Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) limesema mwalimu wa madrasa aliyewachapa viboko wanafunzi wake na kupelekwa mahakamani, alijisahau na hivyo anastahili msamaha kutoka kwa wazazi.
Kauli hiyo imetolewa na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuber, leo Jumapili, Februari 23, 2025, alipozungumza kwenye fainali za mashindano ya Dunia ya Quran Tukufu 2025 yaliyofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
“Alijisahau tu, sio kwamba hajui na hakukusudia. Mimi, kwa niaba ya baraza, naomba wazazi wamsamehe mwalimu huyu, kwani ghadhabu ikimpata mtu, wakati mwingine hata akili na busara vinaondoka,” amesema Mufti.
Februari 19, 2025, mwalimu huyo wa madrasa, Musa Bashiru Musa (24), ambaye picha za tukio hilo zilienea kwenye mitandao ya kijamii, alikamatwa baada ya kuonekana akiwachapa viboko wanafunzi wake kwa mikono na makalioni.
Musa, mkazi wa Mbagala Kiburugwa, jijini Dar es Salaam, alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke kujibu mashtaka ya ukatili dhidi ya watoto wawili wa madrasa.
Mufti ameongeza kuwa anawaomba wazazi wamsamehe na kusema anatarajia mwalimu huyo aachiwe ili arudi katika shughuli zake.
“Niwasihi walimu waangalie namna ya kukaa na wanafunzi, kwani mwanafunzi ni mtoto wa mwalimu na ni mrithi wake. Anapaswa kurithi tabia nzuri, asije akarithi kupiga fimbo zaidi,” amesema Mufti.
Ameisisitiza kuwa Bakwata imeanzisha utaratibu maalumu wa kuwafundisha na kuwanoa walimu, ili kuhakikisha wanazingatia maadili bora katika malezi ya watoto.