwa siku zote anamuona kwenye runinga.
Rehema Mudi amesema anatarajia ziara hiyo italeta msukumo katika utatuzi wa kero mbalimbali zinazoukabili Mkoa wa Tanga.
Miongoni mwa kero hizo, amesema ni uboreshaji wa barabara za vijijini kwa ajili ya kuwezesha usafirishaji wa mazao.
Vikundi mbalimbali vya vijana walioandamana kwa amani kumsubiri Rais Samia vilishuhudiwa katika viunga vya Mkata mkoani humo.

Rais Samia Suluhu Hassan alipowasili katika Uwanja wa Shule ya Msingi Mkata Mashariki kwa ajili ya mkutano wa hadhara na wananchi wa Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga, ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo leo, Jumapili, Februari 23, 2025.
Nyimbo za hamasa na kumsifu mkuu huyo wa nchi kwa utendaji wake, nazo zilisikika kutoka kwa waandamanaji hao, waliovalia fulana nyeupe na suruali nyeusi.
Wapo waliovalia fulana zenye nembo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na nyimbo zao, zilijikita kusifu utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Ingia toka ya magari yaliyobeba mawaziri, wabunge na viongozi wengine wa CCM na Serikali yalionekana pia katika eneo hilo la mapokezi ya Rais Samia.
Mabango pia, ni jambo lingine lililokuwepo, kila moja likiandikwa ujumbe wake, lakini zote zilibeba dhima ya kumkaribisha Rais Samia mkoani Tanga.